Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi ,Zanzibar.
Jeshi la Polisi Zanzibar
limefanikiwa kuwakamata watu watatu wanaosadikiwa kujihusisha na vitendo vya
uhalifu wakiwa na bastola moja ambayo ilikuwa imefichwa katika shamba la
migomba ikiwa imechimbiwa chini ya ardhi kwenye kopo la rangi.
Akizungumza na
waandishi wa habari Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Alli Mussa alisema watu
hao walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema na ndipo walipowakamata na katika mahojiano ya awali watuhumiwa hao walikiri kuwa na bastola
wanayoimiliki isivyo halali.
Kamanda Mussa,
aliwataja watu hao kuwa ni Alli Mwanasai (40) mkazi wa Mbagala Dar es Salaam, Mohamed
Said Mohamed (32) na Miraji Mohamed Rashid (40) wote wakazi wa Bububu
Kigamboni Zanzibar ambapo mpaka hivi
sasa wanaendelea kuhojiwa.
“Kutokana na kukamatwa
kwa bastola hii, tunaendelea kuwahoji watu hawa kwa kina zaidi ili kubaini kama
matumizi ya silaha hii ilihusika katika matukio mbalimbali yaliyojitokeza hapa
Zanzibar yakiwemo tukio la kuuwawa kwa Padri Mushi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda ”Alisema Kamishna
Mussa.
Aidha, Kamishna Mussa
alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili kujua washirika wao wengine,
wakiwemo watu wanaowafadhili kwa kuwapa taarifa zinazowawezesha kufanya
uhalifu, watu wanaowapa usafiri kukamilisha uhalifu huo na watu wanaowafdhili
kwa pesa ili kutekeleza uhalifu huo.
Kamishna Mussa
amewahakikishia wananchi kwamba kutokana na juhudi kubwa za Jeshi hilo wahalifu
wote watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi
kuendelea kutoa taarifa za watu wanaowashuku kuhusika na vitendo vya uhalifu
hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo
vya sheria.
No comments:
Post a Comment