Mwamuzi Anthony Ogwayo mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu (FIFA) kutoka Kenya ndiye atakayechezesha mechi kati ya
Tanzania (Taifa Stars) na Burundi (Intamba Mu Rugamba) itakayochezwa
keshokutwa (Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ogwayo katika mechi hiyo ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, atasaidiwa na Gilbert Cheruiyot na Oliver
Odhiambo wote pia kutoka Kenya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Israel Mujuni
wa Tanzania.
Burundi inatarajia kuwasili nchini leo (Aprili 24 mwaka huu) saa 12
jioni kwa ndege ya Kenya Airways na itafanya mazoezi kesho (Aprili 25
mwaka huu) saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa.
Nayo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini
jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza
tangu kuanza kwa mpango wa maboresho wa timu hiyo.
Makocha wa timu zote mbili pamoja na manahodha wao kesho (Aprili 25
mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia
mechi hiyo.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya
chungwa, bluu na kijani. Kwa VIP A kiingilio kitakuwa sh. 20,000 wakati
VIP B na C ni sh. 10,000.
KOCHA MPYA STARS KUTUA JUMAMOSI
Kocha Mkuu mpya wa Taifa Stars, Martinus Ignatius Maria maarufu kama
Mart Nooij anatarajiwa kuwasili nchini Jumamosi alfajiri (Aprili 26
mwaka huu) tayari kwa ajili ya kuanza kazi ya kuinoa timu hiyo.
Nooij (59) atawasili saa 7.20 usiku kwa ndege ya Ethiopia Airlines
ambapo anatarajia kukutana na waandishi wa habari Jumamosi mchana, saa
chache kabla ya kuanza mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Burundi
itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment