
Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali
mstaafu Fabian Massawe akitoa ufafanuzi namna Serikali livyojipanga kukabiliana
na ugonjwa wa Ebola mkoani humo kwa kuongeza vifaa kinga na
kuwawezesha kielimu wataalam wa afya wanaofanya kazi ya uchunguzi wa
dalili za ugonjwa huo walioko katika vituo vya ukaguzi mpakani.
Afisa Afya
wa Kituo cha ukaguzi cha Kabanga, mpakani mwa Tanzania na Burundi Bw. Amos Mangaluke akipitia fomu
zilizojazwa na raia kutoka nje ya nchi
wanaotumia mpaka huo kufuatia zoezi la uchunguzi wa dalili za awali za
ugonjwa wa Ebola linalofanyika kituoni hapo.
Ofisi ya
Uhamiaji ya Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Kizuizi cha
magari katika mpaka wa Kabanga unaotenganisha Tanzania na Burundi, Wilayani
Ngara.
MKOA WA KAGERA WACHUKUA
TAHADHARI DHIDI YA EBOLA.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Kagera.
Mkoa wa Kagera umechukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa
kuongeza nguvu katika udhibiti na ukaguzi wa raia wa kigeni kutoka nchi za
Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaoingia nchini Tanzania
kupitia vituo vya mpakani vya mkoa huo.
Akizungumza katika
mahojiano maalum wilayani Ngara, Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian
Massawe amesema kuwa kufuatia hali hiyo serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii imeongeza vifaa kinga na kuwawezesha kielimu wataalam wa afya walioko katika hospitali za
mkoa huo na vituo vya ukaguzi mpakani.
Amesema kuwa mkoa huo
kijiografia unapakana na nchi tatu zikiwemo Uganda kwa upande wa Kaskazini,
Rwanda na Burundi kwa upande wa magharibi na kuongeza kuwa mkoa kupitia kamati
za Afya na wataalam wa afya walioko maeneo yote ya vituo vya ukaguzi wanafanya
kazi zao ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa kila anayeingia nchini kupitia vituo
hivyo anachunguzwa dalili za Ebola.
“Mkoa wa Kagera kama
tunavyojua unapakana kwa karibu sana na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda, kuna
mwingiliano mkubwa sana wa watu kutoka eneo moja kwenda jingine hapa lazima
tuchukue tahadhari kubwa , ninawahakikishia wananchi kuwa tumejipanga vizuri katika kuimarisha uchunguzi
kupitia kamati zetu za afya” Amesisitiza.
Amesema kufuatia uwepo
wa ugonjwa huo katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uongozi
wa mkoa kupitia kamati ya Afya na ile ya Ulinzi na Usalama unaendelea kuwaelimisha
wananchi kupitia vituo vya mbalimbali vya radio vya mkoa huo kuhusu dalili za
ugonjwa huo , namna ya kujikinga na namna ya kutoa taarifa kwa mamlaka husika
endapo watabaini mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Kwa upande wake Afisa
Afya wa Kituo cha ukaguzi cha Kabanga, mpakani mwa Tanzania na Burundi Bw. Amos Mangaluke akizungumzia hali ya
ukaguzi wa raia wanaoingia nchini kupitia mpaka huo amesema kuwa zoezi la uchunguzi wa dalili za awali za
ugonjwa wa Ebola linafanyika kwa ufanisi mkubwa kufuatia kituo chake kuwa na
vifaa kinga vinavyomsaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema takribani watu
500 wanaotumia mpaka huo wa Kabanga huchunguzwa
afya zao kwa siku ambapo hujaza fomu maalum ya taarifa ambayo hutumiwa na wataalam wa afya kituoni
hapo.
No comments:
Post a Comment