Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa
2013/2014 inaanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu kwa timu zote 14
kuwa viwanjani katika miji saba tofauti.
Hata
hivyo, kabla ya ligi hiyo kuanza kutakuwa na mechi ya kufungua msimu
(Ngao ya Jamii- Community Shield) kati ya bingwa mtetezi Yanga na Makamu
bingwa Azam itakayochezwa Agosti 17 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Mechi
za VPL za Agosti 14 mwaka huu zitakuwa kati ya Yanga na Ashanti United
(Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mtibwa Sugar na Azam (Uwanja wa
Manungu, Morogoro), na JKT Oljoro na Coastal Union (Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).
Nyingine
ni Mgambo Shooting na JKT Ruvu (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Rhino
Rangers na Simba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na
Kagera Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Ruvu Shooting
na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani).
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Novemba 3 mwaka huu wakati wa pili utamalizika Aprili 27 mwakani. (Ratiba ya mzunguko wa kwanza na wa pili imeambatanishwa- attached).
TAIFA STARS KWENDA KAMPALA J5
Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaondoka Mwanza keshokutwa (Julai
24 mwaka huu) kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya marudiano ya
Kombe la CHAN itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa
Mandela kuanzia saa 10 kamili jioni.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini
Mwanza chini ya Kocha Kim Poulsen tangu Julai 14 mwaka huu kujiandaa kwa
mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali
za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Timu
hiyo itaondoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 7.25 mchana kwa ndege ya
PrecisionAir, na inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Entebbe saa 10.15 jioni.
Wakati
huo huo, Kocha Kim Poulsen kesho (Julai 23 mwaka huu) atakuwa na
mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya kikosi chake.
Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye hoteli ya La Kairo
jijini Mwanza.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment