Na Anna Nkinda –
Maelezo, Lindi
18/4/2014 Vijana mkoani
Lindi wametakiwa kuacha tabia ya kuilalamika Serikali kuwa maisha ni magumu
bali watumie fursa zilizopo katika
maeneo yao kwa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili waweze kujiajiri na
hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Mwito huo umetolewa
jana na Mjumbe wa Baraza kuu na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCC)
taifa kutoka mkoa wa Lindi Jabiri Makame kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji
cha Mnazi mmoja wilaya ya Lindi Mjini kwa ajili ya
kuzipokea mbio za kizalendo za pikipiki na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Jabiri alisema vijana wengi wamekuwa wakiilalamika Serikali
kutokana na changamoto zinazowakabili na kusahau kuwa kazi ya Serikali ni
hakikisha kwamba inawaandalia mazingira mazuri ya wao kuweza kujikwamua
kiuchumi na kuweza kujiletea maendeleo
hii ni pamoja na kuwapatia mikopo .
“Halmashauri zetu zinatakiwa
kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kinamama na vijana naamini hata
Halmashauri za mkoa huu zinafanya hivyo lakini fedha hizo hazitolewi kiholela
ni lazima wahusika wajiunge katika
makundi yaliyosajiliwa kwa mfano kundi la madereva wa bodaboda, bajaji, kina
mama lishe na vikundi vya mpira pia vinaweza kuwa vya ujasiriamali na kuweza
kupata mkopo ambao watautumia katika shughuli zao za maendeleo”, alisema
Jabiri.
Kuhusu suala la uongozi
alisema Rais Kikwete anawaamini sana vijana na ndiyo maana amewateua na kushika
nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama na Serikali na kutoa mfano wa
mawaziri na wakuu wa wilaya.
Jabiri alisisistiza, “Katika
uchaguzi unaokuja wa Serikali za Mitaa na
Uchaguzi mkuu mwakani vijana wa CCM msiogope kuomba nafasi za uongozi wakati ukifika wajitokeze kuchukuwa fursa za
uongozi jambo la muhimu ni kutotangaza nia mapema subirini hadi wakati utakapofika”.
Kwa upande wake Mjumbe
wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo aliwapongeza UVCCM kwa kuandaa mbio hizo
za uzalendo kwani ni ukweli usiopingika kuwa Muungano wenye dhana ya kizalendo
na historia ya nchi unatimiza miaka 50 tarehe 26/4/2014.
Mama Kikwete alisema,
“Leo hii nchi kubwa zenye nguvu kiuchumi Duniani zinazungumzia suala la
kuungana ili kuimarisha nguvu yao ya pamoja , kwanini sisi tukubali kutengana?
Muungano wetu ni kigezo kizuri ndani ya Bara la Afrika na kote Duniani tusikubali kamwe kuuvunja
jambo kubwa hapa na la msingi ni kukaa kwa pamoja na kujadili hatimaye kupata
ufumbuzi yakinifu”.
MNEC huyo alisema
vijana wa CCM ndiyo wanaotegemewa kuwa viongozi hapo baadaye, walipoona kuna
watu wanataka kupotosha ukweli juu ya umuhimu na faida za kuwa na muundo wa
Serikali mbili wakaamua kuzunguka nchi nzima na kuunga mkono umuhimu wa nchi
kuwa na Serikali mbili na siyo moja wala tatu kama vinavyotaka vyama vingine
vya Siasa.
Naye Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Lindi Mzee Ally Mtopa alisema Mwenyezi
Mungu amemuumba binadamu katika umbo la mapenzi na kumpa akili ya kuweza kuchagua lipi alifuate
kati ya jema na baya hivyo ni muhimu kwao kuweza kuamua ni chama gani cha
kuweza kuingia na siyo kukurupuka.
“Sisi wanachama wa
chama cha Mapinduzi mkoa wa Lindi na Tanzania nzima tunaunga mkono muundo wa
Serikali mbili na kuwepo kwa muungano ambao umetuletea manufaa makubwa ikiwa ni
pamoja na watu kutoka Tanzania bara na Visiwani kuishi pamoja kwa amani na
upendo”, alisema Mzee Mtopa.
UVCC mikoa ya Lindi,
Ruvuma na Mtwara waliandaa mbio za uzalendo za pikipiki zenye kauli mbiu Miaka
50 ya Muungano Dumisha Muungano, vijana tutumie fursa zilizopo katika maeneo yetu.
Tanzania kwanza mengine baadaye ambazo zilizinduliwa mkoani Ruvuma katika
wilaya ya Namtumbo tarehe 13/4/2014 kumalizika mkoani Lindi tarehe 17/4/2014.
Mkoa wa Lindi
ulizipokea mbio hizo kutoka kwa UVCCM mkoa wa Mtwara makabidhiano yaliyofanyika
kata ya Madangwa na katika mkutano wa hadhara uliofanyika hapo jumla ya
wanachama watatu walijiunga na Chama hicho wawili kutoka chama cha Civic United
Front (CUF)
na mmoja kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) .
Lengo la mbio hizo ni kuwaenzi
waaasisi wa Taifa la Tanzania ambao ni
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani
Karume Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuwafikishia ujumbe
watanzania juu ya umuhimu wa muungano na
kuwaeleza wapi ulipotoka, ulipo na unakokwenda na vijana kutumia fursa zilizopo
kujiedeleza.
Katika mkutano huo
jumla ya wanachama wapya vijana 19 walijiunga na umoja huo, mmoja alirudisha kadi ya uanachama wa CHADEMA na kujiunga na
chama hicho.
No comments:
Post a Comment