Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi (kushoto) akitoa tamko la Serikali kuhusu Siku ya Ugonjwa wa Kisukari Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14. Kulia ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Seif Rashid.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es
salaam.
Watanzania wametakiwa
kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kupima afya na kuepuka
tabia hatarishi zinazochangia uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein
Mwinyi wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu Siku ya Ugonjwa wa Kisukari
Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14.
Amesema Tanzania kama
zilivyo nchi nyingine inaadhimisha siku hiyo kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa kisukari Tanzania kutoa elimu ya
umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhra mbalimbali yatokanayo na ugonjwa huo.
Amesema maadhimisho ya
Siku ya Kisukari Duniani 2013 yataongozwa na kauli mbiu isemayo “Linda Maisha
yajayo dhidi ya Ugonjwa kisukari” inayolenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo
mbalimbali yanayotokana na ugonjwa wa kisukari katika jamii.
Ameeleza kuwa athari za ugonjwa wa kisukari katika mwili wa
binadamu hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha
kawaida kwa muda mrefu na kuongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikua na
wagonjwa milioni 246 duniani huku mwaka 2012 kukiwa na wagonjwa milioni 371
ambapo nusu ya idadi ya wagonjwa hao walikua hawajaanza kupata matibabu.
Kuhusu dalili za
ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni
rahisi kuzitambua na huambatana na mgonjwa kuwa na kiu isiyoisha, kukojoa mara
kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu na
kuongeza kuwa athari za ugonjwa huo ni kubwa kutokana na ugonjwa huo kuharibu
mishipa ya damu na fahamu, macho, figo, kusababisha upofu, moyo na figo
kushindwa kufanya kazi na miguu kufa nganzi na kuwa na vidonda.
Dkt. Mwinyi ameeleza
kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wote duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo
Tanzania na kuongeza kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2012 nchini Tanzania kwa
kuzihusisha wilaya 50 unaonyesha kuwa asilimia 9.1 ya watanzania wenye umri wa
miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
“Ni jambo lililo wazi
kuwa lazima tubadili tabia hasa tabia hatarishi zinazochangia ugonjwa wa
kisukari zikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi, ulaji usiofaa, ulaji usiofaa
na tabia ya kupuuza kufanya mazoezi”, sasa Tanzania katika nchi 10 za Afrika zinazoongoza
kwa kisukari barani Afrika inashika nafasi ya 8” Amesema Dkt. Mwinyi.
Kuhusu sababu
zinazochangia ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na tabia ya ulaji
usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi , mafuta na sukari, uzito uliozidi,
unene uliokithiri, kutofanya mazoezi , uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo
na tumbaku pamoja, kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yatokanayo na wanyama,
sukari nyingi,kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka, kutokula mbogamboga na
matunda na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Ameeleza kuwa jamii
inapaswa kuepuka mambo yanayochangia chakula kilicholiwa kutotumika vizuri ikiwemo
tabia ya kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi huku akisisitiza kuwa unywaji wa
pombe kupita kiasi huharibu maini na kusababisha utapiamlo kwa wale wanaoishia
kunywa pombe Zaidi bila kula chakula.
“ Natoa ushauri hasa
kwa watumishi kuepuka kuketi ofisini, darasani au kuangalia runinga kwa muda mrefu na hata kutumia lifti kwenda
ghorofani badala ya ngazi na matumizi ya magari katika umbali mfupi unaoweza
kufikika kwa kutembea tu”
Dkt. Mwinyi ameleza
kuwa serikali imejipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na
ugonjwa huo na kusisitiza kuwa utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007
unaendelea kwa kuhakikisha kuwa utoaji wa hudunma za magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ikiwemo kisukari unafanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa serikali
kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari kuanzia mwaka 1983 ilitoa msamaha wa matibabu
kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu pia kuhakikisha
kuwa dawa muhimu zinapatikana katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini.
Kwa upande wake Mganga
mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbando amewataka vijana kote nchini ambao ni kundi
kubwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuepuka maisha ya
anasa ambayo huwaweka katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.
Amesema mapambano ya
ugonjwa wa kisukari yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi hasa kuzingatia
kanuni za Afya na kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara mara.
No comments:
Post a Comment