Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
mwamuzi Methusela Msebula kilichotokea juzi (Januari 13 mwaka huu)
katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Mwamuzi
Msebula ambaye alikuwa mwamuzi daraja la kwanza (class one) alikuwa
akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari, maradhi ambayo yalimsababisha kuwa
nje ya uchezeshaji mechi za mpira wa miguu kwa karibu misimu miwili.
Msiba
huu ni mkubwa kwa jamii ya mpira wa miguu kwani, Msebula alitoa mchango
mkubwa katika fani ya uamuzi nchini, hivyo mchango wake tutaukumbuka
daima. Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo (Januari 15 mwaka huu) nyumbani
kwao Kanyigo, Bukoba mkoani Kagera.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Msebula, Chama cha Waamuzi wa
Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita
(GEREFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment