Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Waislamu nchi
wametakiwa kutumia kipindi cha mfungo wa Ramadhani kuomba na kutubu dhambi zao pia
kuwasaidia watu wasiojiweza ili wapate thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwafuturisha
viongozi wa dini mbalimbali mkoani Lindi.
Mama Kikwete alisema
kuwa kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani ni kipindi cha kuomba na kutubu
dhambi ili yule aliyefunga aweze kujiunganisha na Mwenyezi Mungu.
“Ibada na maombi yenu viendane na kutoka sadaka, wahudumieni watoto
yatima, wagonjwa na watu wasiojiweza, muwe watu wa upendo kwani mahali penye
upendo hakuna chuki, vita wala mafarakano”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa
kila mwaka wamekuwa na utaratibu wa kufuturu kwa pamoja na viongozi wa dini
mbalimbali na kuwaombea kwa Mwenyezi
Mungu awajalie funga ya heri na
kuwazidishia huruma, upendo na mshikamano ndani ya mioyo yao.
Mama Kikwete pia
aliwataka viongozi hao wa dini kuhubiri amani kwa waumini wao na kuhakikisha
kuwa hawaipotezi amani kwa mambo yasiyo na
tija kwani kuna nchi waliichezea amani na
hivi sasa wanaishi kwa hofu na maisha ya
vita.
“Mjitahidi kila
mnapokuwa katika maeneo yenu ya ibada, sherehe na katika huzuni muhubiri juu ya
kuwepo kwa amani kwani pamoja na
umaskini wetu Tanzania tumejaliwa kuwa na amani kuna nchi ambazo ni matajiri lakini hawana amani na wananchi wake
wanaishi maisha ya mashaka na hofu”, alisisita
Mama Kikwete.
Kwa upande wake Shekhe
na Kadhi mkuu wa mkoa wa Lindi Mohamed Mushangani alimshukuru Mama Kikwete kwa
ajili ya futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa kufunga ni moja kati ya nguzo tano za dini ya Kiislamu na hiyo ni
nguzo ya nne.
“Amri ya kufunga iliyotolewa na Mtume Swalallahu Alayhi Wassalam
(S.A.W) akiwa madina mwaka wa pili ndipo ilipoteremka amri hii hivyo basi
waislamu wenye afya njema wanatakiwa kufunga”, alisema Shekhe Mushangani.
Aliendelea kusema kuwa
mtu anayefunga na kuwa na hali ya
kuamini na kutarajia thawabu anasamehewa makosa ya mwaka wote uliopita nyuma na
mfungo mosi anaanza upya kuhesabiwa dhambi zake.
No comments:
Post a Comment