KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Saturday, January 11, 2014

ASKARI POLISI WATAKIWA KUJIUNGA NA SACCOS.

Na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi.
Askari Polisi Nchini wametakiwa kujiunga na Chama cha kuweka na kukopa cha Usalama wa raia (URA SACCOS) ili kiweze kuwasaidia kujiendeleza kimaisha jambo ambalo litawafanya kuishi maisha bora pindi watakapostaafu utumishi wao katika Jeshi la Polisi.
 
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Utawala na Utumishi wa Jeshi la Polisi Thobias Andengenye wakati wa uchezeshaji wa bahati nasibu ya URA SACCOS iliyokuwa ikiendeshwa kwa lengo la kuwahamasisha Askari na familia zao kujiunga na chama hicho pamoja na kuboresha maisha ya wanachama wake.
 
Alisema watumishi wengi wamekuwa wakijisahau kujiwekea akiba pindi wanapokuwa kazini jambo ambalo limekuwa likiwafanya kuishi maisha ya tabu baada ya kumaliza utumishi wao hivyo kupitia chama hicho wataweza kujiwekea akiba ambayo itakuwa mkombozi wao hapo baadaye.
 
Kamishna Andengenye alisema SACCOS hiyo ni mkombozi kwa Askari Polisi nchini kwa kuwa inatoa gawio kwa wanachama wake tofauti na benki za kibiashara zilizopo hapa nchini jambo ambalo linawawezesha wanachama kuchukua mikopo mikubwa ikiwemo ya kujenga nyumba pamoja na ununuzi wa viwanja na mashamba.
 
Kwa upande wake Afisa Mnadhimu  wa Kitengo cha Ustawi wa jamii ndani ya Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Alli Omar alisema katika bahati nasibu hiyo watatoa pikipiki tano aina ya Boxer na Vyerehani 10 ambavyo vikitumika vyema vitaongeza ufanisi na kuwaongezea kipato.
 
“Zawadi hizi zitawasidia Askari wetu na familia zao kuwa wajasiriamali jambo ambalo litastawisha hali za Askari wetu na ambao hawatabahatika leo basi sikuzijazo wasisite kushiriki pamoja na kuongeza akiba zao” Alisema Omar.
 
Bahati nasibu hiyo ilisimamiwa na mwakilishi kutoka Bodi ya michezo ya kubahatisha nchini ambapo baadhi ya Askari waliojishindia zawadi katika bahati nasibu hiyo ambayo ilizinduliwa mwezi Septemba mwaka jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu Said Mwema wanatoka mikoa mbalimbali na vikosi vya Polisi ikiwemo Kikosi cha kutuliza ghasia, Chuo cha Polisi Dar es Salaam, STPU, Mtwara, Shinyanga na Zanzibar.

No comments: