Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi ili kufanya uamuzi wenye manufaa kwa washabiki wa mpira wa
miguu baada ya tarehe ya uchaguzi aliyotangaza kuingilia na mechi ya
watani wa jadi (Simba na Yanga) ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Sekretarieti
ya TFF imepokea maoni kutoka kwa wapenzi mbalimbali wa mpira wa miguu
wakiomba matukio hayo mawili (Uchaguzi wa TFF na mechi ya Simba na
Yanga) yafanyike katika siku tofauti.
Wakati
Kamati ya Uchaguzi inatangaza uchaguzi kufanyika Oktoba 20 mwaka huu
tayari ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ilikuwa imeshatoka, na ikionesha
kuwa timu ambazo zina historia ya kipekee katika mpira wa miguu
zitacheza siku hiyo.
Sekretarieti
imelazimika kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kwa vile yeye
na kamati yake ndiye wenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Uchaguzi. Huko
nyuma TFF imeshafanya mikutano huku kukiwa na mechi za timu ya Taifa
(Taifa Stars), jambo ambalo liliwezekana kutokana na mikutano hiyo kuwa
na ajenda moja tu.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ameitisha kikao cha kamati yake kujadili barua hiyo ya sekretarieti.
COCA COLA YATOA MIPIRA 100, FULANA 800
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa kampuni ya Coca
Cola kwa kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya
mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa
yanayoanza Septemba Mosi mwaka huu.
Coca
Cola ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya
ambapo mwaka huu yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa
kuanzia Septemba 7-14 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa
16 itakayokuwa imefanya vizuri katika ngazi ya kanda.
Kila
mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi
ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika
Septemba 6 mwaka huu.
Kanda
hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma,
Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,
Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.
Zanzibar
itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja
wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara,
Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.
Kanda
ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma
wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.
Mwanza
itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za
Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro
itaingiza timu mbili.
Wakati huo huo,
semina ya makocha 32 wa timu za mikoa zitakazoshiriki michuano ya U15
FIFA Copa Coca-Cola iliyokuwa ikiendeshwa na mkufunzi Govinder Thondoo
kutoka Mauritius inafungwa leo (Agosti 16 mwaka huu) saa 9 alasiri
kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MWANDISHI GRACEMO BAMBAZA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
aliyekuwa mwandishi wa habari za michezo wa Radio ABM ya Dodoma, Gracemo
Bambaza kilichotokea Agosti 14 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean
Road, Dar es Salaam.
Msiba
huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Bambaza
kwa kipindi chote akiwa mwandishi alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo
mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima.
Bambaza
aliyezaliwa mwaka 1973 na ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika vituo
vya redio vya Wapo cha Dar es Salaam na Pride cha Mtwara amesafirishwa
jana (Agosti 15 mwaka huu) kwenda Karagwe mkoani Kagera kwa ajili ya
mazishi.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bambaza, ABM Radio na Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Bambaza mahali pema peponi. Amina
TIKETI MECHI YA YANGA, AZAM KUUZWA ASUBUHI
Tiketi
kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam itakayochezwa
kesho (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitaanza
kuuzwa saa 3 asubuhi.
Vituo
vitakavyouza tiketi hizo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni
Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo,
Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barber Shop iliyoko
Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari yote yanayouza tiketi yatahamia uwanjani saa 7 kamili mchana.
Viingilio
katika mechi hiyo ni sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu
wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya
VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A
watalipa sh. 30,000.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment