KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Thursday, December 5, 2013

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI YA ELIMU TANZANIA (TET) .


Kaimu Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania(TET), Dk, Leonard Akwilapo,(kushoto) akizungumza na waandishi Dar es Salaa kuhusu Utekelezaji wa Majukumu mbalimbali ya Taasisi hiyo ikiwepo Ukuzaji wa Mitaala.Wengine ni Mkurugenzi Idara ya Ubunifu na Uboreshaji Mitandao,Angela Katabaro na Mkurugenzi Utafiti,Habari na Machapisho,Makoye Wangeleja.

Taasisi ya Elimu Tanzania ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 13 ya Mwaka 1975. Hii ni Taasisi ya umma iliyo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. TET imepitia mabadiliko kadhaa ya kimfumo, ingawa kwa kiasi kikubwa bila kuathiri majukumu yake ya msingi ambayo yameainishwa katika sehemu ya 2 ya taarifa hii. Kati ya mwaka 1965 – 1975 ilikuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa imeanzishwa na Baraza la Chuo hicho na ilijulikana kama Taasisi ya Elimu. Mwaka 1975 taasisi ilitoka katika himaya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa taasisi inayojitegemea. Mnamo mwaka 1987, taasisi ilibadilishwa jina na kuwa Taasisi ya Ukuzaji Mitaala. Baadaye mwaka 1993 taasisi ilibadilishwa tena jina na kuwa Taasisi ya Elimu Tanzania, jina hilo linaendelea kutumika hadi leo. Sababu kubwa ya kubadilisha jina na ukweli kuwa taasisi inajihusisha na mambo mengi ya kitaalamu zaidi ya ukuzaji mitaala. Hivyo ilionekana kuwa si sahihi kuitambulisha kwa shughuli moja tu ya mitaala.
Kuanzia mwezi Julai 2009 TET ilipandishwa hadhi kuwa Taasisi ya Elimu ya Juu isiyokuwa chuo kikuu kwa kuzingatia jukumu lake la utoaji wa mafunzo ya kitaalamu yanayohitaji tuzo mbalimbali. Hivyo, TET imesajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (National Council for Technical Education/NACTE). Madadiliko haya yaliambatana na jukumu la kuendesha mafunzo na kutoa tuzo TET; Taarifa kwa Umma 2013 2
mbalimbali zikiwemo za cheti, stashahada na shahada katika ubunifu na ukuzaji mitaala bila kuathiri majukumu yake ya kisheria yaliyoainishwa katika Sheria anzilishi iliyotajwa hapo juu.
2.0 MAJUKUMU YA TAASISI YA ELIMU TANZANIA

2.1 Jukumu Kuu Jukumu kuu la TET ni kutafsiri kwa vitendo sera mbalimbali za Serikali katika programmu za kielimu na mitaala inayowezesha utoaji wa elimu bora kwa ngazi za elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. 2.2 Majukumu Mahususi Kwa mujibu wa Kifungu Na. 4 cha Sheria ya TET Na. 13 ya Mwaka 1975, na kwa muhtasari chini ya taarifa hii, majukumu mahususi ya Taasisi ya Elimu Tanzania yamo katika maeneo makuu manne yafuatayo: (a) Ubunifu na Uboreshaji Mitaala Katika kutekeleza jukumu hili TET hufanya yafuatayo:
(i) Kubuni na kuandaa mitaala;
(ii) Kuboresha na au kubadilisha mitaala*.
(iii) Kuandaa, kurekebisha au kubadilisha mihtasari ya masomo kwa kuzingatia mtaala ulioboreshwa.

* Ufafanuzi:
Ø “Mtaala”ni mwongozo wa utoaji elimu unaobainisha ujuzi, yaani stadi, maarifa na mwelekeo wa kitabia unaokusudiwa kutolewa katika ngazi fulani ya elimu, njia za kufundishia na kujifunzia, rasilimali mbalimbali zinazohitajika katika kufundishia na
TET; Taarifa kwa Umma 2013 3

kujifunzia, utaratibu wa kutathmini wanafunzi, muda wa mafunzo na tuzo za elimu zitakazotolewa.

Ø Kuboresha mtaala” ni mchakato endelevu wa kufanya marekebisho madomadogo kwenye mihtasari ya masomo bila kuathiri mtaala kwa jumla. Maboresho ya mtaala yanaweza kutokea mara kwa mara kadri taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mitaala zinavyoweza kuonesha. Mfano:

Hatua ya kutenganisha somo la Fizikia na Kemia kutoka somo moja na kuwa masomo mawili mwaka 2007 ni kitendo cha kuboresha mtaala
Ø “Kubadilisha mtaala” maana yake ni kufanya mageuzi makubwa yanayoathiri mtaala. Mabadiliko ya mitaala hutokea kwa nadra hasa kunapokuwa na mabadiliko makubwa katika mfumo wa Taifa wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiteknolojia.

Mfano: Azimio la Arusha la Mwaka 1967 lilibadilisha mfumo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hii ilfuatiwa na mabadiliko ya mitaala katika nyakati tofauti yakiwemo mabadiliko ya mwaka 1979 ambapo masomo ya michepuo (Kilimo, Ufundi, Sayansi Kimu na Biashara) yaliingizwa kwenye mitaala. Lengo lilikuwa ni kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Elimu ya Kujitegemea iliyoasisiwa katika Azimio hilo. (b) Uandaaji wa Vifaa vya Kielimu Yafuatayo hufanyika:
(i) Kuandika na kuchapisha vitabu vya kiada na ziada;
TET; Taarifa kwa Umma 2013 4

(ii) Kuandaa vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia kama vile vivunge vya masomo (subject kits), miongozo, chati na vifaa vya elektroniki kwa mfano: diski za video na za kusikiliza.
(iii) Kubuni mbinu za kufaragua (improvise) visaidizi vya kufundishia (teaching aids) kwa ajili ya kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji;
(iv) Kuweka viwango vya ubora wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

(c) Utoaji Mafunzo ya Mitaala Mafunzo kwa walimu, wakaguzi wa shule, maafisa mitihani, maafisa elimu na wadau wengine wahusikao na utekelezaji au usimamiaji wa elimu hutolewa katika maeneo makuu yafuatayo:
(i) Mafunzo kabilishi kuhusu maboresho/mabadiliko ya mitaala;
(ii) Mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji;
(iii) Mafunzo ya muda mrefu kuhusu ubunifu na utekelezaji wa mitaala (kwa sasa TET inaendesha programu ya Stashahada ya Uzamili Katika Ubunifu na Ukuzaji Mitaala).

(d) Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Chini ya jukumu hili TET hutekeleza yafuatayo:
(i) Kufanya utafiti kuhusu masuala/matatizo mbalimbali ya kielimu;
(ii) Kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mitaala;
(iii) Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali na wadau wengine wa elimu au kuchukua hatua zilizo ndani ya mamlaka ya TET kwa lengo la kuinua ubora wa elimu kwa kuzingatia taarifa za utafiti.
(iv) Kuelimisha wadau na umma kwa jumla kuhusu masuala ya elimu.
TET; Taarifa kwa Umma 2013 5

3.0 UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TET

3.1 Miongozo ya Utekelezaji wa Majukumu ya TET Katika kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa hapo juu, TET huzingatia miongozo ifuatayo:
(a) Sheria ya TET Na. 13 ya Mwaka 1975;
(b) Sera, mipango, maelekezo na vipaumbele vya Serikali kupitia nyaraka na matamko mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
(c) Mpango Mkakati wa TET wa Miaka Mitano (uliopo ni wa mwaka 2011 – 2016).

3.2 Utekelezaji wa Majukumu ya TET Katika Kipindi cha Miaka Mitatu Iliyopita (2009/2010 Hadi 2011/2012)

Katika kipindi hicho kazi zilizotekelezwa kwa kuzingatia mipango ya kazi ya kila mwaka zipo katika maeneo makuu matatu yafuatayo:
(a) Uandaaji wa Mihtasari na Miongozo ya Masomo

Kazi zifuatazo zilitekelezwa:
(i) Kuboresha mihtasari ya masomo 26 ya ualimu ngazi ya cheti kwa elimu ya awali na msingi;

(ii) Kuboresha mihtasari ya masomo 28 kwa masomo ya ualimu ngazi ya stashahada.

(iii) Kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, TET ilichapisha na kusambaza mihtasari na miongozo ya masomo yote ya shule za msingi. Ambapo:
TET; Taarifa kwa Umma 2013 6

Jumla ya mihtasari 30,908 ilisambazwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na kila shule ilipata nakala 2.
 Mihtasari 105 iligawiwa kwa Waratibu wa Elimu nakala tano (5) kwa kila mmoja.
 Jumla ya miongozo 15,424 ilisambazwa katika mikoa 21 na kila shule ilipata nakala moja.

(iv) Kuboresha mihtasari 25 ya kufundishia masomo ya sekondari kidato cha V na VI.

(v) Kuchapisha mihtasari ya masomo 25 ya kidato cha V na VI.

(vi) Kuandika mihtasari miwili (2) ya somo la Ujasiriamali kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu ngazi ya Stashahada.

(vii) Kuandaa jumla ya mihtasari 36 ya Elimu Maalum kwa mafunzo ya ualimu katika mchanganuo ufuatao:
 Mihtasari 19 ya ngazi ya stashahada; na
 Mihtasari 17 ya ngazi ya cheti.

(viii) Kuchapisha Moduli 9 za masomo ya ualimu ngazi ya stashahada na 14 ngazi ya Cheti.

(ix) Kuboresha na kuchapisha miongozo 18 ya kufundishia masomo ya sekondari kidato cha I-IV.

(x) Kuchapisha na kusambaza maandiko sita (6) ya mitaala (Curriculum Documents) kwa shule na vyuo vya ualimu.
TET; Taarifa kwa Umma 2013 7

Uendeshaji wa Mafunzo ya Mitaala

Kazi zilizotekelezwa ni kama ifuatavyo:
(i) Kuendesha mafunzo kwa walimu wa shule za msingi wapatao 510 wa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi katika jumla ya Wilaya/ Halmashauri 17.

(ii) Kuendesha mafunzo kwa walimu 240 katika wilaya za Masasi, Tunduru, Same, Kishapu, Meatu, Musoma (V), Ukerewe, Bariadi na Bunda kuhusu mtaala wa elimu ya msingi uliboreshwa.

(iii) Kuendesha mafunzo juu ya utekelezaji wa mtaala wa sekondari ulioboreshwa kwa walimu 30 wa shule za sekondari Mazinde Juu.

(iv) Kuendesha mafunzo kwa walimu 45 na Afisa Elimu Taaluma na Mkaguzi wa Shule za Sekondari za wilaya ya Pangani.

(v) Kuendesha mafunzo ya ufundishaji bainifu (diagnostic teaching kwa wakufunzi 34 wa vyuo vya ualimu ngazi ya cheti.

(vi) Kuendesha mafunzo ya mitaala (competence –based curriculum) kwa Waratibu wa Mitaala 50 na wataalamu 36 kutoka nchi 8 za Afrika kupitia programu za Elimu ya Msingi Katika Afrika (Basic Education in Africa Programmes/ BEAP) kwa kushirikiana na UNESCO.
TET; Taarifa kwa Umma 2013 8

(vii) Kuendesha mafunzo kwa walimu 200 wa somo la French kwa shule za sekondari katika kanda zote 11 za elimu Tanzania Bara.

(viii) Kuendesha mafunzo kwa wakufunzi 64 wa vyuo 16 vya ualimu ngazi ya stashahada.

(ix) Kuendesha mafunzo ya Programu ya Stashahada ya Uzamili katika Ubunifu na Ukuzaji Mitaala (Postgraduate Diploma in Curriculum Design and Development - PGDCDD). Programu hii imekuwa ikipata wanafunzi kutoka takribam mabara yote ya dunia na imekuwa na mafanikio kama ifuatavyo:

§ Awamu ya kwanza: Oktoba 2011; waliodahiliwa 49 na waliofaulu 42 (85.7%).

§ Awamu ya pili: Novemba 2012; waliodahiliwa 47, waliofaulu 43 (91.5%).

§ Awamu ya tatu: Desemba 2013; waliodahiliwa ni 75, na mafunzo yanaendelea.

Tanbihi (N. B.): Mafunzo haya yanalenga kuwa na wataalamu wengi waliobobea katika fani ya ukuzaji na utekelezaji wa mitaala ili kuinua ubora wa elimu na kuchochea kasi ya maendeleo. Kwa wastani Watanzania 20 wamekuwa wakipata mafunzo haya kila mwaka na kuna uwezekano mkubwa wa idadi hii kuongezeka kadri siku zinavyokwenda. TET; Taarifa kwa Umma 2013 9
Kabla ya mwaka 2011 fani ya ukuzaji na ubunifu wa mitaala imekuwa haitolewi na chuo chochote hapa nchini kama eneo la utaalamu linalojitegemea bali kama sehemu tu ya kozi nyingine. Tunatumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati UNESCO na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kushirikiana nasi katika kuendesha programuu hii kila mwaka. Tunaishukuru pia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ambayo ilihakiki na kuidhinisha mtaala wa programu hiyo. (c) Ufuatiliaji na Tathmini ya Mitaala Kazi zifuatazo zilitekelezwa:
(i) Kuanzisha na kutekeleza Mpango wa Ushirikiano kati ya TET na shule (TIE-School Partnership) ambao unahusu Waratibu wa Mitaala kuwa na vipindi maalumu vya kufanya kazi shuleni kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mitaala na kubaini changamoto zilizopo kwa lengo la kuzifanyia kazi. Kwa kuanzia mpango huu unatekelezwa katika shule za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

(ii) Kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mitaala katika ngazi mbalimbali hivyo kuwezesha kupata taarifa zilizotumika kuboresha mitaala ya elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu kama ilivyoelekezwa hapo juu.

4.0 CHANGAMOTO

Changamoto kuu katika kutekeleza kazi za kitaaluma zinajumuisha upungufu/ukosefu wa tengo la fedha kwa ajili ya shughuli za mitaala TET; Taarifa kwa Umma 2013 10
na upungufu wa vitendea kazi hususan vifaa vya ofisi kama kompyuta. Tatizo hili limekuwa likishughulikiwa kwa kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kama vile kushirikiana na wadau wa elimu na kutumia vyanzo vya ndani vya mapato. Baadhi wa wadau wakuu wanaoshirikiana na TET katika kuendesha miradi ya kielimu ni UNESCO, NUFFIC, USAID, UNICEF, Wizara ya Ujenzi (kuhusu Elimu ya Usalama Barabarani) na Wizara ya Afya (elimu ya VVU na UKIMWI) – kwa kutaja wachache. Tunatumia fursa hii kuwashukuru sana wadau hawa wa elimu na wengine wengi ambao hatujawataja.
5.0 MIPANGO YA BAADAYE

Kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa TET wa Maendeleo ya Miaka Miatano (2011- 2016), TET inakusudia kufanya yafuatayo katika kipindi hicho:
(i) Kufanya tahakiki (review) ya mitaala katika ngazi zote.
(ii) Kuandaa vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikiwemo vitabu, vifaa vya kielektroniki na na programu za redio na runinga;
(iii) Kukamilisha andiko la Mwongozo wa Taifa wa Ukuzaji Mitaala;
(iv) Kufanya tathmini ya utekelezaji wa mitaala ya elimu ya awali, msingi na sekondari;
(v) Kuendesha makongamano ya kitaifa na kimataifa kuhusu mitaala;
TET; Taarifa kwa Umma 2013 11

(vi) Kujenga kituo cha kisasa cha mafunzo ya ukuzaji mitaala katika kiwanja cha TET Mikocheni;

(vii) Kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Waratibu wa Mitaala wa TET;

(viii) Kuandika na kutekeleza sera ya utafiti na uelekezi wa kitaalamu;

(ix) Kuendesha mafunzo elekezi kwa walimu na watekelezaji wengine wa mitaala kuhusu utekelezaji wa mitaala.

6.0 HITIMISHO
Nawaomba Watanzania wote, washirika wa maendeleo hasa katika sekta ya elimu na wadau wote wa elimu wakiwemo wa sekta binafsi, kushirikiana na TET katika juhudi za kutoa elimu iliyo bora kwa watoto na umma wa Watanzania. Wanaweza kuwasiliana nasi kupitia tovuti ta TET ambayo ni www.tie.go.tz. Tunakaribisha maswali, hoja, mipango ya kuboresha elimu na hata ukosoaji wa kujenga ili tuendelee kuboresha elimu kwa manufaa ya watu wetu na nchi yetu. Mwisho naishukuru sana Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kutupatia fursa hii adhimu ya kuwasiliana na Watanzania. Na vile vile tunatoa shukrani nyingi kwenu waandishi wa habari kwa kuhudhuria kongamano hili; tunatarajia kuwa mtafikisha taarifa hizi kwa wananchi. ASANTENI SANA Dkt. Leonard D. Akwilapo Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAASISI YA ELIMU TANZANIA
 


No comments: