Rais Jakaya Mrisho Kikwete
akisalimiana na Dr Ally Olot, mtafiti wa chanjo ya malaria na kiongozi wa
watafiti wa Ifakara Health Institute (IH) I Malabo, Equatorial Guinea)
walipomtembelea kwenye makazi yake mjini Malabo ambako Rais alikuwa anahudhuria
mkutano wa kawaida wa Umoja wa Afrika. Wengine ni Dr. Mwajuma Chemba ambaye ni Mtalaamu
mratibu wa tafiti za chanjo ya malaria, na Elizabeth Nyakarungu, Mtaalamu wa
maabara, utambuzi wadudu wa malaria).
Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja.
Rais Kikwete aliwapongeza sana
watafiti hao pamoja na taasisi ya IHI kwa kuiletea sifa Tanzania katika fani ya
utafiti nje ya nchi.
Watafiti hao wako Equatorial Guinea
(EG) kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kutoa msaada wa
kitaalamu katika utekelezaji wa mradi wa utafiti wa chanjo ya malaria iitwayo
PfSPZ na kuwafunza wenzetu kuhusu maarifa ya fani hii ya utafiti wa chanjo ya
malaria. IHI ni shirika la utafiti lenye kufanya tafiti za afya nchini Tanzania
lenye uzoefu wa miaka zaidi ya miaka hamsini. Mfano mmoja wa mafanikio yake ni
utafiti uliopelekea vyandarua vyenye dawa kutumika kama moja wapo ya njia za
kujikinga na malaria nchini Tanzania.
Tunafanya kazi pamoja madaktari na
wataalamu kutoka Wizara ya Afya ya EG, shirika lisilo la kiserikali la Marekani
liitwalo MCDI (Medical Care Development International) na Sanaria ambao ndio
watengenezaji wa chanjo hiyo ya malaria.
Mradi huu wa utafiti unagharamiwa na serikali ya EG pamoja na
sekta binafsi za mafuta. Mradi huu wa miaka mitano una lengo la kuchunguza
kuhusu uwezo wa chanjo hiyo kukinga dhidi ya ugonjwa wa malaria. Ushirikano huu
ni mmoja ya mfano wa mashirikano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili
kutafuta njia bora za kukinga maradhi katika jamii. Vilevile ni moja ya
kielelezo kizuri cha jinsi gani nchi za kusini zinaweza kushirikiana katika taaluma
mbali mbali (south south corporation).
Tumepata fursa ya kukutana na Raisi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshima Jakaya Mrisho Kikwete Malabo na
kumueleza kuhusu kazi tunayofanya na changamoto mbalimbali zinazotukuta pamoja
na kutoa ombi kwa mheshimiwa Rais kusahilisha mashirikano kati ya nchi mbili za
Tanzania na Equatorial Guinea kupitia Wizara za Afya na Tume za Sayansi na
technologia za nchi hizi mbili. Hili litafanya utelekelezaji wa mashirikiano
hayo kuwa bora zaidi kwa lengo la kunufaisha nchi zote mbili.
Mashirikiano haya ni fursa ya
watanzania kuwafunza wenzao pamoja na wao kujifunza kutokana na mashirikiano
hayo. Utafiti huo pia utasaidia juhudi za kutokomeza ugonjwa wa malaria kwa
kufanya tafiti zenye lengo la kutafuta chanjo bora ya malaria pamoja na njia
bora za kusambaza chanjo hiyo kwa nchi zote mbili kama itakuwa ni yenye
mafanikio.

No comments:
Post a Comment