NSSF
TANGAZO
Saturday, March 9, 2013
JAMII YATAKIWA KUFANYA JITIHADA ILI KUHAKIKISHA KUWA MTOTO WA KIKE ANASOMA.
Na Anna Nkinda – Magu
Jamii imetakiwa kufanya kila iwezalo ili kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanasoma na kupata elimu bora kwa kufanya hivyo kutawasaidia watoto hao kuweza kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiweka jiwe la msingi la jengo la Hosteli ya wasichana ya chuo cha sanaa na ufundi Bujora kilichopo wilayani Magu katika mkoa wa Mwanza.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa ni wajibu wa jamii kuwatengenezea watoto mazingira mazuri ya kusoma ikiwa ni pamoja na kuwajengea Hosteli ambayo itawasaidia kuishi shuleni na hivyo kuepukana na vishawishi ambavyo vinaweza kuwahatarishia masomo yao.
“Changamoto katika maisha ya wanawake ni nyingi lakini tunaweza kuzipunguza na hatimaye kuzitokomeza kabisa kwa kuwapatia elimu bora watoto wa kike ili waweze kuwa na ufahamu sahihi wa masuala ya maisha kwa ujumla wake na hatimaye kuwa na ujasiri wa kupambana nayo”, alisema Mama Kikwete.
Aliendelea kusema kuwa alianzisha taasisi ya WAMA mwaka 2006 moja ya malengo yake ikiwa ni kumsaidia mwanamke kielimu na hatimaye aweze kujikwamua kiuchumi. Katika Sekta ya elimu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mtoto wa kike ambaye ni yatima na anatoka katika mazingira hatarishi anapata elimu sawa na watoto wengine.
Mama Kikwete pia aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii hadi kufika elimu ya chuo kikuu na kujiepusha kushika mambo mawili kwa wakati mmoja ambayo yatawapelekea kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na ujauzito na hivyo kutotimiza ndoto zao kwani tabu wanayoipata leo ni mafanikio ya baadaye.
Akisoma taarifa ya chuo hicho Mwalimu Lilian Bwire alisema kuwa chuo kilianzishwa mwaka 1973 kikiwa kinatoa mafunzo ya sanaa na ufundi kwa vijana wa jinsia zote lakini katika miaka ya mwanzoni ya 2000 chuo kilianza kudorora na hatimaye kukosa wanafunzi kwa sababu mashirika ya wahisani kutoka nchini Denmark na Ujerumani yalisitisha msaada na chuo kushindwa kujiendesha kwa vile asilimia70 ya wanafunzi walisoma bure na asilimia 30 walilipa ada kwa kiwango cha chini.
Mwalimu Bwire aliendelea kusema kuwa mwaka 2012 wazo la kukiendesha chuo liliibua kutokana na uhitaji mkubwa wa vijana wengi wanaomaliza kidato cha nne ambao hawapati nafasi ya kuendelea na masomo ya juu hasa watoto wa kike na hivi sasa chuo hicho kina wanafunzi 236 kati ya hao 103 ni wanafunzi wa kike.
“Changamoto kubwa inayotukabili ni uhaba wa nyumba za kulala watoto wa kike, chuo kililazimika kuanza ujenzi wa hosteli yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 50 ambao watapata mazingira mazuri ya kusoma na kujiepusha na vishawishi ambavyo vitawapelekea kupata ujauzito na magonjwa ya zinaa ukiwepo Ukimwi”, alisema Mwalimu Bwire.
Gharama za ujenzi wa jengo hilo unakadiriwa kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 78 kwa kuwa elimu ya mtoto wa kike ni moja ya kipaumbele cha Taasisi WAMA Mama Kikwete kupitia taasisi hiyo alichangia shilingi milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli hiyo.
No comments:
Post a Comment