Na Anna Nkinda – Maelezo, Mbeya
Watanzania wametakiwa kupiga magoti na kuomba kila mtu kwa
imani yake ili mwenyezi Mungu aweze kuwalaani watu ambao wanatishia
kuvuruga amani ya nchi na kusababisha chuki katika jamii.
Wito huo umetolewa na Chifu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Rocket Mwashinga
wakati akiongea na wakazi wa Ushirika wilayani Rungwe kwenye mazishi ya
George Mwaikela aliyefariki Dunia juzi jijini Dar es Salaam kwa ajali
ya gari.
Chifu Mwashinga alisema kuwa hali iliyopo nchini hivi sasa si nzuri
kwani kuna baadhi ya makundi ya watu wanataka kuwalambisha watanzania
sumu mbaya ya chuki ya udini na kuwaomba wasiilambe sumu hiyo bali kila
mmoja kwa imani yake apige magoti na kumuomba Mwenyezi Mungu ili amani
iliyopo iendelee kuwepo.
“Tunashindwa kulala usingizi kutokana na hofu na katika mkusanyiko kama
huu tunakosa raha kabisa kwa kuhofia kuwa jambo baya lolote linaweza
kutokea”, alisema Chifu Mwashinga.
Alisema kuwa marehemu George alikuwa ni kijana mdogo wa kwanza na wa
ajabu aliyeweza kuwafuata mashifu na kuwapa ushauri mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kufuata mila nzuri na kuachana na mila ambazo zimepitwa na
wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abas Kandoro alisema kuwa
binadamu anaweza kupata madhara kwa kutokumtii Mwenyezi Mungu na katika
kitu kibaya ambacho kinaanza kutokea katika jamii ya watanzania ni
pamoja na kubaguana katika misingi ya dini hali ambayo itasababisha watu
kuuana.
Mh. Kandoro alisema, “Tumekusanyika hapa kuja kumzika ndugu yetu si kwa
itikadi ya dini bali ni binadamu mwenzetu, tulikuwa tunaishi naye kwa
amani na upendo na sisi sote mbele ya Mwenyezi Mungu ni kitu kimoja na
matendo yetu katika dunia ndiyo yatakayotufanya tuuone ufalme wa Mungu.
Sisi kama viongozi wenu wa Mkoa huu tunawaomba mdumishe amani na utulivu
tulionao ili tuweze kufanya mambo makubwa kama wanayofanya watu
wengine”.
Naye Baba Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu Ruanda Padre Peter Malya
aliwataka watanzania kuishi maisha yanayoendana na ubinadamu na ya
kumpendeza Mwenyezi Mungu na kuachana na matendo ya kinyama.
Padre Malya alisema kuwa hivi sasa kuna baadhi ya watu wanauza mkaa, juu
ya magunia wanapanga mkaa mkubwa na mzuri lakini chini wanaweka chenga
na wengine wanauza nyanya, juu ya ndoo wanaweka kubwa na nzuri lakini
chini wanaweka ndogo na wengine wamefikia hatua ya kuhifadhi samaki kwa
kutumia dawa za kuhifadhia maiti.
“Ninawaomba muishi kwa upendo na kuwasaidia watu wasiojiweza wakiwemo
yatima, wajane, wagonjwa na vikogwe na kwa kufanya hivyo mtakuwa
mnajiongezea baraka kwa Mwenyezi Mungu na kuacha kumbukumbu pale ambapo
mtakuwa mmeaga Dunia na kutangulia mbele za haki”, alisema Padre Malya.
Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali
walihudhulia mazishi hayo akiwemo Mke wa Rais Mh. Mama Salma Kikwete na
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mh. Adam Malima
No comments:
Post a Comment