Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu ambaye
alikuwa mgeni rasmi wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha
Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) akikata utepe kuashiria uzindunzi wa
maadhimisho ya chuo hicho kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake katika hafla
iliyofanyika Dar es salaam.
Viongozi
mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo
cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiangalia moja ya picha ya
kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopigwa wakati
akifungua Chuo hicho Januari, 1965. Kutoka kushoto ni Mkuu wa chuo hicho Prof.
Emanuel Mjema, Mh. Musa Zungu (Mb) jimbo la Ilala,Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu
Pinda,Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga na Prof.Eliuta
Mwageni Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha.
Viongozi
mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo
cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiwa katika picha ya pamoja
wakiongozwa na Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu na Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu
Pinda (katikati). Nyuma ni bango lenye picha ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopigwa wakati akifungua Chuo hicho mwaka
1965.
Mke wa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda kwa niaba ya
wanafunzi waliosoma katika chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam akizungumza
na wadau na wanajumuiya wa Chuo hicho wakati wa
uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo.
Mkuu wa
Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) akiwaongoza
wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50.
Mke wa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda (katikati) akizungumza akizungumza jambo na Mwenyekiti
wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Mathew Luhanga
(kushoto).Wengine Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema.
Baadhi ya
Wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam wakiendelea na shughuli
mbalimbali chuoni hapo.
Mkuu wa
Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) akiwakaribisha
wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya
uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50.
Wadau
mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo Cha
Elimu ya Biashara wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi
wa maadhimisho.
Kikundi
cha ngoma kutoka Jeshi la Polisi kikiongozwa na Afande Juma Boha Mnyaa kikitoa
burudani ya ngoma ya asili ya ya Kibati kutoka Kusini Pemba wa uzinduzi wa
maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es
salaam.
Na.Aron Msigwa
–MAELEZO.
Dar es
salaam.
Chuo cha Elimu ya
Biashara Dar es salaam (CBE) kimezindua rasmi maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake
huku wadau na wanafunzi waliohitimu chuoni hapo katika fani mbalimbali wakipongeza
hatua iliyofikiwa na chuo hicho katika utoaji wa elimu bora nchini.
Akiwakaribisha wadau
mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo hicho waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho hayo leo
jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuukumbuka na
kuenzi mchango mkubwa alioutoa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
katika kufanikisha kuanzishwa kwa chuo
hicho.
Amesema msingi wa kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965
unatokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa wataalam katika nyanja za biashara na
sekta ya uendeshaji viwanda uliokuwepo nchini
Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wataalam wengi
katika fani za Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na
Ugavi , Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameweza
kuhitimu na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake mgeni
rasmi wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu akizungumza
akizindua maadhimisho hayo ameeleza kuwa
mchango wa chuo hicho unaendelea kuonekana kutokana na baadhi ya wahitimu wa
chuo hicho kushika nyadhifa za juu za kitaifa na kimataifa.
Amesema wataalam
waliopitia katika chuo hicho wamekuwa chachu ya shughuli za maendeleo
serikalini, viwandani ,taasisi za elimu , afya na taasisi za fedha.
“Ndugu zangu ni ukweli
usiopingika, chuo cha Elimu ya Biashara kimefanya mengi yanayohusu utoaji wa elimu
ya biashara kwa watanzania baadhi yao wamekuwa maarufu na wameshika nyadhifa za
juu ndani na nje ya nchi”
Mh. Zungu ametoa wito
kwa uongozi na wataalam wa chuo hicho kuimarisha tafiti mbalimbali hasa katika
eneo la sekta ya biashara kwa lengo la kuendelea kutoa mchango kwa maendeleo ya
jamii na taifa hasa katika eneo la ujasiriamali, vipimo na mizani ,utumiaji
bora na salama wa huduma za kifedha za ki-elektroniki na uboreshaji wa
miundombinu ya chuo hicho.
Aidha, ameiomba
serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kutoa kipaumbele katika
kushughulikia ustawi wa Chuo hicho ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu, vyumba vya
madarasa, maabara za kisasa na ofisi.
Naye mwenyekiti wa Bodi
ya Uongozi wa Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga akizungumza wakati wa uzinduzi wa
maadhimisho hayo amesema kuwa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho
yataambatana na shughuli mbalimbali kwa lengo la kukitangaza chuo hicho pia
kukusanya fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya chuo.
Amezitaja shughuli hizo
kuwa ni pamoja na uandaaji wa chakula cha hisani, kuandaa machapisho, kutoa
mafunzo ya muda mfupi ya elimu ya biashara kwa watu mbalimbali wakiwemo
wajasiriamali na uuzaji wa vitu mbalimbali.
Aidha, ameeleza kuwa
tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 mafanikio mbalimbali yamepatikana
yakiwemo ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kujiunga na masomo
hadi kufikia kutoka 25 pindi chuo kinaanzishwa hadi 14000 wa sasa, ongezeko la
kampasi kutoka 1 hadi kufikia 4.
Mafanikio mengine ni
kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia shahada, kuongezeka
kwa wakufunzi wenye shahada ya uzamivu (PhD) chuoni hapo pamoja na chuo hicho kuanzisha ushirikiano wa
elimu na vyuo vikuu vingine vilivyo nje
ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern Finland katika utoaji wa mafunzo ya
shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.
Kwa upande wake mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mama Tunu Pinda akizungumza kwa niaba ya wanafunzi waliosoma katika chuo
hicho amepongeza hatua ya chuo hicho kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa
kwake na kubainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake chuo hicho kimetoa wataalam
wengi.
“Ninapofika chuoni hapa
ninafarijika sana kwa sababu mafanikio yangu kielimu yameanzia hapa nawaomba
wanafunzi mnaoendelea na masomo muwe mabalozi wazuri wa chuo hiki mkiwa hapa
chuoni na baadaye mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu” Amesisitiza Mama
Pinda.
Aidhaa, ametoa wito kwa
viongozi wa chuo hicho kusimamia rasilimali za chuo hicho kwa kuwatumia
wataalam wenye sifa wanaozalishwa chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment