Mchezaji
Alain Kabange Twite hataweza kuichezea Yanga msimu huu (2012/2013)
baada ya klabu hiyo kuingiza nyaraka zenye upungufu wakati ikimuombea
Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa njia ya mtandao (Transfer
Matching System- TMS).
Kwa
mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), baadhi ya
nyaraka zenye upungufu katika maombi hayo ni mkataba kati ya Twite na
Yanga, lakini vile vile makubaliano ya mkopo (Loan Agreement) kati ya
Yanga na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo ndiyo
inayommiliki mchezaji huyo.
Ili
mchezaji aweze kupata ITC kwa njia ya TMS, kwa mujibu wa Kanuni za
Uhamisho wa Wachezaji za TFF kuna nyaraka kadhaa muhimu zinatakiwa
kukamilika katika maombi hayo ili hati hiyo iweze kupatikana.
AZAM YAIFUKUZIA YANGA VPL
Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 15 kesho (Januari 30 mwaka
huu) kwa mechi mbili ambapo Azam iliyo katika nafasi ya pili nyuma ya
Yanga itakuwa mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza.
Mechi
hiyo itachezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam huku Azam ikisaka
ushindi ili kuikaribia Yanga inayoongoza wakati Toto Africans
inayonolewa na John Tegete ikitaka kurekebisha makosa ya kupoteza mechi
yake iliyopita dhidi ya Oljoro JKT.
Uwanja
wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi
kati ya Oljoro JKT dhidi ya wageni Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani
Kagera itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo wa Musoma.
Ushindi
kwa Oljoro JKT yenye pointi 17 utaihakikishia kubaki katika nafasi yake
ya nane wakati Kagera Sugar inayofundishwa na kocha mkongwe Abdallah
Kibaden utaifanya ipige hatua moja mbele katika msimamo wa ligi.
Ligi
itaendelea tena Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo
vinara Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam wakati Polisi Morogoro ikiikaribisha African Lyon mjini Morogoro.
Nazo
Mgambo Shooting ya Tanga na Ruvu Shooting ya Mlandizi mkoani Pwani
zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
KAMPUNI TANO ZAOMBA KUKARABATI HOSTELI TFF
Kampuni
tano zimewasilisha tenda zao kuomba kupewa kazi ya kukarabati hosteli
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Januari 7 mwaka huu TFF
ilitangaza tenda kwa ajili ya ukarabati wa hosteli hiyo baada ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kukubali ombi lake la kutoa
fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Ufunguzi
wa tenda hizo ulifanyika jana (Januari 28 mwaka huu) kupitia kwa Bodi
ya Tenda ya TFF mbele ya wazabuni wote watano waliowasilisha tenda zao
na kushuhudiwa pia na Mkandarasi mshauri. Wazabuni (kampuni)
waliojitokeza awali walikuwa saba, lakini waliorejesha zabuni zao ni
watano.
Kampuni
hizo ni Crescent Concrete Limited, DGS Company Limited, Mart Builders
Company Limited, Prince General Investment Limited na Send Star Company
Limited.
Bodi ya Tenda ya TFF itakutana Januari 31 mwaka huu pamoja na mambo mengine kuchagua kampuni ambayo itafanya ukarabati huo.
LALA SALAMA DARAJA LA KWANZA KUANZA JUMAMOSI
Mzunguko
wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo itatoa timu tatu
zitakazocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2013/2014) unaanza
Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) katika viwanja tisa tofauti.
Kundi
A litakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa
Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa
Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Mechi
za Kundi B, Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) itakuwa Transit Camp na
Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Moro United dhidi
ya Villa Squad (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam). Jumapili (Februari 3
mwaka huu) ni Tessema na Green Warriors (Mabatini, Pwani), Ashanti
United na Polisi Dar (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam).
Kundi
C Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT
(Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto,
Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora
na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Ligi
hiyo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi
wa kila kundi atapanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao. (Ratiba imeambatanishwa)
WAPAMBE MARUFUKU KWENYE PINGAMIZI, USAILI TFF
Kamati
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema
waliowekewa pingamizi na wa walioweka pingamizi hawaruhusiwi kufika
katika kikao cha kesho (Januari 30 mwaka huu) wakiwa na vikundi vya
ushangiliaji au wapambe.
Kikao
cha kupitia pingamizi kitafanyika saa 4 asubuhi na wapambe au washabiki
wa waombaji uongozi pamoja na waweka pingamizi hawakiwi kuwepo kwenye
eneo la kikao hicho.
Wote walioweka pingamizi na waliowekewa pingamizi barua zao za mwito wa kuhudhuria kikao cha Kamati
ya Uchaguzi ya TFF zimeshatumwa kwenye anwani za barua-pepe zilizo
kwenye taarifa za pingamizi au kwenye fomu za maombi ya uongozi.
Leo
waombaji uongozi watatumiwa barua za mwito kwa barua-pepe wa kuhudhuria
usaili utakaofanyika tarehe 01-02 Februari 2013. Tarehe 01 Februari
2013 watasailiwa waombaji uongozi wa TPL Board na waombaji ujumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 1 hadi Kanda ya 8. Waombaji
uongozi kupitia Kanda ya 9 hadi ya 13 na waombaji uongozi wa Makamu wa
Rais na Rais wa TFF watasailiwa tarehe 02 Februari 2013 kuanzia saa 4
asubuhi.
Vyombo
vingi vya habari vimeonyesha nia ya kuwepo mdahalo wa wagombea uongozi
katika TPL Board na TFF. Kanuni za Uchaguzi za TFF hazizuii jambo hilo
kufanyika, bali tu lizingatie Kanuni za Uchaguzi za TFF. Mojawapo ya
mambo ya kuzingatiwa ni kwamba mdahalo huo ufanyike wakati wa kipindi
cha Kampeni na usiwe na taswira ya kuwapendelea au kuwabagua baadhi ya
wagombea. Kanuni hazimlazimishi mgombea kushiriki mdahalo.
Pia ni vema mdahalo ukaandaliwa na kuratibiwa na
Taasisi inayounganisha vyombo vya habari au waandishi wa habari kama
TASWA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF lazima ijulishwe kwa maandishi nia hiyo
ya kufanyika mdahalo na utaratibu utakaotumika mapema kabla ya
kufanyika mdahalo huo ili kujiridhisha kuwa utaratibu utakaotumika
kuandaa na kuendesha mdahalo haukiuki kanuni za Uchaguzi za TFF.
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF inavishukuru vyombo vya habari kwa kuzingatia Kanuni
za Uchaguzi hadi sasa na kuwaomba waendelee kufanya hivyo hadi mwisho
wa mchakato wa uchaguzi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment