KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Thursday, May 22, 2014

TANZANIA U15 YAANZA KWA SARE MICHEZO YA AYG.

 Tanzania imeanza Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) inayofanyika nchini Botswana kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mali kwa upande wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 katika mechi iliyochezwa leo (Mei 22 mwaka huu).

Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa SSKB jijini Gaborone ambapo Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 52 mfungaji akiwa Amani Ali. Hata hivyo, Mali walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 61.

Tanzania itacheza mechi yake ya pili kesho (Mei 23 mwaka huu) kwa kuwakabili wenyeji Botswana kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 8 kamili mchana kwa saa za Tanzania. Mechi hizo zinaoneshwa moja kwa moja na kituo cha SuperSport.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Tanzania itacheza mechi nyingine Mei 25 mwaka huu dhidi ya Swaziland, itakuwa tena uwanjani Mei 27 mwaka huu kuikabili Nigeria wakati mechi ya mwisho itakuwa Mei 29 mwaka huu dhidi ya Afrika Kusini.

MBEYA CITY YAENDA SUDAN
Timu ya Mbeya City inaondoka leo usiku (Mei 22 mwaka huu) kwenda Sudan kushiriki michuano ya Kombe la Nile Basin inayoanza kutimua vumbi kesho (Mei 23 mwaka huu) jijini Khartoum, Sudan.

Kikosi cha Mbeya City chenye watu 25 wakiwemo wachezaji 20 kinaondoka saa 2.55 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo kesho (Mei 23 mwaka huu) saa 5 asubuhi kitaunganisha ndege nyingine hadi Khartoum.

Msafara huo wa kikosi hicho ambao utawasili Khartoum saa 7.30 mchana kwa saa za huko unatarajia kurejea nyumbani Juni 5 mwaka huu iwapo timu hiyo itafanikiwa hatua ya mwisho ya mashindano hayo.

Michuano ya Nile Basin imeanzishwa mwaka huu na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), na inashirikisha timu zilizoshika nafasi za pili katika ligi za nchi wanachama wa baraza hilo.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO

SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: