Asema kwa dhambi hiyo hakuna dawa lazima Chadema kife.
Adai ni laana ya Mwalimu wasitafute mchawi.
Awaasa waandae mazishi mapema.
NA MWANDISHI WETU, MWANZA
KATIBU
wa wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
amewataka Chadema wasitafute mchawi anayewamaliza nje ya chama chao kwa
kuwa ubaguzi ulioota mizizi kwa muda mrefu ndani ya chama hicho ndiyo
unaowamaliza..
Alisema kwa kukumbatia ubaguzi aliodai kulelewa na
waasisi na viongozi wa kitaifa ndani ya Chadema, sasa iliyobaki waandae
mapema, mazishi ya chama hicho kwa kuwa hakuna jinsi ambavyo
kitanusurika kufa kutokana na dhmabi hiyo mbayo hata Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere aliikemea akisema ni mbaya sawa na kula nyama ya mtu.
Nape aliyasema hayo leo Januari 20, 2013, jijini
Mwanza kwenye mkutano wa hadhara wa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara)
Philip Mangula na baadhi ya mawaziri, uliohudhuriwa na maelfu ya wanachi
wa jiji hilo na vitongoji vyake kwenye Uwanja wa mpira wa Nyamagana.
Nape alisema anashangazwa na viongozi wa Chadema
kuendelea kunyooshea vidole CCM kuwa eti inahusika na mtafaruku na
umahututi wa chama chao wakati CCM walishajitahidi kuwataadharisha
mapema kuwa ubaguzi wanaoukumbatia, licha ya kuathiri umoja na
mshikamano ni dhambi ambayo itakisambaratisha chama hicho.
"Hamuwezi kuwa na chama ambacho ili kiongozi wake
adumu na kuheshimika lazima awe anatoka ukanda fulani au ukoo fulani
ndio adumu, vinginevyo anasukiwa mizengwe na mwisho kutimuliwa" alisema
Nape na kuongeza "walianza na kina Chacha Wangwe na Watanzania wote
wanajua leo kilichompata Chacha Wangwe, sasa wameanza kumwandama Zitto
na wanaoitwa vijana wake, na pia nasikia wamejipanga kumfukuza Shibuda
wiki ijayo."
"Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alishasema dhambi ya
ubaguzi ni kubwa, na ni sawa na kula nyama ya mtu, ambapo mtu akishaila
anazoea kiasi kwamba haachi, basi nao Chadema hawana namna ya kuachana
na ubaguzi unaoendelea ndani ya chama chao, hivyo watasambaratika kwa
laana hiyo ya Mwalimu", alisema Nape.
Nape alilionya kwamba, ikiwa Chadema wanabaguana
kiasi hicho ndani ya alichokiita kichama kidogo, kama hicho watafanyaje
wakipewa dhamana ya kutawala nchi. " Ikiwa wanabaguana ndani ya kichama
kidogo kiasi hichi ambacho hakijai hata mkononi, watafanyaje wakipewa
dhamana ya kuongoza hata kipande cha nchi yetu?" alihoji.
Nape alidai kuwa ubaguzi ndani ya Chadema umejikita
kwenye ukanda, ukabila na hata udini na kwamba ubaguzi huo unajionyesha
zaidi kwenye safu ya uongozi wa chama hicho na maeneo mengine. "Sasa leo
nimeamua kuwapa ushauri wa bure kabisa Chadema wasiendelee kutafuta
mchawi nje ya chama chao", alisema.
Mkutano huo ambao umehusisha wananchi kutoka Wilaya
za Ilelema na Nyamagana, ni moja ya mikutano ya Mangula ambayo amekuwa
akiifanya tangu aanze ziara ya kwanza katika mkoa wa Mwanza ambapo
tayari ameshapita katika wilaya za Magu, Ukerewe na Sengerema.
No comments:
Post a Comment