Na Anna Nkinda –
Maelezo
Tafiti
zilizofanyika mwaka 2010 zinaonyesha kila mwaka wanawake 6200 wanakutwa na
ugonjwa wa saratani ya mlango wa
kizazi kati ya hao 4000 wanapoteza
maisha kwa kuwa asilimia 10 ya wagonjwa hao wanaweza
kuhudhuria Hospitali kwa ajili ya kupata huduma na matibabu.
Kutokana na utafiti huo
Tanzania ni moja ya nchi yenye wagonjwa wengi wanausumbuliwa na ugonjwa wa
saratani ya mlango wa kizazi ukilinganisha na nchi nyingine zilizopo Afrika ya
Mashariki.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu
Mkurugenzi wa Kinga kutoka wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Neema Rusibamayilla
wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi ambayo
inafadhiliwa na Muungano wa Utepe wa Pinki , Utepe
mwekundu wa nchini Marekani uliofanyika leo katika
Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Dk. Rusibamayilla alisema
ugonjwa wa kansa ni tatizo hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania hii
inatokana na sababu mbalimbali zinazozuia watu wasipate vipimo vya ugonjwa hii
ikiwa ni pamoja na ukosekanaji wa taarifa za upimaji na utolewaji wa matibabu
ya saratani, upatikanaji wa vifaa tiba, utoaji wa huduma, upungufu wa watumishi wa huduma ya afya.
“Naamini mradi huu
utaweza kutatua baadhi ya changamoto zinazotukabili
kama kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu ugonjwa
huu na upatikanaji wa vipimo hii
itasaidia kutatuwa tatizo mapema na kupunguza vifo vya wanawake vinavyotokana na ugonjwa huu”,
alisema Dk. Rusibamayilla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano
wa Utepe wa Pinki , Utepe Mwekundu
ambao unafanya kazi na Taasisi ya George W. Bush Dk. Doyin Oluwole
aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa uongozi wake imara na kuamua kupambana na
tatizo la ugonjwa wa saratani na hasa saratani zinazowasumbua wanawake.
Dk. Oluwole alisema,
“Katika nchi zote tunazofanya kazi ikiwa ni pamoja na Tanzania malengo yetu ni
kuimarisha miundombinu ya afya iliyopo na kufanya kazi na wadau wa afya na
hakika tukiungana pamoja na kufanya kazi na watu wengi tutaweza kufika mbali
zaidi.
Tuungane kuzuia
saratani ya mlango wa kizazi kwani
wagonjwa wengi wa saratani ya shingo ya kizazi wako katika hatari kubwa ya
kupata maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi”.
Alisema watafanya
kazi na kuhakikisha wanafika nchi nzima hadi vijijini ili kuona wanawake wanapata elimu , vipimo na matibabu na
hivyo kuweza kuokoa maisha ya wanawake na wasichana ambao wanasumbuliwa na
ugonjwa huo.
Kwa upande wake Dk. Serafina
Mkuwa ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) alisema
lengo la kuzinduliwa kwa mradi huo ni kuihamasisha jamii ili iweze kufanya
uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.
“Tunatoa hamasa kwa
wanawake na wasichana wasiogope bali waweze kujitokeza kwa wingi na kupima kwani
ukipima na kutokutwa na tatizo utafanyiwa
tena uchunguzi baada ya miaka mitatu lakini ukipimwa na kukutwa na ugonjwa unaanza matibabu na ugonjwa huu kama utaanza
matibabu mapema utapona”, alisema Dk. Mkuwa.
Naye Mkurugenzi wa Uboreshaji Afya kutoka Taasisi
ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Dk. Sara Maongezi alisema taasisi hiyo imepewa jukumu la kuzungumza na viongozi wa ngazi ya
juu wa Serikali kuhusiana na ugonjwa huo.
“Tutaongea na kamati za
Bunge za Ukimwi na Ustawi wa jamii ili wakati
wa kujadili bajeti ya wizara ya Afya waangaliea zaidi kuhusu saratani na katika
ngazi ya mkoa tutawakusanya wataalam wa
afya kutoka mikoani na wilayani na kuwapa elimu”, alisema Dk. Maongezi.
Alizitaja dalili za
ugonjwa huo kuwa ni maumivu makali chini ya kitovu, kutokwa na maji machafu
ukeni, wakati wa kufanya tendo la ndoa mwanamke
atatokwa na damu na mwisho ni damu zinatoka zenyewe bila ya kufanya tendo la
ndoa.
Mwezi wa saba mwaka 2013
Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa zamani wa Marekani ambaye pia ni mwanzilishi
wa Taasisi ya George W. Bush walizindua Utepe
wa Pinki Utepe Mwekundu (PRRR) nchini nia ikiwa ni kuzisaidia nchi za Afrika
ikiwemo Tanzania kupunguza idadi ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa saratani
ya kizazi na matiti.
Utepe wa Pinki Utepe
Mwekundu ulitoa dola za Marekani milioni 1.2 fedha ambazo zitatumika katika
mradi huo ambao kwa mara ya kwanza utaanza katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na
Iringa.
Kampeni hiyo inafanywa chini
ya usimamizi wa wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na muungano
wa Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu, Taasisi ya WAMA, MEWATA, T-MARC,TAYOWA na Mtandao
wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi Mkoani Mbeya.
No comments:
Post a Comment