Na Anna Nkinda –
Maelezo
30/8/2014 Jamii
imetakiwa kushirikiana kwa pamoja kuwalea watoto yatima na wanaoishi katika
mazingira hatarishi kwani wengi wao hawana wazazi na walezi wao hawana uwezo wa
kuwapatia mahitaji yao ya msingi ikiwemo elimu.
Mwito huo umetolewa leo
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye hafla fupi ya
kuwapongeza walimu wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyofanyika katika
viwanja vya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) jijini Dar es Salaam.
Walimu hao wa shule ya
Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambayo ni ya
watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu walipongezwa kwa kazi
wanayoifanya ya kuwafundisha na kuwalea watoto hadi kumaliza kidato cha nne na
kufanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA ambayo ndiyo wamiliki wa shule hiyo alisema
bila kuwa na juhudi za dhati na za pamoja watoto wengi wa kundi hilo watakosa
elimu ya Sekondari hali ambayo itawanyima fursa ya kujikwamua katika mzunguko
wa umaskini.
“Napata faraja kubwa
moyoni mwangu kwa mafanikio haya na ninaamini mtaungana nami kuwasaidia watoto
yatima na wanaotoka katika mazingira magumu popote pale walipo, nawakaribisha
mlee watoto wenu na kuchangia katika uendelezaji wa huduma hii muhimu”.
Ili kuhakikisha mradi
huu unakuwa endelevu tumeanzisha program ya wanafunzi wanaolipa ada ili kuweza
kupata rasilimali za kuwasomesha watoto wengi zaidi wasio na uwezo”, alisema
Mama Kikwete.
Kwa upande wa walimu aliwapongeza
kwa kazi wanayoifanya ya kuwalea watoto hao ambao wanahitaji msaada wa malezi
na juhudi za umakini mkubwa katika
kufundishwa ili waweze kufuzu na kuwataka waendelee na moyo huohuo huku wakifuata
maadili yao ya kazi kwani wao ni kama wazazi.
Aidha Mwenyekiti huyo
wa WAMA aliwashukuru wadau mbalimbali ambao wanatoa misaada katika shule hiyo
ambapo hadi sasa wanafunzi 431 hii
inamaana kuwa waliopo shuleni ni 363 na 68 waliomaliza kidato cha nne mwaka
jana wamesajiliwa katika shule ya WAMA-Nakayama.
Akiongea kwa niaba ya
mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mecky Sadick, Mkuu wa wilaya ya Ilala Raymond
Mushi aliwapongeza wadau wote wanaotumia rasilimali zao kuwasaidia watoto hao ambao
wameweza kupata elimu bure ambayo ni
mkombozi wa maisha yao.
Mushi alisema, “Ukiona
kuna watu wanahangaika kwa ajili ya maisha ya watoto ambao ni wahitaji hapo
kuna njia kwa watoto hao ya kuwa na maisha mazuri hapo baadaye kwani vijana ni
rasilimali ya taifa, jambo la muhimu ni kuendelea kutoa michango kwa WAMA ili
kesho iwe nzuri kwa watoto hawa,”.
Kwa upande wa wadau wa ndani wanaoisaidia shule
hiyo walimpongea Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasaidia watoto
hao na kuahidi kuendelea kushirikiana nanye ili kuhakikisha kuwa watoto hao
wanapata elimu sawa na watoto wengine .
Naye Kaimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Suma Mensah
alimshukuru Mama Kikwete kwa ushirikiano na ushauri anaoutoa kwa walimu hao
jambo ambalo limesababisha walimu kufanya kazi kwa bidii na kujituma nahivyo wanafunzi
kufanya vizuri katika masomo yao.
Taasisi ya WAMA
ilianzisha shule hiyo ili kutoa mchango katika juhudi za taifa za kumkomboa
mwanamke. Katika hilo wamelenga kutimiza malengo waliyojiweka ya kuwapatia
fursa za elimu ya Sekondari watoto wa kike wanaotoka katika mazingira magumu
wakiwemo yatima.
Kwa mara ya kwanza mwaka
jana wanafunzi 68 wa kidato cha nne walimaliza katika shule hiyo na katika
matokeo ya mtihani wa taifa hakuna mwanafunzi
aliyefeli. Wanafunzi 10 walipata daraja la kwanza, 20 walipata daraja la pili,
19 daraja la tatu na 19 daraja la nne.
Hadi sasa Taasisi hiyo
imeweza kusaidia watoto zaidi ya 1000 kupata fursa ya elimu ya Sekondari na
watoto 14 kupata ufadhili wa vyuo wa asilimia 100 katika fani mbalimbali.
No comments:
Post a Comment