* Sikinde yajichimbia Bagamoyo
Na Badru Kimwaga
HOMA ya pambano la watani wa jadi
katika muziki wa dansi nchini kati ya Mlimani Park 'Wana Sikinde' na Msondo
Ngoma 'Baba ya Muziki' litakalofanyika siku ya Krismasi imeanza kupanda kwa
bendi hizo kujificha kambini na huku wakipigana vijembe.
Bendi hizo kongwe nchini
zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika onyesho litakalofanyika kwenye viwanja wa
TCC Club Chang'ombe, Temeke Dar es Salaam katika kunogesha sikukuu hiyo ya
Krismasi.
Katika kuonyesha wamelipania pambano
hilo bendi ya Sikinde tayari imeiendea Msondo wilayani Bagamoyo kwa ajili ya
kuweka kambi yao na wamewatahadharisha 'mahasimu' wao hao wasije wakatoa
visingizio baada ya kugaragazwa kwenye onyesho hilo.
"Sisi tumeamua kuweka kambi
yetu mjini Bagamoyo ambako tutatua viwanja vya TCC kutokea huko ili
kuisambaratisha Msondo, na tunataka wajipange sawasawa ili wasije wakatoa
visingizio tena kwa maana kama vyombo vipya bendi zote imepewa na Konyagi,"
Katibu wa Sikinde, Hamis Milambo alisema.
Milambo alisema mashabiki wa dansi
wajitokeze kwa wingi kushuhudia namna gani wanavyowachachafya wapinzani wao
hao, ikizingatiwa hawajakutana kwa muda tangu mwaka jana.
Upande wa Msondo kupitia Meneja wao,
Said Kibiriti, alisema hawana haja ya kutaja mahali kambi yao ilipo isipokuwa
wamejiandaa kuwatoa nishai wapinzani wao siku ya onyesho hilo litakaloanza saa
nane mchana.
"Sisi hatuna mchecheto wowote
na mpambano huo, tunaendelea kujifua kimya kimya mahali ambapo siwezi kupataja
kwa sasa," alisema Kibiriti.
Naye muimbaji anayekuja juu wa bendi
hiyo ya Msondo alitokea Sikinde, Athuman Kambi, alisema amejipanga kuonyesha
umahiri wake katika mpambano huo baada ya kufanya hivyo wakati akiwa Sikinde
dhidi ya Msondo kwenye ukumbi wa Diamond na kuwawehusha mashabiki wa muziki wa
dansi nchini.
"Najua watu watataka kuona
nafanya kitu gani dhidi ya bendi yangu ya zamani iliyonitangaza vyema, wasiwe
na hofu waje Desemba 25 waone nini nitakachofanya TCC Club Chang'ombe,"
alisema Kambi.
Mpambano huo wa Sikinde na Msondo
umeandaliwa na kampuni ya Bob Entertainment na Keen Arts chini ya udhamini wa
Konyagi, gazeti la NIPASHE, Integrated Communications, CXC Africa na Salute5.
No comments:
Post a Comment