Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa akifurahia jambo na Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho (kulia) na Diwani
wa Viti maalum Ilala Mh.Batuli Mziya (katikati) wakati wa ziara ya viongozi wa
TACAIDS kata ya Gongolamboto.
Mmoja wa wanachama wa Asasi ya Vijana ya St. Camilus inayojihusisha na
utoaji wa elimu kuhusu VVU na Ukimwi kwa vijana kupitia sanaa mbalimbali Bi.
Aquila Mawenya akisoma taarifa ya utendaji kazi wa asasi hiyo kwa Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho alipokutana na wanachama wa Asasi hiyo Kiwalani jijini
Dar es salaam.
Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho (katikati) akiwa
na baadhi ya wanachama Asasi ya Vijana ya St. Camilus inayojihusisha na utoaji
wa elimu kuhusu VVU na Ukimwi kwa vijana kupitia sanaa mbalimbali alipowatembela
eneo la Kiwalani jijini Dar es salaam.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia Mmbando (kulia) akitoa
taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi katika jiji la Dar es salaam kwa
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho
alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo kuangalia hatua zilizofikiwa
katika kupambana na ugonjwa huo katika ziara yake ya siku nne.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala
Bw. Raymond Mushi akitoa tathmini ya hali ya maambukizi ya VVU katika jiji la
Dar es salaam na hatua zinazochuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali kukabiliana na janga hilo mara baada ya kupokea ugeni kutoka Tume ya
Taifa ya Kudhibiti Ukimwi.
Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa ambaye pia ni diwani wa kata ya
Gongolamboto akitoa ufafanuzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho kwa kuhusu
hatua iliyofikiwa na mikakati ya manispaa ya Ilala katika kukabiliana na
maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Baadhi ya viongozi wa manispaa ya Ilala wakiongozwa na Meya wa Manispaa
hiyo Mh. Jerry Silaa (katikati) wakiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho (wa tatu kutoka kulia) alipotembelea Kata ya
Gongolamboto kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo
katika ngazi ya kata.
Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho akikutana na
vijana wa kata ya Vingunguti wa Asasi ya Watoto na Vijana –CAFLO.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma
Mrisho akizungumza na viongozi na wakazi
wa kata ya Gongolamboto jijini Dar es salaam alipotembelea eneo hilo kuangalia
hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo katika ngazi ya kata.
Katibu wa mtandao wa Vikoba vya watu wanaoishi na VVU (IDINEPA VICOBA) kata
ya Kiwalani Bw. Shaban Mwasa Wamikole akimkabidhi risala ya kikundi hicho Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho alipokutana na wanachama wa kikundi hicho katika kata
ya Kiwalani jijini Dar es salaam.(Picha
na Aron Msigwa –MAELEZO).
MAAMBUKIZI YA VVU JIJINI DAR ES SALAAM YAPUNGUA.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Licha
ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi vya
Ukimwi na Ukimwi, Jiji la Dar es salaam limefanikiwa kupunguza kiwango cha
maambukizi kutoka asilimia 9.8 za mwaka 2007/2008 hadi kufikia asilimia 6.9 kutokana na jitihada zilizofanywa na
serikali zikiwemo za uundaji wa kamati shirikishi za mkoa kudhibiti maambukizi
hayo.
Hayo
yamebainishwa katika taarifa ya hali ya
maambukizi ya VVU na Ukimwi iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es
salaam Bi. Terezia Mmbando kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi
(TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo
kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo.
Akisoma
taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Bi. Mmbando ameeleza kuwa janga la Ukimwi
ni tatizo la dunia nzima na limekuwa kikwazo cha maendeleo ya jamii hapa nchini
na kuongeza kuwa jitihada za kudhibiti maambukizi ya Ukimwi jijini Dar es
salaam zimechukuliwa kupunguza maambukizi ikiwa ni pamoja na uanzishaji rasmi
wa kamati za kuratibu na kusimamia shughuli za kudhibiti Ukimwi kuanzia ngazi
ya mkoa, halmashauri, ngazi ya kata na mtaa.
Amesema
jiji la Dar es salaam linakabiliwa na changamoto ya ongezeko la kubwa la watu
ikilinganishwa na mikoa mingine hali
inayochangia mwingiliano wa tamaduni, shughulim mbalimbali, masuala ya
kijamii,kimila na kiuchumi na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na
Makazi 2012 idadi ya watu imefikia
4,364,54, wanaume wakiwa 2,125,786 na wanawake 2,238,755 sawa na ongezeko
la asilimia 5 kwa mwaka.
Hali ya VVU na
Ukimwi mkoa wa Dar es salaam.
Hali
ya maambukizi ya Ukimwi katika jiji la Dar es salaam kwa mujibu wa matokeo ya
utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusu viashiria vya Ukimwi na
Malaria mwaka 2011/2012 inaonesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kitaifa ni
wastani wa asilimia 5.1 ambapo maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.2 na
wanaume ni asilimia 3.8.
Sababu za
maambukizi.
Miongoni
mwa sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU katika
mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na kasi ya ukuaji wa jiji na shughuli za
kibiashara hali inayosababisha mwingiliano wa watu na mahusiano ya kimapenzi
pia baadhi ya wakazi kutobadili tabia licha ya kupatiwa elimu ya kujikinga na
maambukizi ya ya ugonjwa huo.
Sababu
nyingine ni hali ngumu ya uchumi hususani maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa
wakazi wa kipato cha chini,kuongezeka kwa vitendo vya ngono isiyo salama
hususani maeneo yenye nyumba nyingi za kulala wageni, kumbi za starehe,
madangulo na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ya madereva wa magari ya
masafa marefu.
Aidha,
ngoma za usiku zinazokesha hasa maeneo
ya pembezoni mwa jiji zinazoambatana na unywaji wa pombe kupita kiasi na uwepo wa makundi maalum ya watu wanaofanya
biashara ya ngono na wale wanaotumia dawa za kulevya hali inayowafanya
washindwe kutoa maamuzi sahihi ya kujikinga na VVU ni miongoni mwa sababu
zinazochangia maambukizi mapya ya VVU.
Hatua
zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi.
Mkoa
kwa kushirikiana na halmashauri za manispaa na wadau mbalimbali pamoja na mambo
mengine umeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na
maambukizi ya VVU,kuhamasisha upimaji wa hiari wa VVU pia kuongeza nguvu katika
mapambano ya kuzuia maabukizi kutoka mama kwenda kwa mtoto kupitia kliniki za
afya ya uzazi.
Hatua
nyingine ni utoaji wa huduma za tiba na virutubisho kwa wagonjwa, kuwahudumia
watoto yatima na wale wanaoishi mazingira hatarishi pia kutoa mafunzo ya
ujasiriamali na kuhamasisha uundaji wa vikundi vya ujasiriamali kwa wanaoishi
na VVU ili waweze kumudu gharama za maisha na uundaji wa vikundi vya sanaa vya
vijana kwa ajili ya kutoa elimu ya VVU na Ukimwi kwa vijana walio katika
mazingira hatarishi ya maambukizi katika jiji la Dar es salaam.
2 comments:
ni hatua nzuri inayofanywa na TACAIDS nachukua nafasi hii kuwapongeza kwani inawapanafasi kujua nini kinatekelezwa na wadau wake,hongera Dr.Mlisho
Nimeipenda hiyo,italete mwamko katika jamii
Post a Comment