1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19. Bajeti hii
inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na Sheria ya Bajeti namba
11 ya mwaka 2015 kifungu cha 26.
2.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vya bajeti. Kitabu cha
Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya
Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali;
Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya
Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha
wa mwaka 2018 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2018
ambayo ni sehemu ya bajeti hii.
3.
Mheshimiwa Spika, ni heshima kubwa na upendeleo wa hali ya juu
kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha bajeti ya tatu ya Serikali ya
awamu ya tano. Hivyo, namshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia
nchi yetu neema nyingi, utulivu na amani na kwa kuniwezesha kuwasilisha bajeti kuu
ya Serikali kwa wananchi wa Tanzania kwa mara ya tatu. Pili napenda kumpongeza kwa
dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, kiongozi wetu shupavu; kiongozi anayeaminiwa na kutumainiwa na
wananchi, hasa wanyonge; kiongozi anayechukia na kupiga vita rushwa, ufisadi na
ubadhirifu wa mali za umma kwa vitendo; na Rais anayejipambanua kwa kufanya
maamuzi magumu ya kulinda rasilimali za Taifa. Ninampongeza kwa kazi kubwa
ambazo ameendelea kuzifanya tangu aliposhika hatamu za uongozi wa Taifa letu,
ambazo zimepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa sana katika kipindi kifupi
cha miaka miwili na nusu tu ya utawala wake. Napenda niyataje mambo kumi tu aliyothubutu
kutenda na kuiletea nchi mafanikio makubwa:
(i)
Kuhamishia
makao makuu ya Serikali Dodoma: Ametekeleza ndoto ya Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na uamuzi wa Chama Tawala wa mwaka 1972 wa
kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma. Aidha, kwa mamlaka aliyo nayo
amepandisha hadhi ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji kuanzia tarehe
26/4/2018;
(ii)
Kujenga ukuta
kuzunguka mgodi wa Tanzanite Mirerani: Amejenga ukuta wenye mzingo wa
kilomita 24.5 kuzunguka machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani, Wilaya ya
Simanjiro uliogharimu shilingi bilioni 5.42. Lengo likiwa ni kudhibiti
uchimbaji na uuzaji holela wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee na
kuliingizia Taifa mapato. Katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi
Machi, 2018 Serikali imefanikiwa kukusanya mrabaha wa shilingi milioni 714.6.
Kati ya kiasi hicho, shilingi milioni 614.6 kilitokana na makusanyo kutoka kwa
wachimbaji wadogo. Kiasi hicho kilichokusanywa kutoka kwa wachimbaji wadogo
kinazidi jumla ya makusanyo ya mrabaha wa miaka mitatu iliyopita. Kiasi
kilichokusanywa na Serikali kilikuwa shilingi milioni 116.8 (2015), shilingi
milioni 71.8 (2016), na shilingi milioni 147.1
(2017);
(iii)
Kudhibiti
uuzaji wa makinikia nje ya nchi na kutunga sheria kuwezesha nchi kunufaika na
rasilimali zake:
Amezuia usafirishaji wa makontena 277 ya makinikia nje ya nchi yenye thamani ya
kati ya shilingi bilioni 829.4 na shilingi bilioni 1,438.8 na kuagiza kutungwa
kwa sheria mpya za mfano katika Afrika kuwezesha nchi zenye maliasili kunufaika
na rasilimali hizo. Sheria hizo ambazo zilipitishwa na Bunge lako Tukufu ni:
(a) Sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusu Umiliki wa
Maliasili ya mwaka 2017 (The Natural
Wealth and Resources - Permanent Sovereignity Act, 2017);
(b) Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu
Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017 (The Natural Wealth and Resources Contracts
(Review and Re- Negotiation of
Unconscionable Terms) Act, 2017; na
(c) Sheria ya Marekebisho ya Sheria
mbalimbali ya mwaka 2017 (The Written
Laws - Miscellaneous Ammendments ) Act, 2017.
(iv)
Kutoa elimu msingi bila ada na kuongeza bajeti ya dawa,
vifaa tiba na vitendanishi kwa zaidi ya mara nane: Ametoa elimu msingi bila ada ambapo kila mwezi Serikali inalipa shilingi
bilioni 20.8. Kutokana na hatua hiyo, uandikishwaji wanafunzi wa darasa la
kwanza umeongezeka kutoka watoto 1,568,378 mwaka 2015 hadi watoto 2,078,379
mwaka 2018. Aidha, uandikishaji wa
wanafunzi wa kidato cha kwanza nao umeongezeka kutoka wanafunzi 448,826 mwaka
2015 hadi wanafunzi 562,695 mwaka 2017. Kadhalika, ameongeza fedha za mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu ambapo mgao uliotolewa mwaka 2017/18 ni shilingi
bilioni 409.9 ikilinganishwa na matumizi halisi ya shilingi bilioni 367.4 mwaka
2015/16. Idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hiyo imeongeza kutoka wanafunzi
96,589 mwaka 2015 hadi 122,623 mwaka 2017. Katika sekta ya afya, amethubutu
kuongeza bajeti kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa
tiba na vitendanishi kufikia shilingi bilioni
269 mwaka 2017/18 kutoka shilingi
bilioni 31 mwaka 2015/16, hivyo kuimarisha huduma za afya;
(v) Ununuzi wa ndege mpya kufufua
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Amefufua Shirika la Ndege la
Tanzania kwa kufanya maamuzi magumu ya kununua ndege mpya tatu aina ya
Bombardier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja ambazo tayari ziko
nchini na zinafanya safari za ndani. Aidha, ndege kubwa
nyingine tatu (3), moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba
abiria 262 na ndege mbili aina ya
Bombardier CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja zitawasili nchini
baadae mwaka huu. Kadhalika, Serikali imekamilisha taratibu za kupata ndege ya
pili kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na
malipo ya awali yamekamilika;
(vi) Kudhibiti matumizi yasiyo ya
lazima, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi: Amedhibiti matumizi yasiyo ya lazima hususan safari za watumishi wa
Serikali nje ya nchi, kuondoa watumishi hewa 19,708 waliokuwa wanalipwa
mshahara wa jumla ya shilingi bilioni 19.8 kwa mwezi, na watumishi 14,404 wenye
vyeti vya kughushi waliokuwa wanalipwa mshahara wa jumla ya shilingi bilioni
15.5 kwa mwezi, ambazo zote hizo zimeokolewa. Aidha, chini ya utawala wake,
nidhamu katika utumishi wa umma imeimarika na ameanzisha Mahakama ya mafisadi
ili kupambana na mafisadi wanaonyonya uchumi wa nchi;
(vii) Ujenzi wa reli ya kati ya
kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard
Gauge Railway – SGR): Ameanza ujenzi wa reli ya kati
ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard
Gauge Railway – SGR). Awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro
(km 205) na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma (km 422)
tayari zinatekelezwa. Awamu zote mbili zitagharimu takriban Dola za Marekani
bilioni 3.14;
(viii) Ujenzi wa mradi wa umeme
katika bonde la mto Rufiji: Amefanya uamuzi wa kuanza
ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme katika mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao nao ulikuwa ndoto ya Baba wa Taifa utakaozalisha
MW 2,100 utakapokamilika nao umeanza katika hatua za awali;
(ix) Kuimarisha usimamizi wa mapato
ya ndani: Ametekeleza ahadi yake kwa Watanzania kuimarisha ukusanyaji wa mapato
na kudhibiti ukwepaji kodi, hatua ambazo zimewezesha Serikali kuongeza
ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi
wastani wa shilingi tirioni 1.3 kwa mwezi;
(x) Kuendeleza umeme vijijini na
kusitisha miradi ya wazalishaji binafsi wa umeme (IPPs): Ameendeleza utekelezaji wa mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini
kupitia REA Awamu ya Tatu kwa ufanisi mkubwa, ambapo ndani ya miaka miwili na
nusu ya utawala wake jumla ya vijiji 557 vimeunganishwa umeme. Vijiji hivyo vimetokana
na utekelezaji wa miradi ya REA II na
REA III ya kuongeza msongamano (densification), mkongo (backbone) na ule wa kusafirisha umeme Makambako
- Songea. Aidha, amesitisha miradi ya wazalishaji binafsi wa umeme (Independent Power Producers – IPPs) ambayo
ilikuwa inaigharimu Serikali fedha nyingi. Vile vile, bila yeye mradi wa Bomba
la Mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi bandari ya Tanga usingepatikana na tayari
ujenzi unaendelea;
4.
Mheshimiwa Spika, yapo
mambo mengi sana makubwa (barabara, meli, madaraja, maji, usimamizi wa sekta ya
fedha n.k.) ambayo Jemadari huyu ametekeleza, lakini kwa uchache wa muda siwezi
kuyataja yote. Haya yote ni ushahidi usio na mashaka kwamba Tanzania chini ya
Rais Magufuli imeshika kasi ya maendeleo. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania
kuchangia katika jitihada hizi za Mheshimiwa Rais kujenga Tanzania mpya. Maeneo
matatu ya msingi sana kwa kila mwananchi kuwajibika ni: (i) uzalendo kwa nchi
yetu; (ii) kupiga vita wizi, ubadhirifu na ufisadi; na (iii) kufanya kazi kwa
bidii na kulipa kodi.
5.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo za dhati kwa Rais
wetu, napenda kumshukuru kwa moyo wangu wote kwa kuendelea kuniamini na
kuniongoza katika kazi zangu za Waziri wa Fedha na Mipango. Hata pale
nilipoelemewa na kazi na kulaumiwa kwamba waziri huyu ni bahili mno katika
kutoa fedha na baadhi wakinipaka tope la kiburi, alinitia moyo. Niliwahi kumuuliza
Mheshimiwa Rais kwa nini alinitwika mimi kazi hii nzito kama msalaba wa zege,
tena bila matumaini ya kutokea mtu mfano wa Simon wa Kirene katika Biblia wa
kuja kunipokea mzigo huu!. Yeye alinijibu kwamba “Mungu atawatuma malaika wake watakusaidia!” na akaongeza kwamba “lazima watu wachache tuwe tayari kuumia kwa
faida ya Watanzania wengi maskini”. Naomba nikiri kuwa, majibu hayo
yalinichoma na kunikumbusha sala ya wana “Opus
Dei” katika mateso isemayo “Mapenzi
ya Mungu, yenye haki na yanayopendeza sana, yafanyike, yatimizwe, yasifiwe na
kutukuzwa kuliko vitu vyote milele. Amina. Amina.” Baada ya hapo, nilipata amani
ya kuendelea katika utumishi huu. Asante sana Mheshimiwa Rais. Najua
unasikiliza!.
6.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mama Samia
Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumsaidia
Rais kuongoza Taifa letu kwa hekima na uadilifu. Kadhalika, ninatoa pongezi kwa
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuiongoza Zanzibar kwa busara, jambo
ambalo limepelekea wananchi wa Zanzibar kuishi katika hali ya amani na utulivu
mkubwa kwa kipindi cha miaka saba na nusu sasa. Aidha, ninampongeza sana
Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye
pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, kwa kuwa kapteni hodari wa timu ya Serikali
hapa Bungeni na kwa kumsaidia Rais kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama
Tawala CCM ya mwaka 2015 – 2020. Vile vile, ninawapongeza wakuu wa mihimili
mingine ya dola, nikianza na wewe Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa kwa kuliongoza Bunge kwa
umahiri; na Mheshimiwa Profesa
Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa
Tanzania kwa kazi nzuri ya kuongoza chombo cha utoaji haki. Napenda vile vile
kumpongeza Mheshimiwa Balozi Mhandisi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia
ni mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri kwa utumishi
uliotukuka.
7.
Mheshimiwa Spika, ni vema pia
niwapongeze waheshimiwa wenza wa viongozi wakuu wa
kitaifa kwa umuhimu wao wa kipekee. Niruhusu niwataje kwa
majina yao Mwalimu Janet Magufuli,
Bwana Ameir Hafidh Ameir, Mama Mwanamwema Shein, Mwalimu Mary Majaliwa, Dkt. Fatuma
Ramadhani Mganga, na Mama Marina Papadopoulos Juma. Tunawapongeza na
kuwashukuru kwa kuwawezesha viongozi wetu wakuu wa kitaifa kutekeleza vizuri
majukumu yao kwa utulivu, hamasa na tabasamu kutokana na mapenzi makubwa
wanayopata nyumbani.
8.
Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na kuwashukuru wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na
usalama ambao ni Mkuu wa Majeshi,
Jenerali Venance Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro; Kamishna Jenerali
wa Magereza, Dkt. Juma Ali Malewa; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna
Makakala; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus Kipilimba; Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Valentino
Mlowola; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya
Bw. Rogers William Sianga; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Bw.
Thobias Andengenye. Mimi na Watanzania wenzangu tunawapongeza kwa dhati kabisa viongozi
hawa, pamoja na makamanda, askari na watumishi wote wa vyombo hivi nyeti kwa
kuendelea kuilinda nchi yetu kwa ushupavu, kudumisha amani na
usalama na kuwawezesha wananchi wote wa Tanzania kufanya shughuli za maendeleo
kwa utulivu. Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Dkt Adelardus Lubango Kilangi kwa kuteuliwa na Rais kuwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, na ninamshukuru kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya
Fedha wa mwaka 2018 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2018.
9.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii pia kutoa shukrani
mahsusi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Makamu wake Mheshimiwa Jitu V.
Soni, Mbunge wa Babati Vijijini. Maoni na ushauri uliotolewa na Kamati ya
Bajeti wakati wa kuchambua mapendekezo ya bajeti ninayoiwasilisha mbele ya
Bunge lako Tukufu, ulikuwa wa kizalendo na wenye tija. Aidha, ninawapongeza
Wenyeviti, Makamu wenyeviti na wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge kwa
michango yao waliyoitoa kupitia vikao vya kamati za kisekta katika kuboresha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19 ili kuwapatia
wananchi wa Tanzania huduma bora zaidi.
10.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyokuwa mwaka 2017/18, dhima ya
bajeti ya mwaka 2018/19 kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa
ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao chochea ajira na ustawi endelevu wa
jamii”. Bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia uhalisia wa nchi yetu ambao
sisi wote tunaufahamu, kwa maana ya changamoto kuu za kiuchumi na kijamii
zinazotukabili, fursa tulizo nazo, mafanikio hadi sasa na malengo yetu kama
Taifa. Naomba nifafanue haya kwa kifupi:
a) Changamoto
(i)
Bado tuna kiwango kikubwa cha umaskini ambapo taarifa kutoka Ofisi ya Taifa
ya Takwimu zinaonesha kiwango cha umaskini kimepungua kidogo kutoka asilimia
28.2 (2011/12) hadi asilimia 26.4 (2015/16). Matarajio ni kuwa Utafiti wa
Matumizi ya Kaya unaoendelea hivi sasa utatupatia taarifa nzuri zaidi ya
kuendelea kupungua kwa umaskini kwa kuzingatia kuwa uchumi wa Taifa umeendelea
kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.0 kwa mwaka katika miongo miwili sasa;
(ii) Ukosefu wa fursa za ajira hasa kwa vijana, ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 10.4 ya
Watanzania hawana ajira. Vile vile kati ya vijana wanaohitimu masomo yao
wapatao 800,000 kila mwaka, uwezo wa Serikali kuajiri ni wastani wa watu 40,000
tu;
(iii) Sekta ya kilimo (inayojumuisha mazao, mifugo na uvuvi) ambayo inaajiri asilimia 66 ya
Watanzania na inachangia asilimia 30 ya Pato la Taifa inaendelea kukua kwa kasi
ndogo ya wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita
kutokana na uwekezaji mdogo, tija ndogo na kutegemea mvua, sambamba na mchango
mdogo wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa wa asilimia 5.5;
(iv) Mahitaji makubwa ya upatikanaji
wa huduma muhimu za jamii (hasa maji, afya na elimu bora) na yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu (asilimia 3.1
kwa mwaka). Aidha, hali ya miundombinu ya umeme, usafiri na usafirishaji
(barabara, reli, usafiri wa anga na majini) bado haikidhi mahitaji ya uchumi
kukua kwa kasi zaidi na kugusa wananchi wengi. Mathalani, mtandao wa barabara
nchini ni kilomita 86,472 ambapo ni asilimia 9.7 tu ndiyo za kiwango cha lami.
Aidha, mahitaji ya umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani bado ni
makubwa ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji. Mitambo iliyopo kwa sasa ina
uwezo wa kuzalisha Megawati 1,424.6 ikilinganishwa na mahitaji ya zaidi ya
Megawati 3,000 ili kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa viwanda; na
(v) Wigo mdogo wa ukusanyaji wa mapato
ya ndani ambapo uwiano wa mapato ya ndani na Pato la Taifa ni takriban asilimia
15.0 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 17.0 kwa nchi za Afrika Kusini mwa
Jangwa la Sahara.
b) Fursa
11.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya bajeti hii pia yamezingatia
fursa mbalimbali tulizo nazo katika Taifa letu hususan nguvukazi kubwa ya Taifa
ambao ni vijana; rasilimali na fursa nyingi tulizonazo katika kilimo (mazao, mifugo,
na uvuvi); madini; gesi; vivutio vya utalii; viwanda vya huduma za kilimo
(agri-business); vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme; biashara na huduma
za usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
c) Mafanikio
12.
Mheshimiwa Spika, bajeti hii pia imezingatia mafanikio
tuliyopata hadi hivi sasa ambayo hatuna budi tuyaimarishe na nitayaeleza kwa
muhtasari katika sehemu ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti.
d) Malengo
13.
Mheshimiwa Spika, bajeti hii vile vile imeandaliwa kwa
kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) na Ilani ya CCM ya mwaka
2015 – 2020. Malengo makuu ni kuondokana na umaskini na kuibadilisha Tanzania kuwa
nchi ya uchumi wa viwanda na kuingia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati
(Middle Income Countries) ifikapo mwaka 2025.
14.
Mheshimiwa Spika, changamoto, fursa mafanikio na malengo
niliyoyaeleza sasa hivi lazima yaende pamoja na wajibu upande wa Serikali,
sekta binafsi, wadau wengine na mwananchi mmoja mmoja, wa kuzipatia majibu
changamoto hizo na kuchangia ipasavyo katika jitihada za kulipeleka Taifa letu
mbele. Tutafanya hivyo ikiwa kila mwananchi atafanya kazi na kutumia uwezo wake
wote kwa ajili ya maendeleo yake na ya Taifa. Aidha, ni muhimu pia tuendelee
kujenga na kutumia ubia wa kimkakati (harness
strategic partnerships). Ujumbe wangu kwa Watanzania kupitia bajeti hii ni
kuwa, lazima tuendelee kufanya chaguo gumu (tough
choices) katika kuelekeza rasilimali kidogo tunazokusanya ili tuweze kuzishinda
changamoto hizo zilizoko mbele yetu. Ukweli ni kuwa, mabadiliko ni magumu na
mara nyingi yanapingwa!. Hivyo, lazima tuwe imara, tukusudie kufanikiwa na
tutumie vizuri fursa na uwezo wa Watanzania, sekta binafsi na Serikali ili
kufikia azma yetu.
15.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba niliyosoma
leo asubuhi, nilieleza kwa kirefu hali ya uchumi wetu ilivyokuwa katika mwaka
2017, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18, mafanikio yetu
na changamoto tulizokumbana nazo na niliainisha pia maeneo ya vipaumbele kwa
mwaka 2018/19. Katika hotuba hii nitajikita zaidi katika masuala ya kibajeti,
nikianza na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18, hatua muhimu zitakazopewa
msukumo zaidi upande wa matumizi katika mwaka ujao wa fedha, maboresho ya mfumo
wa kodi na tozo mbalimbali na mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018/19.
I.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2017/18
Mwenendo wa Mapato
16.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai,
2017 hadi Aprili, 2018 mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi trilioni 21.89
sawa na asilimia 69 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi trilioni 31.71
Mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:
A.
Mapato ya Ndani
17.
Mheshimiwa Spika, Mapato ya ndani
yakijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi trilioni 14.84
ikilinganishwa na lengo la kukusanya shilingi trilioni 19.98 kwa mwaka sawa na
asilimia 74.3. Kati ya kiasi hicho, makusanyo ya kodi yalikuwa shilingi trilioni
12.61; makusanyo yasiyo ya kodi ni shilingi trilioni 1.79; na makusanyo ya
Halmashauri ni shilingi bilioni 437.6. Kutofikiwa kwa malengo ya
ukusanyaji kumetokana na changamoto
mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
(i)
Ukwepaji wa kodi;
(ii) Ugumu wa kutoza kodi wafanya biashara walioko katika sekta isiyo rasmi
kwa vile hawana sehemu rasmi na za kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi
kumbukumbu;
(iii) Mazingira yasiyo rafiki ya ulipaji kodi na mlolongo wa kodi na tozo,
hasa huduma zinazotolewa na mamlaka za
udhibiti na usimamizi (zikiwemo TBS, TFDA,
EWURA, TCRA, OSHA, Zimamoto), viwango vikubwa vya kodi; urasimu katika
taratibu za kulipa kodi, na ugumu na gharama kubwa za kulipa kodi;
(iv) Matumizi hafifu ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD);
(v) Udhaifu katika usimamizi wa uvunaji wa rasilimali za nchi hasa madini,
gesi asilia, misitu, rasilimali bahari, utalii na ardhi; na
(vi) Mchango mdogo na utegemezi wa mashirika ya umma katika bajeti ya
Serikali.
B.
Mikopo ya Ndani na Nje yenye Masharti ya Kibiashara
18. Mheshimiwa Spika, Serikali ilikopa jumla ya
shilingi trilioni 4.96 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 80 ya shilingi trilioni 6.17
zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka 2017/18. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 4.13
zilikopwa kwa ajili ya kulipia dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva
(rollover), na shilingi bilioni 832.3 zilikopwa ili kugharamia miradi
mbalimbali ya maendeleo. Aidha, Serikali ilikopa kutoka soko la nje shilingi bilioni
224 sawa na asilimia 14 ya lengo la kukopa shilingi trilioni 1.6. Fedha hizi
zimeelekezwa kwenye utekelekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati. Aidha,
mwezi Mei, 2018, Serikali ilipokea mkopo wa kibiashara kiasi cha shilingi trilioni
1.13.
C.
Misaada na Mikopo Nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo
19. Mheshimiwa Spika, misaada na
mikopo nafuu iliyopokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilikuwa shilingi trilioni
1.87 sawa na asilimia 47 ya makadirio ya mwaka ya shilingi trilioni
3.97. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 70.2 ni misaada na mikopo nafuu ya
kibajeti sawa na asilimia 7.5 ya makadirio ya shilingi bilioni 941.3, shilingi
bilioni 182.9 ni misaada na mikopo nafuu ya Mifuko ya Kisekta sawa na asilimia
33 ya makadirio ya shilingi bilioni 556.1, na shilingi trilioni
1.61 ni
misaada na mikopo nafuu ya Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 65 ya makadirio
ya shilingi trilioni 2.47.
Mwenendo wa Matumizi
20. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili 2018, Serikali imetoa jumla shilingi trilioni
21.68 sawa na asilimia 68.4 ya lengo la mwaka la shilingi trilioni 31.71. Kati
ya kiasi hicho, shilingi trilioni 16.56 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya
kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 5.63 kwa ajili ya mishahara ya
watumishi wa umma na shilingi trilioni 8.42 kwa ajili ya kugharamia Deni la
Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.
21. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2018 Serikali imetoa jumla ya shilingi trilioni 5.12 kwa ajili
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 4.35 ni fedha za
ndani na shilingi bilioni 775.8 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki
hakijumuishi fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa
moja kwenye utekelezaji wa miradi ambazo hazikupita kwenye mfumo wa malipo wa
Serikali. Fedha hizi zitajumuishwa pindi taratibu ya kiuhasibu
zitakapokamilika.
22.
Mheshimiwa Spika, naomba nieleze mafanikio
yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 katika kipindi cha
Julai 2017 hadi Aprili 2018 kama ifuatavyo:
(i)
Jumla ya shilingi bilioni 59.0
zimetolewa katika Halmashauri za Wilaya 110 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa
vituo vya afya, na shilingi bilioni 24.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali za
mikoa 24. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 125.7 zimetolewa kwa ajili ya
ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi;
(ii) Kiasi cha shilingi bilioni 156.1 kimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
ya maji mijini na vijijini;
(iii) Kiasi cha shilingi bilioni 409.9 kimetolewa kwa ajili ya miradi ya
nishati vijijini, umeme wa jotoardhi, uzalishaji wa umeme katika vyanzo
mbalimbali na usambazaji wa gesi asilia;
(iv) Katika kutekeleza azma ya kutoa elimumsingi bila ada na kugharamia
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali imetoa shilingi bilioni 618.0;
(v) Serikali imeendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu ili kupanua fursa
za uchumi, kilimo, biashara na viwanda ikiwemo barabara zinazounganisha mikoa
na nchi jirani, barabara zinazopunguza msongamano katika majiji, barabara za
vijijini, reli, viwanja vya ndege, na bandari. Katika eneo hili kiasi cha
shilingi trilioni 1.87 kimetolewa; na
(vi) Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai ya watumishi umma,
wazabuni, wakandarasi na watoa huduma ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.17 kimelipwa.
23.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea
kuchukua hatua nyingine zenye lengo la kuimarisha usimamizi wa bajeti ya
Serikali kama ifuatavyo:
a)
Deni la Serikali
24.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Deni
la Serikali linadhibitiwa na linaendelea kuwa himilivu, Serikali inaendelea
kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134. Aidha, Serikali
inatekeleza Mkakati wa Muda wa Kati wa Kusimamia Deni unaotoa dira ya namna
bora ya ukopaji ili kuepuka gharama na athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza
katika kusimamia deni la Serikali. Katika kudhibiti kuongezeka kwa gharama za
mikopo, Serikali ilijikita zaidi kukopa kwenye mikopo yenye masharti ya kati (Semi Concessional Loans) hasa mikopo
inayowezesha uagizaji wa vifaa na mitambo kutoka nchi inayokopesha (Export Credit Agency - ECA) na pale ilipolazimu,
mikopo ya masharti ya kibiashara ilikopwa kwa uangalifu mkubwa ikiwemo
kuhakikisha kwamba mikopo hiyo inatumika kwenye maeneo ambayo yanachochea
ukuaji wa uchumi.
25.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2018,
deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 49.65 ikiwa
ni sawa na ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na shilingi trilioni 43.79 Aprili
2017. Kati ya kiasi hicho, deni la ndani
lilikuwa shilingi trilioni 14.05 na deni la nje shilingi trilioni 35.60 sawa na asilimia 71.71 ya deni lote.
Ongezeko la deni hilo limetokana na mikopo ya zamani na inayoendelea
kupokelewa yenye masharti nafuu au kibiashara na malimbikizo ya riba ya Deni la
Nje hasa kwenye nchi zisizo wanachama wa
kundi la Paris ambazo Serikali bado inajadiliana nazo kuhusu msamaha wa
madeni kulingana na makubaliano na kundi
hilo.
26.
Mheshimiwa Spika, Mikopo nafuu kutoka
Mashirika ya Fedha ya Kimataifa imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha mikopo
kutoka nje ambayo imechangia asilimia 59.6 ya deni lote la nje. Mikopo yenye
masharti ya kibiashara imechangia asilimia 28.5, wakati mikopo kutoka nchi
wahisani imechangia asilimia 11.9. Mikopo hii imetumika kugharamia miradi
mbalimbali ya maendeleo.
27.
Mheshimiwa Spika, Deni la Serikali limekuwa
likiongezeka. Hata hivyo deni hilo limeendelea kuwa himilivu na ukuaji wake
unawiana na kasi ya ukuaji wa uchumi wetu. Tathmini ya uhimilivu wa deni
iliyofanyika Novemba 2017 inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa kipindi cha muda
wa kati na muda mrefu. Uwiano wa deni kwa thamani ya sasa (present value) kwa
Pato la Taifa ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56; thamani
ya deni la nje kwa mauzo ya nje ilikuwa asilimia 81.8 ikilinganishwa na ukomo
wa asilimia 150; thamani ya deni la nje kwa mapato ya ndani asilimia 117.1
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250; ulipaji wa deni la nje kwa mapato
yatokanayo na mauzo nje asilimia 9.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20; na
ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani ulifikia asilimia 13.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20.
Napenda kusisitiza tena kwamba hakuna dhambi kwa nchi kukopa kwa busara
(prudently). Mambo ya muhimu ya kujiridhisha nayo ni kuwa mikopo hiyo inatumika
kujenga uwezo zaidi wa kuzalisha mali (productive capacity) na kurejesha mikopo
hiyo kwa kuzingatia uwezo wa uchumi kuhimili mzigo wa madeni (debt sustainability).
b)
Kudhibiti Malimbikizo ya Madai ya Serikali
28.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya
juhudi mbalimbali za kupunguza malimbikizo ya madai ikiwa ni pamoja na kutenga
fedha kila mwaka kwenye bajeti kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa; kuhimiza
uzingatiaji wa sheria na kanuni zake kama vile, Sheria ya Bajeti Na. 11 ya
mwaka 2015; Sheria ya Ununuzi wa Umma SURA 410; Sheria ya Fedha za Umma SURA
348 na kanuni zake na kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali yakiwemo Waraka
Na. 1 wa Mlipaji Mkuu wa Serikali unaotolewa kila mwaka kuhusu utekelezaji wa
bajeti na Mwongozo wa Mpango na Bajeti unaotolewa kila mwaka.
29.
Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na
changamoto hiyo ya malimbikizo ya madai, Serikali imeandaa Mkakati wa Kulipa Madeni na Kuzuia ulimbikizaji wa Madeni. Madai
yanayohusika kwenye Mkakati huo ni yale yaliyozalishwa na Wizara, Idara
Zinazojitegemea (MDAs) na
Sekretarieti za Mikoa (RSs) yakiwemo
madeni ya Watumishi, Wazabuni na Watoa Huduma, pamoja na madai ya Wakandarasi.
Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa kwa
kuzingatia mpango (roadmap) ulioandaliwa kulipa madeni
hayo hadi yatakapofikia kiwango himilivu. Katika ulipaji wa madeni, kipaumbele
kitatolewa kwa madeni yanayogusa watoa huduma wengi na yale ambayo yanaongezeka
kutokana na riba.
30. Mheshimiwa Spika, Mkakati huo unamtaka kila Afisa Masuuli kushiriki kikamilifu katika
utekelezaji wake ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kudhibiti malimbikizo
ya madai na kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati. Hivyo, katika kuhakikisha
kwamba hakuna madeni mapya yanayozalishwa, kila Afisa Masuuli atapaswa
kuzingatia yafuatayo:
(i)
Mikataba yote ya ujenzi wa
miundombinu inazingatia viwango vya bajeti vilivyowekwa katika kila Fungu.
Aidha, Fungu husika lisiingie mikataba nje ya viwango hivyo bila kibali cha
Mlipaji Mkuu wa Serikali; vile vile Kifungu cha 51(1) na (2) cha Sheria ya Bajeti
ya 2015 kinaelekeza kwamba miadi yote ya miaka zaidi ya mmoja (Multi-year Commitments) lazima ipate
idhini ya Waziri wa Fedha ikiwa imezingatia viwango vya bajeti, malipo ya miadi
hii isizidi viwango/bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, pamoja na kulipa madai baada
ya uhakiki;
(ii) Kutoa kipaumbele kwa ukamilishaji wa miradi inayoendelea kabla ya
kuanzisha miradi mipya, sambamba na kuhakikisha kwamba miradi inayoanzishwa
inatengewa fedha katika bajeti;
(iii) Maafisa Masuuli kutoingia makubaliano ya kupatiwa huduma au bidhaa bila
ya kuwa na fedha au kibali cha maandishi kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali;
na miadi yoyote ni lazima iingizwe kwenye mtandao wa IFMS;
(iv) Madai ya watoa huduma wote na Wakandarasi lazima yafanyike baada ya
kupata hati za ununuzi (LPO) kutoka
kwenye mfumo wa IFMS iliyozingatia
bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, pamoja na kuwepo kwa ridhaa ya matumizi (Exchequer Issue Notification) kwa
vifungu husika vya matumizi. Hivyo, Serikali inasisitiza kwamba, LPO zilizotoka
kwenye mfumo wa Malipo ya Serikali (IFMIS)
ndiyo zitumike kama msingi wa malipo kwa Watoa Huduma; na
(v) Kuzingatia matumizi ya Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 na waraka wa
Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu utekelezaji wa bajeti.
II.
SERA ZA BAJETI
KWA MWAKA 2018/19
Shabaha za Uchumi Jumla na
Bajeti
31.
Mheshimiwa Spika, Shabaha za uchumi jumla na
bajeti katika kipindi cha mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:-
(i)
Pato la Taifa kukua kwa
asilimia 7.2 mwaka 2018 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.1 mwaka 2017;
(ii) Mfumuko wa bei kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja;
(iii) Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19
kutoka matarajio ya asilimia 15.3 mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia
15.6 mwaka 2016/17;
(iv) Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.6 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19
kutoka matarajio ya asilimia 13.0 mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia
13.3 mwaka 2016/17;
(v) Matumizi ya Serikali kufikia asilimia 24.5 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia
23.0 mwaka 2017/18 na matumizi halisi ya
asilimia 22.2 mwaka 2016/17; na
(vi) Nakisi ya bajeti kufikia asilimia 3.2 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19
kutoka matarajio ya asilimia 2.1 mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia 1.5
mwaka 2016/17.
Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato
32. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza
na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, sera za mapato kwa mwaka 2018/19
zitalenga katika kuongeza wigo wa kodi, kuimarisha usimamizi wa vyanzo
vilivyopo hususan katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki na hatua nyingine
za kiutawala.
33.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza wigo wa kodi, yapo maeneo
makuu mawili yatakayozingatiwa na Serikali ambayo ni kurasimisha sekta isiyo
rasmi na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kupata vyanzo vipya vya mapato
vitokanavyo na uwekezaji huo. Zipo hatua za urasimishaji zilizoanza kufanyika
mfano uthaminishaji wa majengo, na upimaji wa viwanja, zoezi ambalo linaendelea
nchi nzima. Serikali itaongeza kasi ya urasimishaji ikiwa ni pamoja na kuwepo
na mbinu bunifu, rafiki, shirikishi na za kimkakati.
34.
Mheshimiwa Spika, mazingira bora ndio
msingi mkuu wa kuvutia biashara na uwekezaji ikiwemo kuboresha miundombinu
msingi, vivutio vya kikodi, sera zisizobadilika (policy consistency and predictability), upatikanaji wa ardhi na
taratibu za kisheria na usimamizi. Pale mazingira yanapokuwa mazuri, uwekezaji,
uzalishaji, ajira na miamala ya kibiashara inaongezeka na hivyo kupelekea kuongezeka
kwa vyanzo vipya vya mapato.
35.
Mheshimiwa Spika, uchambuzi uliofanywa na
Serikali mwaka 2017/18 ulibaini changamoto zifuatazo kuhusiana na mazingira ya
biashara na uwekezaji :
(i)
Migongano ya sheria, kanuni na
taratibu zinazotumiwa na mamlaka mbalimbali;
(ii) Gharama kubwa za kuanzisha na
kuendesha biashara kutokana na wingi wa kodi, ada na tozo zinazoambatana na
taratibu ngumu na nyingi zenye urasimu
usio na tija na hivyo kutoa
mianya na mazingira ya rushwa; na
(iii) Muingiliano wa majukumu na wingi wa mamlaka za udhibiti katika
kuidhinisha na kutoa hati, vibali na vyeti kwenye shughuli za uwekezaji na
biashara.
36.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uchambuzi
huo, Serikali imeandaa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve
Business Environment for Tanzania). Miongoni mwa mapendekezo ya Mpango huo
ambayo yatatekelezwa kwa nguvu zaidi kuanzia mwaka ujao wa fedha (2018/19) ni kurahisisha taratibu za kulipa
kodi, tozo na ada mbalimbali, na kupunguza muda na mlolongo mrefu wa kusajili
makampuni na biashara. Serikali ya Awamu ya Tano inaamini kuwa maendeleo
endelevu yatapatikana kwa haraka zaidi katika mazingira yenye ushirikiano wa
kweli na wa dhati kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
37.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato vilivyopo,
Serikali itaendelea na zoezi la uunganishaji wa Wizara, Idara,
Wakala, taasisi na mashirika ya umma kwenye Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki
wa ukusanyaji wa mapato (Government electronic Payment Gateway -GePG) ili kuboresha ukusanyaji na
kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali. Mfumo huu
ulianzishwa mwaka 2017 na kupitishwa na Bunge kupitia marekebisho ya Sheria ya
Fedha za Umma SURA 348 ambayo iliziagiza taasisi zote za Serikali kukusanya
mapato kwa kutumia Mfumo wa GePG. Hadi
mwezi Mei, 2018, jumla ya taasisi 234 zinazokusanya maduhuli zikijumuisha
Halmashauri zote 185 zimeunganishwa kwenye Mfumo huu. Nachukua fursa hii
kuagiza Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara, Idara na Taasisi zote za
Serikali zilizobaki zihakikishe kwamba zimeunganishwa na kuanza kutumia mfumo
wa GePG kabla ya Juni, 2019. Mbali na
Mfumo huu, ninawakumbusha Maafisa Masuuli wote kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa
maduhuli unafanyika kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) pamoja na benki
na siyo risiti za kuandikwa kwa mkono.
38.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hatua nyingine za kiutawala za kuongeza
mapato ya Serikali, ninaelekeza yafuatayo:
(i)
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ichukue hatua za makusudi za kuboresha mahusiano kati yake na walipa
kodi kwa lengo la kuondoa dhana
iliojengeka miongoni mwa walipa kodi kuwa TRA inatumia nguvu na vitisho
kudai kodi;
(ii) Ofisi ya Msajili wa Hazina iimarishe
usimamizi na ukaguzi kwenye
kampuni ambazo Serikali ina hisa ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata gawio
stahiki katika uwekezaji wake; na
(iii) Mamlaka za Serikali za Mitaa zijielekeze kwenye miradi itakayochochea
upatikanaji wa mapato katika mamlaka hizo hususan viwanda, masoko na machinjio
ya kisasa, stendi za mabasi, stendi za maegesho ya malori kwenye mipaka na nchi
jirani na maghala ya kuhifadhi nafaka.
Kuimarisha
Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo
39.
Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu imekuwa ikipungua kutoka wastani wa asilimia 26.3
ya bajeti halisi ya mwaka 2010/11 hadi asilimia 10.4 mwaka 2016/17. Kutokana na
umuhimu wa kuwa na maendeleo endelevu na kuhakikisha kuwa misaada na mikopo
nafuu inapatikana kama ilivyoahidiwa na
kwa wakati, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendelo na wadau wengine
imekamilisha Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework - DCF). Mwongozo huo
uliidhinishwa na Serikali mwezi Agosti 2017 na umebainisha:
(i)
Misingi ya jumla ya kuongoza ushirikiano
ambayo ni pamoja na Serikali kuongoza michakato ya kuibua vipaumbele vya miradi
ya maendeleo; na
(ii) Mfumo wa majadiliano ambao uko katika ngazi tatu; Majadiliano ya Kitaifa
ya Kimkakati, Majadiliano ya Kisekta na Majadiliano yenye Mwelekeo wa Kisiasa.
Sera za
Matumizi
40.
Mheshimiwa Spika, sera za matumizi katika
mwaka 2018/19 zitajumuisha:
(i)
Kudhibiti nakisi ya bajeti isizidi asilimia 3.2 ya
Pato la Taifa;
(ii)
Kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele na yenye
tija ili kuchochea ukuaji wa kilimo na viwanda, kupanua fursa za ajira, kujenga
na kuboresha miundombnu ya uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za
jamii;
(iii)
Kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na
kuendelea kupunguza matumizi yasiyo ya lazima; na
(iv)
Kudhibiti ulimbikizaji wa madai.
41.
Mheshimiwa Spika, Katika kusimamia sera hizi,
Serikali itachukua hatua zifuatazo:
(i)
Kuwachukulia hatua za
kisheria, kinidhamu na kiutawala wote watakaothibitika kwenda kinyume na sheria
na kanuni zinazoongoza utendaji katika nafasi zao. Napenda niwakumbushe tena kuwa kula fedha za miradi ya wananchi ni sawa
na kula sumu – wasijaribu!!
(ii) Kuhakikisha kuwa Maafisa Masuuli hawaingii mikataba bila kuwa na uhakika
wa upatikanaji wa fedha au ridhaa ya Mlipaji Mkuu wa Serikali na kuzuia
matumizi na ahadi (commitments) za
matumizi nje ya mfumo wa “IFMS”. Lengo ni kudhibiti ulimbikizaji wa madai;
(iii) Kuwianisha matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi;
(iv) Kulipa madai mbalimbali yaliyohakikiwa;
(v) Kuhakikisha kuwa ununuzi wa umma unawiana na thamani ya fedha
itakayotumika; na
(vi) Kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma ili zitumike kama ilivyokusudiwa.
Maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2018/19
42.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyoainishwa
katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 ambao niliuwasilisha leo
asubuhi, bajeti ya matumizi katika mwaka 2018/19 itaweka mkazo zaidi katika
uendelezaji wa miradi ya kielelezo; kufungamanisha maendeleo ya watu; na ujenzi
wa mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na uendeshaji biashara.
43.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya kipaumbele
katika bajeti hii ni yafuatayo:
(i)
Kilimo:
Fedha zitaelekezwa zaidi kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, maghala na
masoko, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo, kupanua huduma za
ugani, kuboresha mfumo wa utafiti na utoaji wa matokeo ya utafiti kwa wananchi,
na uendelezaji wa sekta ndogo za uvuvi na mifugo. Mkazo umewekwa katika sekta
hii kwa kuzingatia kuwa inategemewa na wananchi wengi na ndiyo itakayotupatia
malighafi kwa ajili ya viwanda, kutuhakikishia usalama wa chakula na kuongezeka
kwa kipato cha wananchi;
(ii) Viwanda: Katika kuchochea
ukuaji wa viwanda nchini, Serikali itaelekeza nguvu zake kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara ili
kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi hususan viwanda vya nguo, ngozi na nyama,
samaki, mafuta ya kula, madawa na vifaa tiba, vyakula vya binadamu na mifugo,
na katika sekta ya madini. Aidha, uendelezaji wa viwanda na kilimo utapaswa
kuzingatia uendelevu wa mazingira;
(iii) Huduma za Jamii: Maji:
Eneo lingine muhimu ni kuongeza upatikanaji na usambazaji wa maji safi hasa
vijijini na uondoshaji wa majitaka, uchimbaji wa visima katika maeneo kame
nchini na ujenzi wa mabwawa makubwa ya kimkakati. Elimu:
Serikali itaendelea kugharamia elimu msingi bila ada, kuongeza idadi ya
wataalam katika fani adimu kwenye maeneo ya madini, mafuta na gesi, madaktari
bingwa (moyo na figo) pamoja na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya
juu.
Afya: rasilimali fedha zitaelekezwa kuongeza usambazaji wa dawa, vifaa
tiba, vitendanishi na uboreshaji wa huduma katika vituo vya afya, zahanati
na hospitali za rufaa. Vile vile katika mwaka ujao wa fedha, Serikali
itaelekeza fedha zaidi za LGCD kwenye
miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri hususan miradi ya elimu na
afya. Aidha, Serikali itaweka msukumo kuimarisha upatikanaji wa lishe bora kwa mama na mtoto hususan katika
siku 1,000 za mtoto tangu kutungwa kwa mimba ili kuondokana na changamoto ya
kuwa na watoto wenye udumavu na hivyo kukua vema kimwili na kiakili. Aidha,
mahitaji ya makundi maalum katika
jamii yetu (wanawake, vijana, watoto, watu wenye ulemavu na wazee) yataendelea
kuangaliwa kipekee;
(iv) Kujenga na
kukarabati miundombinu wezeshi
hususan kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali, kuendelea
na ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa na zile za
vijijini, na kuimarisha usafiri wa anga na majini; na
(v) Maeneo mengine
ya kipaumbele ni: kurahisisha umiliki wa ardhi, kuimarisha huduma za mawasiliano, kifedha na utalii na kuimarisha ulinzi,
usalama, utawala bora, na utoaji haki.
III.
HATUA ZA MAPATO NA MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA
TOZO MBALIMBALI
Maboresho
ya Mfumo wa Kodi, Ada na Tozo Mbalimbali
44.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwasilisha
mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo kurekebisha baadhi
ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na pia
taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya
yanalenga pamoja na mambo mengine, kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan
katika sekta ya Viwanda, Utalii, kukuza ajira, na kuongeza mapato ya Serikali.
Aidha, marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuwa na mfumo wa
kodi ambao ni tulivu na wenye kutabirika. Marekebisho hayo yanahusu Sheria
zifuatazo:-
a.
Sheria
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b.
Sheria
ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c.
Sheria
ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d.
Sheria
ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290;
e.
Sheria
ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438;
f.
Sheria
ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348; na Sheria ya Benki Kuu, SURA 197;
g.
Sheria
ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
h. Sheria
zinazosimamia Bodi za Mazao;
i.
Sheria
ya Michezo ya Kubahatisha SURA 41;
j.
Marekebisho
madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
k.
Marekebisho
ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara
zinazojitegemea.
a) Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
45.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani,Sura 148 kama
ifuatavyo:-
(i)
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifungashio vya madawa ya binadamu
vitakavyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya viwanda vinavyozalisha dawa hapa
nchini. Aidha, vifungashio hivyo vitakuwa na machapisho ya majina ya kiwanda
husika cha utengenezaji madawa ili kuhakikisha kwamba vinatumiwa na viwanda
hivyo na siyo vinginevyo. Lengo la hatua hii nikupunguza gharama za uzalishaji
na kuvilinda viwanda vinavyotengeneza madawa hapa nchini ili viweze kumudu
ushindani na kuongeza uzalishaji;
(ii)
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye virutubisho vinavyotumika kutengenezea
vyakula vya mifugo (animal and poultry
feeds additives) vinavyoagizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama kwa wafugaji na kuhamasisha ufugaji bora ili kuongeza mchango wa Sekta
hiyo katika Uchumi;
(iii)
Kufanya
marekebisho kwenye kifungu cha 6(2)(a) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana na maswala ya fedha kutoa msamaha wa kodi kwa miradi ya Serikali
inayotekelezwa kwa mikopo ya kibiashara. Hivi sasa Sheria ya Kodi ya Ongezeko
la Thamani inakataza kusamehe kodi kwenye mikopo ya kibiashara hali ambayo
imesababisha kukwama kwa utekelezaji wa miradi muhimu ya Serikali kama vile
miradi ya Maji, barabara n.k. Hivyo, marekebisho yanayopendekezwa yatawezesha
utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa wakati uliopangwa;
(iv)
Kufanya
marekebisho kwenye kifungu cha 6(2)(a) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kusamehe
kodi hiyo pale ambapo kuna mkataba uliosainiwa baina ya Serikali ya Tanzania na
Taasisi ya Fedha au Benki ambayo ni “mwakilishi” wa Serikali nyingine aliyepewa
dhamana na Serikali hiyo kuingia mikataba na kusimamia utekelezaji wa miradi
husika. Hivi sasa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani inampa mamlaka Waziri
huyo kusamehe kodi pale ambapo kuna mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na
Serikali ya nchi nyingine unaotoa msamaha wa kodi. Hivyo miradi mingi
inayohusisha mikataba ya misaada au mikopo kupitia mabenki na Taasisi za fedha
imekwama utekelezaji wake. Kwa msingi huo, marekebisho haya yanalenga katika
kuondoa ukwamishaji na ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi mingi ya Serikali
inayotekelezwa kwa fedha za Washirika wa Maendeleo kupitia mikataba
inayosainiwa na Serikali yetu na Benki au Taasisi za Fedha za Serikali za nchi
nyingine; na
(v)
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taulo za kike (sanitary pads) HS Code 9619.00.10. Lengo la hatua hii ni kuwezesha
upatikanaji wa bidhaa hii muhimu kwa bei nafuu kwa ajili ya kulinda afya ya
mama na mtoto wa kike hasa watoto walio shuleni na vijijini. Ni matarajio ya
Serikali kuwa wazalishaji na wauzaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu
baada ya kusamehewa kodi hii.
Hatua hizi zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa
ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 219.1
b) Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
46.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya
Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-
(i)
Kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kupunguza kiwango cha Kodi ya
Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax)
kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2018/19
hadi mwaka 2022/23 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya madawa ya binadamu na
viwanda vinavyotengeneza bidhaa za
ngozi. Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano (performance agreement) na kila mwekezaji
ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo la hatua hii ni kuongeza
uwekezaji katika sekta ya madawa ya binadamu na usindikaji wa ngozi ambao kwa
sasa haufanyiki nchini na pia kuongeza ajira na mapato ya Serikali. Aidha,
hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza dawa hizo
kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wa madawa mengi zaidi hapa nchini;
(ii)
Kufuta
kifungu cha 10A cha Sheria ya Kodi ya Mapato kinachomkataza Waziri mwenye
dhamana ya masuala ya fedha kutoa msamaha wa kodi kwenye miradi ya Serikali
inayotekelezwa kwa fedha za mikopo ya kibiashara (non concessional loans). Lengo la hatua hii ni kumpa mamlaka
Waziri huyo kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa miradi hiyo ambayo imekuwa na
changamoto katika utekelezaji wakati Serikali inapopata mikopo ya aina hiyo; na
(iii)
Kurekebisha
Sheria ya Kodi ya Mapato ili kutoa msamaha wa Kodi ya zuio inayotozwa kwenye
riba kwa mikopo inayotolewa kwa Serikali na Benki, Taasisi za Fedha na wahisani
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Hatua hizi za
Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi milioni 220.5.
c) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
47.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya
Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya Ushuru
wa Bidhaa (specific duty rates)
zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa
bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Hata hivyo, ili kutekeleza azma ya
Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda, napendekeza kutofanya
mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa zisizo za petroli
zinazozalishwa hapa nchini na kuongeza viwango vya Ushuru wa Bidhaa zisizo za
petroli zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kama ifuatavyo:-
(i)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 61
kwa lita;
(ii)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka
nje utaongezeka kutoka shilingi 61 kwa lita hadi shilingi 64.05 kwa lita ikiwa
ni ongezeko la shilingi 3.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji
yanayozalishwa hapa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha sasa cha shilingi 58 kwa lita;
(iii)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda
yanayozalishwa hapa nchini (local juices)
hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 9 kwa lita;
(iv)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo
hayazalishwi hapa nchini (imported
juices) utaongezeka kutoka shilingi 221 kwa lita hadi shilingi 232 kwa lita
ikiwa ni ongezeko la shilingi 11 kwa lita;
(v)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo
haijaoteshwa (Beer from Local Unmalted
Cereals) hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 450
kwa lita;
(vi)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye bia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi utaongezeka kutoka
shilingi 765 kwa lita hadi shilingi 803.25 kwa lita ikiwa ni ongezeko la
shilingi 38.25 kwa lita;
(vii)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu
vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi utaongezeka kutoka shilingi 561 kwa lita hadi
shilingi 589.05 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 28.05 kwa lita. Aidha,
Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza
nguvu vinavyozalishwa hapa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha sasa cha
shilingi 561 kwa lita;
(viii)Kuanzisha Ushuru wa Bidhaa wa
shilingi 200 kwa lita kwenye mvinyo uliotengenezwa kutokana na usindikaji wa
matunda (kama ndizi, rozela/choya, nyanya, nk) yanayozalishwa hapa nchini
tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi asilimia 75;
(ix)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi
kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa
kiwango cha shilingi 200 kwa lita;
(x)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa
kiwango kinachozidi asilimia 25, utaongezeka kutoka shilingi 2,349 kwa lita
hadi shilingi 2,466 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 117 kwa lita;
(xi)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka
shilingi 3,481 kwa lita hadi shilingi 3,655.05 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la
shilingi 174.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali
vinavyozalishwa nchini hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha
shilingi 3,315 kwa lita;
(xii)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na
utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja;
(xiii)Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara
zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini
kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa
kiwango cha shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja;
(xiv) Ushuru wa
Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na (xii)
na (xiii) utaongezeka kutoka shilingi 53,235 hadi shilingi 55,896.75 kwa
kila sigara elfu moja ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,661.75 kwa kila sigara
elfu moja;
(xv)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) inayoagizwa kutoka nje
utaongezeka kutoka shilingi 26,888 hadi shilingi 28,232.4 kwa kilo, ikiwa ni
ongezeko la shilingi 1,344.4 kwa kilo; na
(xvi) Ushuru wa
Bidhaa wa ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30.
48.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kuanzisha
Mfumo Mpya wa Stempu za Kodi za kielektroniki utakaoanza kutumika tarehe 1
Septemba 2018. Mfumo mpya wa Stempu za Kodi za kielektroniki utaiwezesha
Serikali kutumia teknolojia ya kisasa kupata taarifa sahihi za uzalishaji
viwandani na kwa wakati (real time) zinazotumika kupanga mipango ya maendeleo ya
Taifa. Pia mfumo huu mpya utaiwezesha Serikali kudhibiti uvujaji wa mapato na
kutambua mapema kiasi cha Kodi ya Ushuru wa Bidhaa, Kodi ya Mapato na ile ya
Ongezeko la Thamani itakayolipwa. Aidha, mfumo wa Stempu za Kodi za
kielektroniki utadhibiti tatizo la uwepo wa stempu za karatasi za kugushi
ambalo linachangia uwepo wa bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na zinazoweza
kuathiri afya za binadamu. Mfumo huu mpya unatumika katika nchi nyingine ikiwa
pamoja na Kenya, Morocco, Uturuki, Malaysia na Switzerland na umekuwa na
mafanikio makubwa.
Hatua za Ushuru wa Bidhaa kwenye
bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
119,456.6
d) Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290.
49. Mheshimiwa Spika napendekeza kufanya marekebisho ya
Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kama ifutavyo:-
(i)
Kuongeza
kifungu cha 37A kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa ili kumpa Mamlaka Waziri
mwenye dhamana na Serikali za Mitaa Kuzitaka Serikali za Mitaa kutenga asilimia
10 ya fedha wanazokusanya kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya
kuwezesha vikundi vya vijana na wanawake. Aidha asilimia 50 ya fedha hizo
zitatengwa kwa ajili ya vikundi vya vijana na asilimia 50 kwa vikundi vya
wanawake. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI ataandaa Kanuni ambazo
zitaweka utaratibu wa kusimamia utoaji wa fedha hizo kwa vikundi vya vijana na
wanawake vilivyosajiliwa. Pia, fedha zitatolewa kwa kuwakopesha bila kutoza
riba yoyote; na
(ii)
Kurekebisha
kifungu cha 16(6) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, ambacho
kinatoa mwanya kwa Taasisi/Makampuni yanayolipa Ushuru wa Huduma kutolipa
Ushuru wa Mazao. Mfano, Makampuni mengi yanayochakata zao la mkonge ili
kuzalisha nyuzi za katani yanamiliki pia mashamba ya mkonge. Hivyo siyo busara
kuwalipisha ushuru wa mazao na ushuru wa huduma. Hata hivyo, yapo makampuni
yenye mashamba ya mkonge ambayo hayachakati mkonge, haya yanapaswa kulipa
ushuru wa mazao badala ya ushuru wa huduma. Napendekeza kiongezwe kifungu cha
16(7) kwenye Sheria hiyo kuyataka Makampuni yanayozalisha mazao na hayachakati
kwa ajili ya kuyaongezea thamani yawajibike kulipa Ushuru wa Mazao.
e) Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438
50. Mheshimiwa Spika, napendekeza
Kurekebisha Sheria ya Usimamizi wa Kodi SURA 438, ili kuanzisha utaratibu
maalum wa kusamehe kodi (Tax Amnesty) ambao unalenga kusamehe malimbikizo ya
nyuma ya riba na adhabu (Interest and Penalties) kwa kiwango cha asilimia 100.
Msamaha huo utatolewa kwa kipindi cha miezi sita (6) kinachoanzia tarehe 1
Julai 2018 mpaka tarehe 31 Desemba 2018. Aidha kwa kufanya hivyo, Serikali
inatarajia kukusanya malimbikizo ya madeni ya nyuma ya kodi (Principal Tax)
pamoja na kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiyari kwa zaidi ya asilimia 10.
Hatua hiyo ya
marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi inatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
500,000.
f)
Sheria ya
Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290, Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348 na
Sheria ya Benki Kuu, SURA 197.
51. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kurekebisha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290, Sheria ya Fedha za
Umma Sura 348, na Sheria ya Benki Kuu, Sura 197 ili kuanzisha Akaunti Jumuifu
ya Hazina (Treasury Single Account) ambapo akaunti hii itatumika kupokea fedha
zote za Serikali na kufanya malipo yote ya Serikali. Msingi wa kuanzishwa kwa
akaunti hii ni kutekeleza makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki yaliyozitaka nchi wanachama kuanzisha akaunti jumuifu ili kuimarisha
usimamizi wa fedha za Serikali. Uwepo wa akaunti hii pamoja na mambo mengine
utarahisisha usimamizi wa fedha za Serikali kwa kupunguza idadi ya akaunti
kwenye benki za biashara na Benki Kuu, kupunguza gharama za kibenki zinazolipwa
hivi sasa na Serikali kufuatia huduma zinazotolewa kwa Serikali na Benki za
Biashara, kupunguza nakisi kwenye mfuko Mkuu wa Serikali ambapo akaunti maalum
zitajumuishwa kwenye ukokotoaji wa bakaa katika Mfuko Mkuu wa Serikali tofauti
na utaratibu wa hivi sasa ambapo akaunti hizi hazijumuishwi katika ukokotoaji
huo.
g) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
ya mwaka 2004
52. Mheshimiwa Spika, kikao cha
Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti
(Pre-Budget consultations of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 4 Mei,
2018 mjini Arusha, Tanzania kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya
Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa
Mwaka 2018/19. Mapendekezo hayo yanalenga kwa kiwango kikubwa katika kuchochea
maendeleo ya viwanda ili kukuza ajira na ustawi wa jamii (Industrialization for
Job Creation and Shared Prosperity).
53. Mheshimiwa Spika, mapendekezo
ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja Ushuru wa Forodha ni kama
ifuatavyo:-
(i)
Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano (HS
Code 1001.99.00 na HS Code 1001.99.90) kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni
kuendelea kutoa unafuu kwa viwanda vya wazalishaji wa bidhaa na vyakula
vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei kwa bidhaa zinazozalishwa kwa
kutumia ngano hiyo. Aidha, hatua hii inazingatia kwamba bado kiwango cha
uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu ni kidogo katika nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki na hivyo hautoshelezi mahitaji. Ili kudhibiti uagizaji wa bidhaa hii,
utaratibu wa “Duty Remission”
utatumika ambapo viwanda vinavyotumia ngano ya aina hii katika uzalishaji
ndivyo vitakavyohusika na kutumia kiwango hicho cha msamaha wa Ushuru wa
Forodha;
(ii)
Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10
kwenye mashine za Kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali
(Electronic Fiscal Devices) zinazotambulika katika HS Code 8470.50.00 kwa mwaka
mmoja. Hatua hii inatarajiwa kuendelea kutoa unafuu na kuhamasisha
wafanyabiashara na walipa kodi kutumia mashine hizo katika kufanya mauzo na
kuongeza ufanisi katika Usimamizi na Udhibiti wa kodi;
(iii)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 15 badala
ya asilimia 25 kwenye karatasi zinazotambulika katika HS Codes 4804.11.00;
4804.21.00; 4804.31.00; na 4804.41.00. Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika ambapo wazalishaji wanaotumia karatasi
hizo katika kutengeneza madaftari na vitabu ndio watakaofaidika. Lengo la hatua
hii ni kupunguza gharama kwa wazalishaji hao. Ni matarajio ya Serikali kwamba
wazalishaji watauza bidhaa hizi kwa bei nafuu na hivyo kuwezesha watumiaji,
hususan wanafunzi, kuzipata kwa gharama nafuu;
(iv)
Kutoza
Ushuru wa forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye
karatasi zinazoingizwa kutoka nje kwa ajili ya utengenezaji wa gypsum board
(Gypsum paper for manufacturing of gypsum board) zinazotambulika katika HS Code
4805.92.00;
(v)
Kutoza
Ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 100 kwenye sukari ya
matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa
vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji hapa nchini.
Hivi sasa sukari hiyo inatozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
asilimia 100;
(vi)
Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye "Gypsum Powder" inayotambuliwa
kwa HS Code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja. Marekebisho haya yanalenga katika
kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo hapa nchini na kuhamasisha wawekezaji
watumie "gypsum"
inayopatikana hapa nchini kuzalisha "gypsum"
powder. Aidha, hatua hii inatarajiwa kuongeza ajira na mapato ya Serikali;
(vii)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye
bidhaa ijulikanayo kama "Self-adhesive
label" (HS Code 4821.10.90) ambayo hutumika kama alama ya kutambulisha
aina ya bidhaa kwa watengenezaji wa dawa za meno. Hatua hii inalenga katika
kupunguza gharama ya uzalishaji kwenye viwanda vya dawa za meno kwa kuwa
self-adhesive labels hazizalishwi hapa nchini;
(viii)Kutoza Ushuru wa Forodha wa
asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates"
(ABL) HS Code 3920.10.90 kwa mwaka mmoja. Aidha utaratibu wa “duty remission” utatumika ambapo hatua
hii itawahusu wenye viwanda vinavyoagiza bidhaa hiyo kwa matumizi ya kiwandani.
Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama ya uzalishaji kwa viwanda vya dawa za
meno. Aidha, ina lengo la kuvilinda viwanda hivi kutokana na ushindani na
ajira;
(ix)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye
mafuta ghafi ya kula ya mawese (Crude Palm Oil) yanayotambulika katika HS Code
1511.10.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kulinda na kuhamasisha
uzalishaji wa mbegu za mafuta na mafuta ya kula hapa nchini kwa kuzingatia kuwa
nchi yetu ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo. Aidha, lengo ni kuhamasisha uwekezaji katika
viwanda vya kuchakata mafuta ghafi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa hapa
nchini. Pia inatarajiwa kwamba uzalishaji wa mbegu utaongezeka na kuongeza
ajira viwandani na mashambani pamoja na kuongeza kipato cha wakulima;
(x)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 au asilimia 10 kwa mwaka
mmoja kwenye mafuta ghafi ya kula (mfano alizeti, mawese, soya, mzaituni, nazi,
karanga, mahindi n.k). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uzalishaji wa mbegu na
mafuta ya kula hapa nchini kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini. Aidha,
inatarajiwa kwamba hatua hii italinda viwanda na ajira katika sekta ndogo ya
mafuta ya kula, na kuongeza mapato ya serikali na wakulima;
(xi)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye
mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha kati na cha mwisho (semi-refined, refined/double refined oil)
mfano alizeti, mawese, soya, mzaituni, nazi, karanga, mahindi n.k. Ongezeko
hilo la Ushuru wa Forodha linatarajiwa kulinda uzalishaji wa mafuta ya kula na
kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta zinazozalishwa nchini badala ya
kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Aidha, hatua hii inatarajiwa
kupunguza fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi;
(xii)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za Kimarekani 350 kwa kila tani moja
ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye
bidhaa za chuma za misumari zinazotambulika katika HS Code 7317.00.00 (nails,
tacks, drawing pins, corrugated nails, staples other than those of heading
83.05). Hatua ya kuweka kiwango hicho cha Ushuru wa Forodha inalenga katika
kulinda viwanda vya bidhaa hizo hapa nchini kutokana na uingizaji wa bidhaa
kama hizo kutoka nje ya nchi;
(xiii) Kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti (safety
matches) vinavyotambuliwa kwenye HS Code 3605.00.00 kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa. Hatua hii inazingatia kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina
uwezo wa kuzalisha viberiti na kutosheleza mahitaji katika soko hivyo kuwepo na
umuhimu wa kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo;
(xiv) Nchi za Jumuiya
zimekubaliana kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0
kwenye malighafi ya kutengeneza bidhaa za rangi za kupaka nyumba ijulikanayo
kama “polyvinyl Alcohol” (HS Code
3905.30.00). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa
bidhaa hizo;
(xv)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kwa utaratibu wa “duty remission” kwenye malighafi (inputs) zinazotumika katika kutengeneza dawa za kuua wadudu (pesticides, fungicides, insecticides na
acaricides). Hatua hii itahusisha viwanda vinavyotumia malighafi hizo
kutengeneza dawa za kuua wadudu. Aidha, viwanda vitakavyoagiza malighafi hizo
vitatakiwa kupata kibali cha Wizara ya Kilimo. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama za uzalishaji na kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda hivyo;
(xvi) Kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa utaratibu wa duty remission
kwenye bidhaa ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama “RBD Palm Stearin” inayotambulika katika HS Code 1511.90.40. Hatua
hii inahusisha viwanda vinavyotumia bidhaa hiyo katika kutengeneza sabuni.
Aidha, hatua ya kupunguza ushuru huo imezingatia kwamba Serikali imeongeza
ushuru wa forodha katika mafuta ghafi ya mawese;
(xvii)Kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye viazi (potatoes fresh or chilled, other than
seeds) vinavyotambulika katika HS Code 0701.90.00. Lengo la hatua hii ni
kulinda uzalishaji wa viazi hapa nchini;
(xviii) Kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Chingamu (Chewing Gum) zinazotambulilka katika HS
Code 1704.10.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kwa kuwa kuna
uwezo wa kuzalisha chewing gum katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xix) Kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye peremende HS Code
1704.90.00. Hatua hii inachukuliwa kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani na
ajira;
(xx)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Chokoleti (chocolates) HS Code 18.06. Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazalisha bidhaa hizi na zina uwezo wa
kutosheleza mahitaji ya soko;
(xxi) Kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Biskuti (Biscuits) zinazotambullika kwa HS Code
1905. Hatua hii inazingatia kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina uwezo
wa kuzalisha bidhaa hiyo na kutosheleza mahitaji ya soko;
(xxii)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyanya
zilizosindikwa (tomato sauce)
zinazotambulika katika HS Code 2103.20.00. Lengo la hatua hii ni kulinda
uzalishaji wa bidhaa hiyo katika viwanda vya ndani na mashambani. Aidha,
imezingatia kwamba nchi yetu inazalisha nyanya za kukidhi mahitaji na pia kuna
umuhimu wa kusindika nyanya hizo hapa nchini ili kuongeza thamani na kuongeza
ajira katika kilimo cha nyanya;
(xxiii)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 60 badala ya asilimia 25 kwenye maji (mineral water) yanayotambulika katika HS
Code 2201.10.00. Hatua hii ni muhimu katika kuhamasisha uzalishaji na kulinda
viwanda vya hapa nchini vinavyozalisha bidhaa hiyo;
(xxiv)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyama (meat and edible meat offal in chapter 12)
kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya
uchakataji wa nyama hapa nchini na hivyo kuongeza thamani yake. Aidha,
itaongeza fursa za ajira na kipato katika sekta ya ufugaji na viwandani; na
(xxv) Kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Soseji (sausages) na bidhaa za aina hiyo (HS
Code 1601.00.00). Hatua hii ina lengo la kulinda na kuhamasisha Viwanda
vinavyozalisha bidhaa hiyo katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
54. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa
Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia
marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kama
ifuatavyo:-
(i)
Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki linalotoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari yanayotumika
kwenye mashindano ya mbio za magari (rally
cars) na kuingiza pikipiki (motorcycles)
ili nazo ziweze kupata msamaha huo. Aidha, magari na pikipiki husika
hutengenezwa mahsusi kwa ajili ya mashindano hayo. Hatua hiyo inatarajiwa
kuhamasisha mashindano hayo na kukuza sekta ya utalii;
(ii)
Kufanya
marekebisho kwenye Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ili kutoa msamaha kwa boti inayotumika mahsusi kwa ajili ya kutoa
huduma kwa wagonjwa kwenye maji (Motor
Boat Ambulance) inayotambulika katika HS Code 8903.99.10 kama vile
yanavyosamehewa magari ya kutoa huduma kwa wagonjwa (Motor Vehicle Ambulance). Hatua hii ina lengo la kupunguza gharama
na kuwezesha utoaji wa huduma za matibabu katika usafiri wa majini; na
(iii)
Kufanya
Marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari ya kubebea
watalii (Motor vehicle for Transport of
Tourists). Magari haya yanajumuisha magari ya aina mbalimbali ambayo
yametengenezwa mahsusi kwa ajili ya kubebea watalii (Motor sightseeing buses, overland trucks). Lengo la kutoa msamaha
huo ni kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya utalii, kuboresha huduma ya
usafiri kwa watalii na kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
55. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa
Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tumekubaliana kupunguza Viwango vya Ushuru
wa Forodha (duty remission) kwenye
malighafi na vipuri vinavyohitajika katika kutengeneza nguo na viatu katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, tayari nchi hizi zimewasilisha orodha ya
malighafi na vifaa vitakavyopunguziwa Ushuru wa Forodha. Uamuzi huo utaanza
kutekelezwa mwaka 2018/19.
Hatua hizi za Ushuru wa Forodha kwa
pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,630.2
h) Sheria zinazosimamia Bodi za Mazao.
56. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho kwenye sheria zote zinazosimamia Bodi za mazao mbalimbali
kwa lengo la kuwezesha ushuru wote unaokusanywa na bodi hizo kuingizwa kwenye
Mfuko Mkuu wa Serikali. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kwamba mapato
yatokanayo na ushuru unaotozwa kwenye mazao mbalimbali yanasimamiwa ipasavyo na
kutumika kwa ajili ya shughuli zilizokusudiwa. Aidha, shughuli za kuendeleza mazao pamoja na
gharama za uendeshaji wa Bodi zitagharamiwa kupitia Bajeti ya Serikali.
i)
Sheria ya
Michezo ya kubahatisha, SURA 41
57. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya mabadiliko ya kiwango cha kodi katika michezo ya kubahatisha ya
ubashiri wa matokeo ya michezo (sports
betting) kutoka asilimia 6 ya mauzo ghafi hadi asilimia 10. Lengo ni
kuongeza mapato ya Serikali kutoka kwenye sekta ndogo ya michezo hiyo ya
kubahatisha.
58. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho ya kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye mashine za michezo
ya kubahatisha (slot machines) kutoka
shilingi 32,000 hadi shilingi 100,000 kwa kila mashine kwa mwezi. Lengo ni
kuongeza mapato ya Serikali.
59. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kuongeza kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye michezo ya kubahatisha (Casino) kutoka asilimia 15 hadi asilimia
18 ya mapato halisi ambayo hupatikana baada ya kutoa zawadi (Gross Gaming Revenue -GGR). Lengo ni
kuongeza mapato ya Serikali kwa sababu kiwango cha asilimia 15 kimedumu kwa
muda mrefu kuanzia mwaka 2012.
60. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho ya kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye mashine arubaini (Forty Machines Site) za michezo ya
kubahatisha kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20 ya mapato halisi ambayo
hupatikana baada ya kutoa zawadi (Gross
Gaming Revenue -GGR). Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua hizi za marekebisho ya michezo
ya kubahatisha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 21,198.8.
j)
Marekebisho
madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali.
61. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria
mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine mbalimbali ili ziwe sanjari na
azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika
Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
k) Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa
na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
62. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na
Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi
ya ukuaji wa uchumi. Aidha, marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa
Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na Matangazo ya Serikali (Government Notices). Marekebisho hayo yatajumuisha:-
(i)
Kusamehe
Kodi ya Ardhi kwa Taasisi za Serikali kwa sababu taasisi hizi ni za umma
hazitengenezi faida. Aidha, marekebisho mengine ya ada na tozo mbalimbali
yanayohusu sekta ya ardhi yalitangazwa na Waziri mwenye dhamana ya ardhi kwenye
hotuba yake;
(ii)
Kufuta
na kupunguza baadhi ya viwango vya tozo na ada zinazotozwa kwenye sekta ya
uzalishaji wa Chumvi. Hatua hii imetokana na kuwepo kwa utitiri wa tozo na ada
zinazotozwa kwenye Madini ya Chumvi hali ambayo inasababisha gharama za
uzalishaji kuwa juu na kuwakatisha tamaa wazalishaji kuendelea na uzalishaji wa
chumvi. Hivyo napendekeza kufanya marekebisho ya tozo na ada kwenye sekta ya
uzalishaji chumvi kama ifuatavyo:-
a) Kufuta ushuru
wa mazao ya chumvi unaotozwa na Halmashauri;
b) Kufuta ada ya
ukaguzi wa madini ya chumvi (Inspection
and Clearance fee) inayotozwa kwa kiwango cha asilimia moja (1%) ya thamani
ya madini;
c) Kufuta ushuru
wa Mikoko (Mangrove Levy) unaotozwa
kwenye maeneo ya uzalishaji wa chumvi kwa kiwango cha shillingi 100,000 kwa eka
moja kwa mwaka;
d) Kufuta ada ya
kupitia andiko la mradi kwenye sekta ya uzalishaji chumvi inayotozwa na Baraza
la Taifa la Usimamizi wa Mazingira;
e) Kufuta ada ya
usajili wa Jangwa la Chumvi (Solar Salt
Panel);
f) Kufuta ada ya
Usimamizi kwenye eneo la Chumvi (Supervision
fee) inayotozwa na Wakala wa Misitu
Tanzania;
g) Kufuta ada ya
usajili wa mradi wa uzalishaji chumvi inayotozwa na Baraza la Taifa la
Usimamizi wa Mazingira;
h) Kufuta ada ya
Ukaguzi wa Mazingira (Environmental
Impact Assesment) inayotozwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
kwenye sekta ya uzalishaji chumvi;
i) Kupunguza ada
ya gharama za ukaguzi wa usalama mahala pa kazi inayotozwa kwenye sekta ya
uzalishaji chumvi kutoka shilingi millioni 2 hadi shilingi millioni 1 kwa
mwaka; na
j) Kupunguza ada
ya kibali cha kusafirisha madini ya chumvi nje ya nchi kutoka Dola za
Kimarekani 100 hadi shilingi 20,000 kwa mwaka.
(iii)
Napendekeza
kufanya marekebisho ya ada na tozo zinazotozwa na Mamlaka ya Afya na Usalama
(OSHA) mahali pa kazi kama ifuatavyo:-
a)
Kufuta
ada inayotozwa kwenye fomu ya usajili sehemu za kazi;
b)
Kufuta
tozo ya usajili sehemu za kazi;
c)
Kufuta
faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto inayotozwa kwa kiwango cha
shilingi 500,000;
d)
Kufuta
Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya afya na usalama; na
e)
Kufuta
tozo ya ushauri wa kitaalam ya usalama wa afya.
63. Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya tozo na ada zinazotozwa na
mashirika, taasisi na wakala mbalimbali ili kuendelea kuweka mazingira bora ya
kufanya biashara na kuwekeza na kuondoa kero kwa wananchi. Hii itajumuisha
kupitia upya na kuvisawazisha viwango vya tozo na ada hizo na pia kuondoa tozo
na ada za usumbufu.
l)
Tarehe ya
Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
64. Mheshimiwa Spika, hatua hizi za
kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2018, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
IV.
SURA YA BAJETI
KWA MWAKA 2018/19
65.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na sera
za bajeti kwa mwaka 2018/19, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni
32.48 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya
mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni
20.89, sawa na asilimia 64.3 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali
inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 18.0 sawa na
asilimia 13.6 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato yasiyo ya kodi yanakadiriwa kuwa
shilingi trilioni 2.16 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni
735.6.
66.
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo
wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 2.68 ambayo ni asilimia 8.2 ya bajeti
yote. Misaada na mikopo hii inajumuisha misaada na mikopo nafuu ya miradi ya
maendeleo shilingi trilioni 2.0; mifuko ya pamoja ya kisekta shilingi bilioni
125.9; na misaada na mikopo nafuu ya kibajeti (GBS) shilingi bilioni 545.8.
67.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 8.90
kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara. Mikopo ya ndani
inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 5.79, ambapo shilingi trilioni 4.6 ni kwa
ajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na shilingi trilioni 1.19 ni mikopo mipya kwa ajili ya
kugharamia miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu,
Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 3.11 kutoka soko la nje.
68.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Serikali
inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 32.48. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 20.47 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi
trilioni 7.41 za mishahara na shilingi trilioni 10.00 kwa ajili ya kulipia deni
la Serikali, michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na huduma
nyinginezo. Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi trilioni 12.01 sawa
na asilimia 37 ya bajeti yote, ambapo shilingi trilioni 9.88 ni fedha za ndani
na shilingi trilioni 2.13 ni fedha za nje. Kiwango hiki cha bajeti ya maendeleo
kimezingatia matakwa ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21
wa kutenga bajeti ya maendeleo kati ya asilimia 30 na 40 ya bajeti yote.
69.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2018/19 ni kama
inavyooneshwa katika Jedwali A.
Jedwali A: Mfumo wa Bajeti ya
Mwaka 2018/19
Chanzo: Wizara
ya Fedha na Mipango
V.
HITIMISHO
70.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, dhima ya bajeti ya mwaka 2018/19
ni kuendelea “kujenga uchumi wa viwanda
utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Mageuzi haya ya uchumi wa
viwanda yatajengwa kupitia ushiriki wetu katika shughuli za kiuchumi, ubia na
kuunganisha juhudi zetu pamoja. Ili kufikia malengo tunayoyakusudia, maamuzi
magumu ni lazima yafanyike katika kuelekeza rasilimali chache tulizonazo katika
maeneo ya kimkakati. Mabadiliko yoyote ni vigumu kuyakubali na mara nyingi
mabadiliko hupingwa. Naomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla
tuunganishe nguvu zetu, vipaji vya wananchi wetu na biashara zetu ili kufikia
malengo tunayoyakusudia. Hivyo, tunahitaji uzalendo na nidhamu ya kazi ya hali
ya juu tukikusudia kuondoa umasikini, kuongeza ajira na kuwa na uchumi
jumuishi.
71.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuchukua hatua zaidi
kuongeza uzalishaji katika sekta za viwanda na kilimo na ukusanyaji wa mapato
ya ndani yatakayowezesha ugharamiaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya
kawaida na hivyo kupunguza utegemezi. Hatua hizo ni pamoja na: kuvutia uwekezaji;
kuelekeza rasilimali kwenye maeneo machache yenye tija; kusimamia utekelezaji
wa sheria za kodi; kurasimisha sekta isiyo rasmi ikiwemo usajili wa wamiliki wa
ardhi na majengo katika mfumo wa walipa kodi; na kuhimiza matumizi ya mifumo ya
kielektroniki katika miamala mbalimbali ikiwemo matumizi ya EFD na kadi za kielectroniki za benki (Debt/credit cards) katika maeneo
yanayotoa huduma kama vile katika maduka makubwa, hoteli na vituo vya mafuta.
Hivyo, napenda kuwahimiza Watanzania tuwajibike kulipa kodi na kuhakikisha
tunatoa na kudai risiti kulingana na
muamala uliofanyika. Aidha, Serikali inawashukuru kwa dhati wananchi wote ambao
wameonesha uzalendo kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari.
72.
Mheshimiwa Spika, kipaumbele kikuu cha Serikali ni kujenga uchumi wa viwanda vinavyotumia
malighafi zinazopatikana nchini hususan zinazotokana na kilimo, mifugo na uvuvi
ili kupanua fursa za ajira, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii
(maji, afya, elimu) na kupunguza umaskini. Aidha, Serikali itaendeleza
mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma na kudhibiti
matumizi ya fedha za umma. Serikali pia itaongeza msukumo katika kuboresha
mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa
Udhibiti wa Biashara (Blueprint for
Regulatory Reforms to Improve the Business Environment). Mpango huu, pamoja
na mambo mengine unakusudia kuhuisha na kurahisisha taratibu za kulipa kodi,
tozo na ada mbalimbali.
73.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano inalenga kujenga utamaduni na nidhamu ya kukubali maoteo halisia ya
ukusanyaji wa mapato ambayo yanapaswa kuwa
ukomo wa matumizi (expenditure ceiling) badala ya utarabu
uliozoeleka wa kuanza kupanga au kuorodhesha mahitaji kwanza. Hivyo, Serikali
itajielekeza katika utekelezaji wa miradi michache ya kimkakati kwa namna
ambayo itashirikisha sekta zote zinazotegemeana na kuhakikisha kuwa miradi hiyo
inakamilika kabla ya kuanza miradi mipya.
74.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mpenzi sana wa kujisomea kuhusu maisha na sifa za viongozi
mashuhuri, viongozi bora na wa kipekee wa nchi mbalimbali waliofanikiwa
kuongoza mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika nchi zao
kama vile Deng Tsiaoping –Jamhuri ya Watu wa China; Dkt. Mahithir Mohamed –
Malaysia; Lee Kuan Yew – Singapore; Park Chung Hee – Korea, Nelson Mandela
–Afrika ya Kusini, Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere, Quett Masire – Botswana
nk. Nilichojifunza na nilieleza katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali mwaka jana kuwa viongozi wa aina hiyo wana
sifa muhimu zifuatazo:
(i)
Dira au maono dhahiri kuhusu maendeleo ya nchi zao;
(ii)
Hawasiti kutekeleza dira hizo kwa dhamira kubwa tena bila
kusita au kubadili msimamo;
(iii) Ni jasiri,
shupavu na wenye kuthubutu kutekeleza jambo wanaloliamini bila kigugumizi;
(iv)
Wana kipaji cha kujali maumivu ya wanyonge;
(v)
Ni waadilifu, wanachukia rushwa na ufisadi na ni wenye
nidhamu ya kazi ya hali ya juu;
(vi)
Wanaongoza kwa vitendo; na
(vii) Huvumilia
magumu ili kuiletea nchi mabadiliko chanya.
75.
Mheshimiwa Spika, ninapenda niwaambie tena Watanzania kwamba Mwenyezi Mungu ametutunukia
kiongozi Mkuu wa nchi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwenye sifa
hizo zote nilizotaja. Nilieleza mwanzoni
mambo machache ambayo amethubutu kutenda kwa kipindi kifupi kuthibitisha sifa
hizo. Rai yangu kwa Watanzania wenzangu ni kuwa tutumie fursa hii adimu kwa
kufanya kazi kama njia bora ya kumuunga mkono Rais wetu katika jitihada zake za
kuijenga Tanzania mpya, Tanzania ya Viwanda. Jambo hili ni muhimu kwa sababu kama
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alivyotabiri, katika safari ya maendeleo –
ya kuelekea kujenga uchumi wa viwanda – kiongozi wetu atakumbana na vikwazo na
kelele nyingi za kuzomea kutoka kwa wale wasiotutakia mema ili kutukatisha
tamaa tusifikie malengo. Hivyo, Watanzania wote tunao wajibu wa kumtia nguvu
Rais wetu ili asirudi nyuma katika safari aliyoianza na aweze kutuvusha
kuifikia Tanzania ya viwanda. Niruhusu nimalizie rai yangu kwa nukuu ya
mazungumzo ya Mwalimu Nyerere kwa “TANU
study Group” tarehe 13 Juni, 1967:
“Maendeleo na kazi
ni kitu kile kile, hakuna namna nyingine sisi ya kuendelea, hatukupewa namna
nyingine sisi ya kuendelea….. Huwezi kutenganisha vitu viwili hivi, kuendelea na kazi, kwani kazi ndiyo shughuli ya ….. kuondoa matatizo yanayomzuia binadamu hali
yake kukamilika…. Hakuna njia nyingine lazima kufanya kazi…… na kila unavyozidi
kufanya kazi kwa akili zaidi ndivyo mnavyozidi kwenda, ndivyo mnavyozidi
kuendelea,….. Kazi ndio utu …kazi ndio maendeleo…kazi ndio maisha, ni uhai,
kazi ndio civilization, ndio uungwana, ndio kula vizuri, ndio kuvaa vizuri,
ndio kuishi katika nyumba nzuri,…. ndio kushinda matatizo yote tuliyo nayo duniani
– namna ya kuyashinda ni kazi….”
76.
Mheshimiwa Spika, ninapoelekea mwisho wa hotuba hii, napenda kuwashukuru Washirika wa
Maendeleo kwa misaada na mikopo wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza
miradi na programu mbalimbali za maendeleo nchini. Wahisani hao wanatarajiwa kuchangia jumla ya
shilingi bilioni 2,676.6 katika bajeti ya mwaka 2018/19 kama ifuatavyo: Benki
ya Dunia/IDA shilingi bilioni 863.13; Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
shilingi bilioni 358.63; Global Fund shilingi bilioni 313.90; Sweden shilingi
bilioni 179.80; Jumuiya ya Umoja wa Ulaya shilingi bilioni 158.40; India
shilingi bilioni 104.57; Ujerumani (Kfw & GIZ) shilingi bilioni 81.31; Japan/JICA
shilingi bilioni 76.96; Uingereza/DFID shilingi bilioni 71.21; Denmark shilingi
bilioni 69.57; French/AFD shilingi bilioni 61.06; Canada shilingi bilioni
48.84; BADEA shilingi bilioni 40.01; Korea ya Kusini/EDCH shilingi bilioni
39.05; UNICEF shilingi bilioni 36.53; Finland shilingi bilioni 28.08; IFAD
shilingi bilioni 26.82; Italy shilingi bilioni 22.05; Norway shilingi bilioni
20.04; Benki ya Uwekezaji ya Ulaya shilingi bilioni 17.88; Uswisi shilingi
bilioni 15.74; UNDP shilingi bilioni 12.34 ; Ubelgiji shilingi bilioni 11.08;
Saudi Arabia/Saud Fund shilingi bilioni 4.81; USAID shilingi bilioni 4.20;
OPEC/OFID shilingi bilioni 2.75; na UNFPA shilingi bilioni 2.56. Ni matarajio
yetu kuwa fedha zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kama nilivyozisoma
na kwa wakati muafaka. Sisi kama Serikali tunaahidi kuwa fedha watakazotupatia zitatumika
kama ilivyokusudiwa.
77.
Mheshimiwa Spika, ninakiri kuwa bajeti niliyowasilisha isingekuwa hivi ilivyo bila kupata
michango mizuri ya kuboresha kutoka kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Sekretariaeti ya Baraza la Mawaziri na
wataalam wa wizara zote na taasisi za Serikali. Ninatoa shukrani kwa kila mmoja
wenu kwa michango mliyotoa katika mchakato mzima wa maandalizi ya bajeti hii.
78.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru viongozi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango,
nikianza na Mheshimiwa Dkt. Ashatu K. Kijaji, Mbunge wa Kondoa na Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, pia Bwana Doto M. James, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Amina Kh.
Shaaban, Dkt. Khatibu M. Kazungu, na Bibi Susan B. Mkapa. Wote hawa kwa pamoja
wamenipatia ushirikiano na msaada wa hali ya juu katika kusimamia utekelezaji
wa majukumu ya Wizara na wameratibu vizuri maandalizi ya bajeti hii. Aidha,
ninampongeza Profesa Florens Dominick Makinyika Luoga kwa kuteuliwa na Rais
kuwa Gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania na kwa kusimamia vema majukumu
makubwa ya mhimili huo wa sekta ya fedha akisaidiwa na Naibu Gavana watatu,
Wakurugenzi na watumishi wote wa Benki Kuu ya Tanzania. Vivyo hivyo, napenda
kutambua kazi nzuri ya viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
katika kukusanya mapato ya Serikali wakiongozwa na Bw. Charles E. Kichere,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Profesa Musa Assad, Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Aidha, nampongeza Bwana Athumani Selemani Mbuttuka
aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais hivi karibuni kuwa Msajili wa Hazina (Treasury Registrar).
79.
Mheshimiwa Spika, vile vile, ninawashukuru Wakuu wengine wa taasisi zilizo chini ya Wizara
ya Fedha na Mipango ikijumuisha Mabenki (TADB, TIB-DFI, TIB-CBL,TPB Bank);
Mifuko ya hifadhi ya jamii (PSPF, GEPF, PPF); Rufani za kodi (TRAB, TRAT);
Huduma za bima (TIRA,NIC); Mitaji na dhamana (CMSA, TCEM, DSE); Dhamana za
uwekezaji (UTT-MFI, UTT-AMIS,UTT-PID); Bodi ya michezo ya kubahatisha; Taasisi
za mafunzo (IFM, IRDP, IAA, TIA, EASTC); na Mfuko wa huduma ndogo za fedha (SELF Microfinance Fund). Nawashukuru pia
Wakuu wa Idara na Vitengo, bila kuwasahau wataalam, makatibu muhtasi, watunza
kumbukumbu, madereva, wahudumu na walinzi wa Wizara yetu na taasisi zake kwa
kazi kubwa walizofanya katika mwaka 2017/18 na katika kukamilisha Bajeti hii.
80.
Mheshimiwa Spika, nashindwa kumaliza hotuba hii bila kumtaja mke wangu na rafiki yangu
mpenzi Mbonimpaye. Moyo wake wa ibada kwa Mungu na uaminifu wake vimekuwa ndiyo
nguzo yangu kuu katika utumishi wangu. Ninamshukuru sana yeye pamoja na watoto
na wajukuu wetu wote tuliopewa na Mungu na familia nzima. Aidha, ninawiwa
kuwashukuru wananchi wote wa Tanzania (wakulima, wafanyakazi, na
wafanyabiashara). Ninawashukuru sana kwa uzalendo wao wa kufanya kazi kwa bidii
na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Ninawashukuru pia wanafunzi wote wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo
wanaosoma kwa bidii maana miongoni mwao tutapata viongozi na nguvukazi bora ya
Taifa. Ninawashukuru pia Wazee wetu ambao walitoa mchango mkubwa kwa Taifa letu
katika umri wao wa kufanya kazi. Aidha, siwezi kuwasahau wananchi wa wilaya za
Buhigwe na Kasulu, na mkoa wetu wa Kigoma kwa ujumla. Ninyi ni fahari yangu
maana mlinikuza. Ninawapenda! Vile vile ninawashukuru wananchi wenzangu wa
Nzinje hapa Dodoma (Zuzu kwa jina la zamani), kwa kunipokea vizuri mimi na
familia yangu.
81.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa inatarajiwa leo itakuwa siku ya mwisho wa mwezi Mtukufu wa
Ramadhan, naomba nihitimishe hotuba hii kwa kuwatakia Waislamu wote Eid
Mubarak.
82.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema ASANTE SANA MUNGU” kwa baraka zako zilizoniwezesha
kukamilisha kusoma hotuba hii. Na kwenu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote
…….
(i)
“SANDENYI SANA”!
(ii)
“NGW’ABHEJA SANA”
(iii) “WAITU MWAKORA”
(iv)
“OKORREE BHUYA”
(v)
“HAIKENI SANA”
(vi)
“MSENGWILE”
(vii) “NDAGHA FIJO”
(viii) “HEWELA”
(ix)
“KAJEKAJE”
(x)
“MURAKOZE CHANE”
(xi)
“ASANTENI SANA”
83.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja