Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
Dar es
salaam.
Serikali imewataka
wananchi kuzitumia ipasavyo fursa za elimu zinazotolewa kupitia programu mbalimbali
za ikiwemo Elimu ya Watu Wazima (EWW) na ile ya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi
(ENMRA) ili kupunguza tatizo la umasikini, maradhi na ujinga.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Said Meck Sadiki
wakati akitoa taarifa kwa wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kuhusu Maadhimisho
ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yatakayofanyika jijini
Dar es salaam kuanzia Novemba 13, 2013 yakiongozwa na kauli mbiu “Kisomo kwa
ajili ya Karne ya 21”
Amesema serikali imeanzisha programu mbalimbali za
elimu kuanzia msingi mpaka sekondari kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata
fursa hiyo na kuondokana na tatizo Umaskini, maradhi na ujinga na kuwawezesha
kujikwamua kiuchumi, Kijamii, Kisiasa na
Kiutamaduni.
Ameeleza kuwa mkoa wa Dar
es salaam kwa sasa unaratibu program mbalimbali zikiwemo Mpango wa Elimu ya
Msingi kwa walioikosa (MEMKWA) unaowahusisha wanafunzi wenye umri kati ya miaka
9 hadi 18 ambao husoma katika mfumo wa makundi rika.
Amesema jumla ya wanafunzi 1,846 wamejiunga na program
hiyo kwa mwaka 2013 wakihusiha wale wenye umri wa miaka 9 mpaka 13 na 14 mpaka
18.
Bw. Meck Sadiki
ameeleza kuwa mkoa wa Dar es salaam pia unasimamia Mpango wa Uwiano kati ya
Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) unaohusu utoaji wa Elimu kupitia kisomo
cha kujiendeleza na kisomo chenye manufaa kinachowahusisha watu wazima wenye
umri zaidi ya miaka 18 wapatao 1,678 waliojiunga kwa mwaka 2013.
Ameongeza kuwa
wanafunzi wapatao 2,309 wamejiunga na programu ya Elimu ya Sekondari Huria
(PESH) ambayo huendeshwa kwa wanafunzi ambao wamekosa sifa za kuchaguliwa
kujiunga na shule za sekondari kupitia chaguo la mfumo rasmi.
“Wanafunzi wanaosoma
katika mpango wa PESH serikali imewawekea utaratibu wa kusoma katika shule za
msingi na sekondari ambazo hazina utaratibu wa awamu mbili za kusoma, wao
husoma jioni baada ya muda wa kawaida wa masomo”
Aidha amezitaja
programu nyingine za elimu zinazowahusisha watu wazima na vijana kuwa ni pamoja na Elimu ya Masafa na
Ana kwa Ana (ODL) ambayo ina jumla ya wanafunzi 335 wanaoendelea na masomo na
Elimu Changamani (IPPE) ambayo inawahusisha vijana 112 waliomaliza elimu ya
msingi na kukosa nafasi ya kujiunga na sekondari ambao hujengewa uwezo katika
masomo ya maarifa, ufundi, afya, maktaba na mazingira.
Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu Bw. Mecki Sadiki
ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine yatakuwa na mchango mkubwa katika
kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu kusikiliza, kusoma na kutoa maoni ya
upatikanaji wa katiba mpya nchini, kuongeza mwamko kwa jamii katika masuala ya
elimu, kutathmini utekelezaji wa azimio la ulimwengu kuhusu utoaji wa elimu kwa
wote na kutathmini mafanikio na mapungufu ya utekelezaji wa Elimu ya Watu Wazima
(EWW) na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (ENMRA).
No comments:
Post a Comment