JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
Siku za hivi karibuni, ongezeko la huduma za mawasiliano nchini limekuwa
kwa kasi sana. Huduma za mawasiliano nchini katika kipindi kifupi zimekuwa sana
na kuwafikia Watanzania wengi zaidi. Kutoka laini za simu za mkononi milioni tatu tu mwaka 2000 hadi kufikia laini
28,000,000.
Watanzania walio wengi hivi sasa wanafaidika kwa huduma za mawasiliano, yakiwemo
mawasiliano ya simu za mikononi, utangazaji. Vile vile huduma za ziada kama
kutuma na kupokea fedha kwa kutumia mitandao na simu za mkononi zimeongezeka
maradufu. Wananchi wengi wanapata huduma za kibenki kwa kutumia simu zao,
wanawasiliana kwa kutumia simu zao kupitia sauti, SMS na kadhalika.
Hali kadhalika kumekuwa na ongezeko la matumizi ya intaneti kwa
watanzania walio wengi kutoka watumiaji laki tatu miaka mitatu iliyopita hadi
watumiaji milioni 7.6 kwa takwimu za hivi karibuni. Wengi wa watumiaji wa
intaneti matumizi yao ni katika kujifunza na kujielimisha pamoja na matumizi ya
mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, BBM, LinkedIn na blog
mbalimbali zinazotoa habari mbalimbali zikiwemo za kimaendeleo, burudani pamoja
na michezo.
Matumizi haya ya intaneti yamewanufaisha watanzaia walio wengi kwani ni
fursa murua ya kujifunza kupitia mitandao hiyo ya kijamii kwa kupata habari
mpya, kujifunza na kuelimishana kuhusu shughuli za maendeleo na kuleta amani
miongoni mwa watanzania.
Hata hivyo pamoja na maendeleo haya, kumekuwepo na baadhi ya watu
wachache wanaotumia mawasiliano ya simu, mitandao ya kijamii, redio, TV na
mawasiliano mengine kwa lengo la kuvuruga amani, kuchocheo vurugu,
kuchonganisha watu, kusababisha ugomvi, kuwaumiza wengine kwa mambo yasiyo na
ukweli, kupotosha jamii na hata kuvuruga maendeleo kwa ujumla.
Leo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) inazindua kampeni ya kuelimisha umma kuhusu matumizi mazuri ya
mawasiliano na inawatahadharisha wananchi kwamba kutumia mawasiliano vibaya
kama ilivyoainishwa katika sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta
(EPOCA) ya mwaka 2010 ni makosa. Katika kampeni hii, Mamlaka inakusudia
kuwasihi wananchi kuhakikisha wanatumia mawasiliano vizuri ili kudumisha amani,
mshikamano na upendo miongoni mwa watanzania.
Katika uzinduzi huu, Mamlaka
imewaalika baadhi ya watumiaji mahiri wa mitandao ya kijamii ambao wamekuwa
mstari wa mbele kuhakikisha watanzania walio wengi wanafaidika na mawasiliano.
Miongoni mwao wako wamiliki wa blog mbalimbali, wasimamizi wa makundi
mbalimbali katika mtandao wa FB na mengineyo. Nia ya Mamlaka ni kuomba
ushirikiano kwao ili waweze kushiriki katika kampeni hii na kuwahamasisha
mashabiki wao kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili kunufaisha Taifa letu kwa
matumizi mazuri.
Watumiaji wa simu za mkononi na wananchi wote wanashauriwa
kuunga mkono juhudi zinazofanyika ili kufanikisha kampeni hii kwa ajili ya
kudumisha na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha maendeleo ya sekta ya
Mawasiliano inaendelea kuchangia uchumi wa Taifa na kuiweka Tanzania katika
mazingira mazuri zaidi kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
Mamlaka ya mawasiliano TaNzania
31 Julai 2013
No comments:
Post a Comment