*Asema sasa ni fundisho kwa watakaolala*ziara za Kinana zimesaidia sana kutatua kero
*Bado moto wa ziara hizo haujapamba*2015 CCM kurejesha viti vya ubunge, Udiwani vilivyoko upinzani
NA BASHIR NKOROMO
KATIBU
wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amesema amepokea kwa faraja
kubwa, hatua ya mawaziri wanne kuenguliwa nyadhifa zao kwa ridhaa ya
Rais Jakaya Kikwete.
"Najisikia vizuri, maana kwa kitendo cha mawaziri hao wanne
kuchuliwa hatua, ninaamini kitasaidia wale wengine waliolala nao waamke.
Bila shaka sasa hakuna atakayelala na akilala anajua itakula kwake.",
alisema Nape akijibu swali la mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha
ITV, Emmanuel Buhohela, kwenye kipindi cha 'mahijiano' cha televisheni
hiyo, mjini Dar es Salaam, leo asubuhi.
Mtangazaji huyo alitaka kujua, Nape kama kiongozi wa ngazi ya juu CCM, amejisikia au kupokeaje hatua ya Bunge
kumuomba
Rais kuwawajibisha mawaziri hao wanne na kisha Rais kuridhia ombi hilo
kwa kutengua uteuzi wake wa nafasi za mawaziri hao jana.
Mawaziri waliofutiwa uteuzi wao na Rais na nafasi walizotoka zikiwa
kwenye mabano ni, Dk. Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani),
Shamsi Vuai (Waziri wa Ulinzi), Mathayo David Mathayo ( Mifugo na
Maendeleo ya Uvuvi) na Khams Kagasheki (Maliasili na Utalii) ambaye
ndiye pekee pamoja na uteuzi wake kutenguliwa na Rais lakini alitangaza
kujiuzulu akiwa Bungeni, jana.
Kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao kulitangazwa rasmi Bungeni
jana jioni, na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hatua inayoaminika kuwa
imetokana na shinikizo la bunge, baada ya Kamati yake ya Kudumu ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira kubaini 'uozo' katika operesheni
iliyofanyika hivi karibuni ya tokomeza ujangili.
Chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli, Kamati hiyo ilieleza kwamba
pamoja na mambo kadhaa iliyoyaeleza kuwa ya hovyo yaliyojitokeza kwenye
operesheni hiyo, vitendo vingi ikiwemo ubakaji na udhalilishaji
vilifanyika ambapo ni kinyume na utu na haki za binadamu.
Kufuatia kadhia hiyo, Kamati hiyo kupitia kwa Lembeli, iliwataka
mawaziri wanaohusika kutazama kama wanafaa kuendelea na nyadhifa zao au
wajiuzulu, na pia Kamati hiyo ikaenda mbali zaidi kwa kumuomba Rais
Jakaya Kikwete kuchukua hatua ya kuwawajibisha.
Akizungumzia zaidi hatua hiyo, Nape alisema, pamoja na mawaziri hao
kuwajibika, lakini ipo haja ya kwenda mbali zaidi kwa kutazama mifumo na
sheria zilizopo sasa kwa kuwa inaonekana navyo ni miongoni mwa vyanzo
vya vikwazo katika utekelezaji wa utawala bora.
"Kwa mfano leo hii, mawaziri wameng'oka, sawa ni jambo jema,
sitetei, lakini inawezekana kabisa kuna mifumo na sheria ambazo
zilimkwaza Waziri huyu kutimiza wajibu wake. Mfano, alihitaji kumfukuza
mtu kazi kwa kuzembea jambo fulani, lakini malmaka ya kufukuza kazi
mtumishi yapo kwa Katibu Mkuu wa Wizara, hapa atafanyaje!", alisema Nape
na kuongeza;
"La msingi hapa ni lazima sasa hatua hizi ziende mpaka chini huku
kwa watendaji, ili isiwe mawaziri wanawajibishwa tu kwa sababu ya
dhamana zao za kusimamia kisiasa, huku watendaji wanazidi kuvuta shuka
bila hofu wakati baadhi yao ni sehemu ya matatizo".
Akijibu swali kuhusu ziara za Katibu Mkuu na sekretarieti ya CCM
mikoani, Nape alisema, ziara hizo ndiyo kwanza zimeanza, na mado moto
wake mkubwa zaidi unakuja hasa itakapokaribia uchaguzi mkuu wa 2015.
Nape
alisema, ziara hizo, zimeonyesha matunda makubwa sana, klwa kuwa
zimesaidia kupunguza kero nhyingi katika maeneo zilikofanyika.
Alitoa mfano wa ziara hiyo ilivyoweza kuondoa msongamano wa malori
wilayani Tunduma mkoani Mbeya, akisema kwamba wakati Kinana na msafara
wake wanaingia tunduma walikuta msongamano ni mkubwa sana kutokana na
wafanyakazi wanaohudumia malori hayo kufanya kazi kwa mda mfupi.
"Baada ya kuiagiza serikali isimamie wafanyakazi wa eneo hilo
wafanya kazi kwa saa 24, kwa zamu, siku ya pili yake ya agizo hilo,
msongamano ulionekana kupungua sana na kuleta nafuu kwa madereva na
wafanya biashara kwa jumla pale Tunduma", alisema Nape.
Nape alisema, pia kutokana na ziara hizo, mgogoro uliokuwa mkubwa
baina ya wananchi na wenye mgodi wa machimbo Nyamongo, umepungua kwa
asilimia 90 sasa, na hali imekuwa ya kuridgisha sana.
Akizungumzia
wabunge wanaodaiwa kulipwa posho bila kuzifanyia kazi, Nape alisema,
kurudisha fedha pekee hakutatosha, kwa upande wa CCM ambayo ndiyo yeneye
wabunge wengi itabidi ichukue hatua zaidi dhizi ya waliohusika na
kadhia hiyo bila kuoneka mtu.
Kuhusu ajira kwa vijana, Nape alaisema ili kutimiza hilo, ni lazima
viwanda vifufuliwe kwa dhati kabisha, ikiwa ni kuchukua hatua za
kuwanyang'anya wawekezaji waliochukua viwanda mbalimbali kwa lengo la
kuviendeleza lakini baadhi yao majengo ya viwanda hivyo wakayafanyia
shughuli zingine tofauti ikiwemo kuyageuza maghala.
Nape aliitaka pia serikali kupunguza au kuondoa kabisa urasimu
katika kupokea wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi hapa nchini
akisema, kwamba, kwa sasa vikwazo na urasimu bado ni vingi sana kiasi
kwamba wawekezaji waanakwazika na hivyo kupunguza kasi ya uwekezaji
ambao wakiongezeka haraka ajira kwa vijana nazo zitakua haraka.
Alisema, hatua ya sasa inayofanywa na CCM kusimamia serikali ni ya
kawaida kabisa kwa kuwa kazi hiyo haipaswi kufanya na wapinzani kwa kuwa
sera inayotekelezwa siyo yao, na wahaijui.
Nape aliahidi kwamba
katika uchaguzi zijazo CCM itakomba viti vyote vya ubunge na udiwani
vililivyopo sasa chini ya wapinzani, akisema, kwamba, baada ya wapinzani
kujaribiwa wameshindwa kuonyesha matunda yoyote ya kusaidia wananchi na
hivyo kutokuwa mbadala wa CCM.
No comments:
Post a Comment