Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Handeni
Juhudi zinazochukuliwa na mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, za kutoa elimu juu
ya Sera ya Polisi Jamii na Ulinzi Shikishi nchini kwa kuwashirikisha
wadau mbalimbali zinazaa matunda karibu kila pembe ya nchi yetu.
Hayo yamedhihirika baada ya Wafanyabiashara wilayani Handeni katika
mkoa wa Tanga, kuamua kwa hiari yao kuwachangia Polisi kwa vifaa
ambavyo navyo vinatolewa kwa vikundi vya Polisi Jamii wilayani humo.
Wafanyabiashara hao wametoa vitendea kazi kama vile, tochi na
betrii ili ziwasaidie Polisi lakini pia Mkuu wa polisi wilayani Handeni
SP Zuberi Chembera, kwa kujua umuhimu wa Polisi Jamii naye ameamua kutoa
msaada huo kwa vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na ulinzi
mitaani.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu huyo
wa Polisi wilayani handeni amesema kuwa ameamua kukabidhi sehemu ya
misaada hiyo kwa kutambua kuwa Vikundi vya Ulinzi ni msaada mkubwa kwa
Jeshi la Polisi katika kukomesha uhalifu nchini.
Amesema ofisi yake itajitahidi kutoa kila aina ya msaada kwa
vikundi hivyo vya Polisi Jamii ili navyo viweze kuimarisha na kudumisha
usalama katika maeneo yao.
Aidha SP Chembera ametoa wito kwa wananchi mbalimbali wilayani humo
pia kuwaunga mkono katika kuvisaidia vikundi hivyo ambavyo amesema ni
muhimu kuwepo ndani ya Jamii zetu katika kulinda usalama wa watu na mali
zao kama ilivyo kwa jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment