Na Anna Nkinda – Maelezo
Taasisi ya Fursa
ya Elimu (Opportunity Education
Foundation) ya nchini Marekani imetoa mchango wa dola za kimarekani laki moja
kwa ajili ya udhamini wa wanafunzi wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika
mazingira hatarishi katika shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo wilaya
ya Rufiji mkoani Pwani.
Fedha hizo ambazo ni zaidi ya shilingi milioni mia moja na sitini na mbili zitaweza kuwasomesha wanafunzi 75 kwa kipindi cha mwaka
mzima kwa kuwapatia malazi, chakula, sare za shule, viatu, shajara, vitabu na
mahitaji mengine ya kila siku ya mwanafunzi.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) ambao ndiyo wamiliki wa shule hiyo wakati wa hafla fupi ya
uzinduzi wa mradi wa laptop ndogo (tablets computer) uliofanyika shuleni hapo
jana.
Mama Kikwete pia alimpongeza Joe Ricketts ambaye ni mwanzilishi na mtendaji
mkuu wa Fursa ya Elimu kwa moyo wa
upendo alionao na dhamira ya kuisaidia jamii ya watanzania kwa kutambua kwamba
kupata elimu bora kwa wanafunzi wote ni ufunguo wa kuwa na afya bora, uchumi
imara, miundombinu bora na ya kutosha, jamii yenye uelewa jambo ambalo
litasababisha ustadi wa taifa kunasonga mbele.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alisema , “Kwa mantiki hiyo ningependa kusema kwamba kukosekana kwa fursa ya
kumpatia mtoto wa kike elimu bora ni kulikosesha taifa fursa ya maendeleo kwani
kadri mtoto wa kike anavyopata elimu ndivyo anavyoweza kupunguza vifo
vinavyotokana na uzazi na ataweza kuboresha uzazi wa mpango, afya ya mtoto na
kujiongezea kipato”.
Akizungumzia kuhusu mradi wa laptop
ndogo (tablets) ambapo shule hiyo ilipata 61 Mama Kikwete aliiomba Taasisi hiyo na
wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuangalia uwezekano wa kuongeza mitaala ya
mafunzo ya kitanzania ili iwasaidie wanafunzi kumudu masomo wanayofundishwa
darasani halikadhalika kuandaa mkakati wa kuzifikia shule zilizopo pembezoni
ambazo zinakuwa na uhaba wa walimu.
“Ninawaasa walimu na
wanafunzi wa shule hii na kupitia wanafunzi wa shule zitakazofaidika na mpango
huu kutumia vifaa hivi kwa mahitaji ya masomo kama ilivyokusudiwa na siyo
kupoteza muda kwa michezo isiyo na manufaa. Napenda mjione kama watu wenye
bahati ambao mmepata fursa ya kipekee ambayo wanafunzi wengi nchini hawana,
mvitunze vifaa hivi ili viwafae wanafunzi wengine watakaokuja baada yenu”,
alisisistiza Mama Kikwete.
Kwa upande wake Ricketts alisema
kwa mara ya kwanza alikuja nchini mwaka 2006 wakati anaelekea Serengeti alikuta mwalimu mmoja anafundisha
wanafunzi zaidi ya miamoja aliamua kuanzisha mahusiano na shule hiyo ambayo aliwapelekea vifaa
mbalimbali vya kufundishia.
Alisema lengo la kuanzishwa kwa Taasisi yake ni kutoa msaada
wa kielimu ikiwa na nia ya kufanya upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi
kutoka nchi zinazoendelea ili wale wanaotoka katika familia maskini waweze
kusoma na kupata ajira pale watakapokuwa wamemaliza masomo yao na hivyo
kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
“Vijana wadogo wanategemea
kupata elimu bora kwa kuwa elimu kwa
wanafunzi imegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni technolojia na mwanafunzi
mwenyewe kukuwa na kukomaa kiakili ili aweze
kufanya vizuri katika masomo yake.
Kama mradi huu utafanikiwa
walimu watakuwa na mwamko mkubwa wa kufundisha na nitahakikisha kuwa zinapatikana
laptop ndogo (tablets) za kutosha kwa ajili ya kusomea nchini kwani matokeo ya
maisha ya watoto wetu yanategemea elimu
wanayoipata” , alisema Ricketts.
Taasisi ya Fursa ya Elimu ilianzishwa mwaka 2005 na kusajiliwa
nchini mwaka 2006 walianza kufanya kazi na shule moja ya msingi na hadi kufikia
sasa shule 434 zikiwemo za Sekondari 33
zimenufaika kwa kupata vitabu, DVD na zana za kufundishia.
Kwa shule za sekondari
wanatoa mwongozo wa mwalimu ambao unamuongoza kirahisi jinsi ya kuwafundisha
wanafunzi , laptop ambazo zinamasomo yaliyorekodiwa ambayo ni ya sayansi,
hesabu, kiingereza na maarifa ya jamii ,projecta na Televisheni ambazo
zinasaidia kuonyesha masomo na vitabu na video inawasaidia wanafunzi kujifunza
somo la kiingereza kwa njia ya kusikiliza na kusoma.
Wanafunzi watakaonufaika na program hiyo
ni wa kidato cha pili kutoka shule za
Sekondari Ilboru,(Arusha) Mzumbe (Morogoro), Msalato, (Dodoma),FidelCastro (Pemba), WAMA -
Nakayama (Pwani), shule ya Sekondari ya wavulana Bwiru (Mwanza), J Ossian
(Bukoba), Laureatte
(Zanzibar), Notredame (Arusha) na Tusiime (Dar es Salaam).
(Zanzibar), Notredame (Arusha) na Tusiime (Dar es Salaam).
No comments:
Post a Comment