Kaimu Mkurugenzi wa shughuli za kitakwimu
Bi.Aldegunda Komba.
Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
Dar es
salaam.
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu imesema kuwa itaendelea na jukumu la kukusanya na kutoa takwimu Bora zinazokidhi
mahitaji na viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuiwezesha serikali na wadau
mbalimbali kufanya maamuzi sahihi katika mipango ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi wa shughuli za kitakwimu
Bi.Aldegunda Komba wakati akitoa ufafanuzi wa ushiriki wa Tanzania katika
maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika kwa mwaka 2013.
Bi. Aldegunda amesema maendeleo ya serikali yoyote ile duniani
yanategemea uwepo wa takwimu Bora ambazo hurahisisha utungaji wa sera sahihi na
upangaji wa mipango ya maendeleo ya wananchi kwa kufuata vipaumbele na fursa
zilizopo.
Ameongeza kuwa takwimu
bora huiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi na kutathmini mwenendo na
mafanikio ya mipango mbalimbali inayopangwa na kukidhi mahitaji ya wadau
mbalimbali kwa kuwapatia taarifa za Afya, kilimo, watu na makazi, taarifa za
mapato na matumizi ya kaya.
Amesema Tanzania ikiwa
miongoni mwa nchi zinazothamini mchango wa takwimu kwa maendeleo ya taifa
inaungana na mataifa mengine barani Afrika kuadhimisha Siku ya Takwimu Afrika
ambayo huadhimishwa tarehe 18 Novemba.
Ameeleza kuwa hiyo
nchini Tanzania itaadhimishwa tarehe 20 jijini Dar es salaam chini ya kauli
mbiu isemayo “Takwimu Bora kwa Maendeleo ya Afrika” ikilenga kuifahamisha jamii juu ya umuhimu wa matumizi
ya Takwimu bora katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
Kuhusu ufanisi wa
ukusanyaji wa takwimu Bora wa Tanzanzania ikilinganishwa nan chi nyingine
barani Afrika Bi. Aldegunda amefafanua Ofisi ya Taifa ya Takwimu hutoa takwimu
zake kwa kuzingatia sifa mbalimbali za upataji wa takwimu bora zikiwemo za matumizi
ya mbinu na viwango vinavyokubalika kimataifa.
Pia ameongeza kuwa takwimu
zote zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu huakisi hali halisi ya eneo
husika pia takwimu hizo hutolewa kwa wakati
maalum.
No comments:
Post a Comment