Taifa Stars na Malawi (Flames) zinapambana kesho (Mei
27 mwaka huu) katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni.
Malawi tayari ipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
mechi hiyo wakati Taifa Stars iliyopiga kambi yake Tukuyu mkoani Mbeya
inawasili jijini Dar es Salaam kesho (Mei 27 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwa ndege
ya Air Tanzania.
Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 5,000 kwa
viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio
kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.
Hiyo itakuwa ni mechi ya mwisho ya majaribio kwa Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kabla ya kwenda jijini Harare
kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty
Warriors).
Malawi (Flames) inayonolewa na mchezaji wake wa zamani
Young Chidmozi nayo itakuwa inacheza mechi ya mwisho ya majaribio kabla ya
kwenda N’djamena kuikabili Chad.
U15 TANZANIA
NG’ARING’ARI AYG
Tanzania
imeendelea kung’ang’ara kwenye Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) kwa upande wa
mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya jana (Mei 25
mwaka huu) kuichapa Swaziland mabao 3-0.
Mabao
ya Tanzania katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Gaborone,
Botswana yalifungwa na Amani Ally dakika ya sita, Nasson Chanuka dakika ya 32
wakati Amos Kennedy alikamilisha ushindi huo kwa bao la dakika ya 53.
Katika
mechi yake ya kwanza, Tanzania ilitoka sare ya bao 1-1 na Mali na baadaye
kuwafunga wenyeji Botswana mabao 2-0. Mechi za michuano hiyo zinaoneshwa moja
kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
Tanzania
itacheza mechi yake ya nne kesho (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya Nigeria wakati
mechi ya mwisho itafanyika Mei 29 mwaka huu dhidi ya Afrika Kusini.
KOZI ZA UKOCHA LESENI A, B KUFANYIKA JUNI
Kocha a ukocha wa mpira wa miguu
kwa ajili ya Leseni A na B zinazotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) zitafanyika jijini Dar es Salaam
kuanzia Juni 2 mwaka huu.
Ada
kwa kozi ya Leseni A itakayoanza Julai 21 hadi 26 mwaka huu ni sh. 300,000
wakati ile ya Leseni B itakayofanyika kuanzia Juni 2 hadi 15 mwaka huu ni sh.
200,000. Maombi ya kushiriki kozi hizo yatumwe kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati kwa upande wa Zanzibar yatumwe kwa Katibu
Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kabla ya Mei 31 mwaka huu.
Washiriki
ambao watajitegemea kwa chakula watalipa ada hizo wakati wa usajili
utakaofanyika Juni 1 mwaka huu kwa upande wa Leseni B na Leseni A watalipa
Julai 20 mwaka huu vilevile wakati wa usajili.
TFF
itatoa malazi kwa washiriki kwenye hoteli yake iliyopo Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume wakati wakufunzi wa kozi hizo ni Sunday Kayuni na Salum Madadi ambao wanatambuliwa
na CAF. Pia CAF baadaye itatuma Mkufunzi atakayetunga na kusimamia mitihani
hiyo.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment