KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Thursday, August 15, 2013

YANGA, AZAM KUVAANA NGAO YA JAMII J’MOSI.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga na makamu bingwa Azam wanavaana keshokutwa (Jumamosi) kwenye mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa 2013/2014.

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa kivutio kwa wapenzi wa mpira wa miguu nchini itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni ambapo mshindi atakabidhiwa ngao.

Iwapo dakika 90 za mechi hiyo hazitatoa mshindi, timu hizo zitatenganishwa kwa mikwaju ya penalti huku asilimia 10 ya mapato ya mechi hiyo yakienda kwa kituo cha kulelea watoto cha SOS.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000.

LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA SEPT 14
Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoshirikisha timu 24 zilizogawanywa katika makundi matatu msimu huu (2013/2014) itaanza kutimua vumbi Septemba 14 mwaka huu.

Kila timu itakayoongoza kundi lake katika ligi itakayochezwa kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini) ndiyo itakayopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2014/2015.

Mechi za ufunguzi kwa kundi A zitakuwa kati ya Tessema vs Green Warriors (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam) wakati Septemba 15 mwaka huu ni Transit Camp vs Polisi Dar (Uwanja wa Mabatini, Pwani), Ndanda vs Friends Rangers (Uwanja wa Nangwanda, Mtwara) wakati Villa Squad vs African Lyon itachezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Kundi B ni Burkina Faso vs Polisi Moro (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Mkamba Rangers vs Lipuli (Uwanja wa CCM Mkamba, Morogoro), Majimaji vs Mlale JKT (Uwanja wa Majimaji, Songea) wakati Septemba 15 mwaka huu Kimondo SC vs Kurugenzi (Uwanja wa Sokoine, Mbeya).

Mechi za ufunguzi kundi C ni Polisi Mara vs Polisi Dodoma (Uwanja wa Karume, Musoma), Kanembwa JKT vs Polisi Tabora (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Stand United vs Mwadui (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), na Pamba vs Toto Africans (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza).

Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Oktoba 26 mwaka huu wakati wa pili utamalizika Machi 22 mwakani. (Ratiba imeambatanishwa)

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments: