Mechi
ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa wanawake
chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini iliyokuwa ichezwe
Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada
ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho ambayo hayawezi
kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo inatakiwa kuchezwa.
Vyumba
vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa.
KILIMANJARO
STARS YATUA SALAMA NAIROBI
Timu
ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya tayari kwa
mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27 mwaka huu) katika
Uwanja wa Nyayo.
Kilimanjaro
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku kwa
ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko katikati ya
Jiji la Nairobi.
Kwa
mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo (Novemba 26
mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi kujiandaa kwa mechi yake
ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa
Machakos.
WANNE WASHINDA
UCHAGUZI CECAFA
Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata wajumbe
wapya wa wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya leo (Novemba 26
mwaka huu) hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi
huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake
Leodegar Tenga na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais
wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence
Mulindwa ndiye aliyeongoza katika uchaguzi huo ambapo wasimamizi walikuwa
Bwalya na Maradas.
Mulindwa
alipata kura zote 12 na kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10), Abdigaani Saeb
Arab wa Somalia (9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Atta, Arab na Gisanura
walikuwa wakitetea nafasi zao.
Walioshindwa
ni Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor aliyepata
kura tano na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya
aliyepata kura nne.
MICHUANO YA
UHAI YAHAMIA CHAMAZI
Michuano
ya Kombe la Uhai imeingia hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi zinachezwa
kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam.
Uamuzi
wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote
kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa
wameathirika kutokana na uamuzi huo.
USAJILI
DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15
Wakati
dirisha dogo la usajili linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia
muda uliowekwa.
Pia
tunakumbusha kuwa kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi
nafasi ya kusajili mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30 maana yake ni
kuwa haina nafasi ya kuongeza wachezaji.
Kwa
upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), tunakumbusha kuwa kuanzia
msimu ujao 2014/2015 watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.
Kuhusu
usajili wa wachezaji kutoka nje mpaka sasa hakuna hata klabu moja imeshaingia
kwenye TMS kuomba uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system ya TMS itafunga.
RAMBIRAMBI
MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha
mwamuzi wa zamani wa FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa,
Ramadhan Mahano, Kiloyi alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka huu) kutoka na
ugonjwa wa fangasi ya ubongo, na marehemu amesafirishwa kwenda kwao Kigoma
ambapo atazikwa.
Kiloyi
alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988 ambapo
alipata beji ya FIFA mwaka 2001 akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka
2009, na hadi anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu, IREFA,
ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa na moyo wa
subira na uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu aiweka mahali pema
roho ya marehemu Kiloyi.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment