Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza
mechi ya kirafiki na Burundi (Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni
sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager tayari ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo
ikiwa na wachezaji waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.
Baadaye wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo
nje ya programu ya kusaka vipaji wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza
kikosi cha mwisho kitakachoivaa Burundi.
Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam itachezeshwa na waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu (FIFA) kutoka nchini Kenya.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI YACHACHAFYA BRAZIL
Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa
kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de
Janeiro nchini Brazil baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.
Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu
hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua
mshindi. Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.
Kwa
matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya
Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu.
Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho (Aprili 6 mwaka
huu).
Timu
nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka
huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.
Katika
mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika
Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines
mabao 2-0.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment