KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Tuesday, August 6, 2013

RUKSA 3PILLARS KUCHEZA MECHI ZA KIRAFIKI.

Timu ya 3Pillars Football Club ya Nigeria sasa inaruhusiwa kucheza mechi za kirafiki nchini baada ya kupata idhini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Nigeria (NFF).

Awali tuliikatalia timu hiyo kucheza mechi za kirafiki nchini kwa vile haikuwa na barua kutoka NFF, lakini sasa Shirikisho hilo limetoa idhini hiyo. Pia ziara yake haikuwa inaratibiwa na wakala wa mechi anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) au mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Klabu hiyo kutoka Jimbo la Lagos ilipanga ziara hiyo kwa kuwasiliana na chama cha mpira wa miguu cha jimbo hilo ambacho nacho kilitakiwa kuomba idhini NFF kwa niaba ya 3Pillars.

Hivyo timu hiyo inaweza kucheza mechi, kwani ziara hiyo sasa inaratibiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ambaye ni mwanachama wetu.

Tunapenda kukumbusha kuwa watu pekee wanaotakiwa kuandaa mechi za kirafiki za kimataifa ni mawakala wa mechi wanaotambuliwa na FIFA au wanachama wa TFF.

USAJILI WA WACHEZAJI HATUA YA KWANZA WAMALIZIKA
Hatua ya kwanza ya usajili wa wachezaji kwa msimu wa 2013/2014 imefungwa rasmi jana (Agosti 5 mwaka huu) ambapo klabu zote za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zimewasilisha usajili wa vikosi vyao ndani ya wakati.

Baadhi ya klabu zimefanya makosa madogo madogo katika usajili ambapo zimepewa siku ya leo (Agosti 6 mwaka huu) kufanyia marekebisho kasoro hizo. Hivyo kesho (Agosti 7 mwaka huu) majina ya vikosi vyote yatabandikwa kwenye mbao za matangazo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kipindi cha pingamizi kitakachomalizika Agosti 12 mwaka huu.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa itakutana Agosti 13 na 14 mwaka huu kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa wachezaji wenye matatizo.

Hatua ya pili ya usajili itaanza tena Agosti 14 mwaka huu ikihusisha wachezaji ambao watakuwa hawajasajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na wale kutoka nje ya Tanzania. Hivyo, dirisha la uhamisho kwa wachezaji wa kimataifa litafungwa baada ya hatua ya pili ya usajili kumalizika Agosti 29 mwaka huu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments: