Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na wanahabari kulaani kitendo cha kupigwa waandishi. Jambo lingine alilozungumzia ni kuhusu mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wakati akilaani kupigwa kwa waandishi wa habari na askari polisi wakati Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alipokuwa akihojiwa makao makuu ya jeshi hilo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Habari na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (katikati), akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Habari, Abdul Kambaya, Mkurugenzi wa Habari na Uchaguzi, Shaweji Mketo, Yussuf Kaiza kutoka Idara ya Vijana na Pavu Juma.
Wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanachama wa CUF wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Wapiga picha wa vyombo mbalimbali wakichukua tukio hilo.
Dotto Mwaibale
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimelaani kitendo cha baadhi ya polisi kuwapiga wanahabari wakati Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alipokuwa akihojiwa na Polisi Makao Makuu ya Jeshi hilo mapema wiki.
"CUF inalaani kwa nguvu zote kitendo kilichofanywa na polisi cha kuwashambulia wanahabari ni kitendo ambacho hakivumiliki tunaomba askari wote waliohusika kuwashambulia wanahabri hao walikuwa kazini wachukuliwe hatua" alisema Mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba.
Katika hatua nyingine chama hicho kimetoa malalamiko yake kuhusianana na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu.
Kimesema hadi wiki iliyopita kilikuwa na taarifa kuwa uchaguzi huo
utafanyika Februari mwakani baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukamilisha taratibu zote zinazohusiana na daftari la kudumu la wapiga kura, ikiwemo kuwaandikisha wananchi wote hadi ngazi ya vijiji navitongoji.
Akizungumza na waandishi wa habari, kwenye makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa. Ibrahim Lipumba ,alisema hawana taarifa sahihi ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Alifafanua kuwa taarifa walizozipata kupitia vyombo vya habari kuwa iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda siku chache zilizopita,kuwa uchaguzi huo utafanyika Desemba 14, mwaka huu, ingawa walipokutana na Rais Kikwete alisema uchaguzi huo utafanyika Februari mwakani.
Prof. Lipumba, alisema hatua hiyo ilikwenda kinyume na
makubaliano waliyoafikiana na serikali katika Mkutano wa Vyama vya Siasa ulioandaliwa na TAMISEMI Julai 14 mwaka huu mkoani Morogoro kujadili Kanuni za Uchaguzi wa serikali za mitaa.
Alisema katika mkutano huo walikubaliana kuwa uchaguzi huo usimamiwe na NEC kuanzia uratibu na uandikishaji wapiga kura hadi mwisho ikiwa ni suluhisho la muda baada ya Katiba Mpya kuchelewa kukamilika na kutotumika kwenye uchaguzi huo.
Pia alidai walipendekeza madiwani wajumuishwe kwenye uchaguzi waserikali za mitaa kama ilivyokuwa ikifanyika kabla ya mwaka 2000
kwa kuwa ndiye kiongozi wa juu katika ngazi ya Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment