KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Friday, April 4, 2014

SIMBA KUIVAA KAGERA SUGAR VPL.

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 24 kesho (Aprili 5 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo Kagera Sugar itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine itakuwa kati ya Mbeya City ambayo itakuwa mgeni wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam. Ashanti United inayofundishwa na Abdallah Kibaden ipo katika mkakati wa kukwepa kushuka daraja.

Keshokutwa (Aprili 6 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Coastal na Mgambo Shooting Stars (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT na Tanzania Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers na Mtibwa Sugar (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na Yanga dhidi ya JKT Ruvu (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam).

Raundi hiyo itakamilika Aprili 9 mwaka huu kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Azam itakayochezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
 
NI MWADUI AU STAND UNITED VPL MSIMU UJAO
Ni ipi kati ya timu za Mwadui na Stand United, zote za Shinyanga itakayocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao itajulikana kesho (Aprili 5 mwaka huu) baada ya kundi C kuhitimisha mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu.

Mwadui yenye pointi 28 ndiyo inayoongoza, na itacheza na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Nayo Stand United yenye pointi 26 itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Pamba na Kanembwa JKT itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Polisi Mara na Polisi Tabora zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Timu ambazo tayari zimepanda daraja kutoka FDL kucheza VPL msimu ujao ni Ndanda SC kutoka kundi A na Polisi Morogoro ya kundi B.

21 ZA KUCHEZA RCL ZAJULIKANA
Timu 21 kati ya 27 zitakazocheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kutafuta tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao tayari zimejulikana.

Timu hizo ni Abajalo SC (Dar es Salaam), AFC (Arusha), African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Geita Veterans (Geita), JKT Mafinga (Iringa), JKT Rwamukoma (Mara), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Milambo SC (Tabora) na Mshikamano FC (Dar es Salaam).

Nyingine ni Mvuvumwa FC (Kigoma), Navy SC (Dar es Salaam), Njombe Mji (Njombe), Pachoto Shooting Stars (Mtwara), Panone FC (Kilimanjaro), Singida United (Singida), Tanzanite (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi FC (Rukwa) na Volcano (Morogoro).

WATANO WAFANYA MTIHANI WA UWAKALA WA WACHEZAJI
Watanzania watano wamefanya mtihani wa uwakala wa wachezaji wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ulifanyika jana (Aprili 3 mwaka huu) duniani kote.

Watahiniwa katika mtihani huo ambao ulikuwa na maswali kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) walikuwa Godlisten Anderson, Jesse Koka, Lutfi Binkleb, Rwechungura Mutahaba na Silla Yalonde.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: