Mkuu wa
Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema akizungumza wakati
wa hafla ya kuwakaribisha waliokuwa wanafunzi wa chuo hicho waliohitimu miaka
iliyopita wakati wa mwendelezo wa
shughuli mbalimbali za chuo hicho kutimiza miaka 50.
Alexander Msofe akizungumza na wahitimu wa miaka ya nyuma wa chuo cha CBE kwa
niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi
wakati wa hafla ya kuchangia maendeleo ya CBE iliyowahusisha wahitimu hao
jijini Dar es salaam.
Isdori
Kwayi, mmoja wa wahitimu wa chuo cha CBE mwaka 1972 akitoa mchango wake kuhusu
namna chuo hicho kinavyoweza kukusanya
fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali ili kuboresha miundombinu yake
wakati wa hafla fupi iliyowahusisha wahitimu wa chuo hicho jijini Dar es salaam.
Baadhi ya
wahitimu wa CBE wa miaka iliyopita wakifuatilia masuala mbalimbali wakati wa
hafla ya kuchangia maendeleo ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam
ambacho kimetimiza miaka 50.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Wahitimu wa vyuo
mbalimbali nchini wameaswa kujenga utaratibu wa kuchangia miradi na shughuli
mbalimbali za maendeleo ya elimu katika vyuo walivyosoma na kuepuka kutumia fedha
nyingi katika kuchangia masuala yasiyo na tija kwa maendeleo ya taifa.
Hayo yamebainishwa jana
jijini Dar es salaam na mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Prof.
Emanuel Mjema , wakati wa hafla ya kuwakaribisha chuoni hapo waliokuwa
wanafunzi wa chuo hicho waliohitimu miaka iliyopita kwenye mwendelezo wa
maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho.
Akizungumza na wahitimu
hao amesema kuwa wanayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu
hapa nchini kwa kushiriki na kutumia sehemu ya mapato wanayopata kupunguza
changamoto za elimu za uhaba wa vyumba vya madarasa, maabara na miundombinu
mingine isiyo rafiki kwa maendeleo ya wanafunzi.
“Elimu ndio msingi wa
maendeleo, sisi tulipata elimu iliyo bora lazima tuchangie kwa sehemu yetu kuonyesha
tunayajali maeneo tuliyosoma, hivi sasa mwamko wa watu wengi uko katika kuchangia sherehe na
harusi lakini kwenye suala la elimu hali ni tofauti” Amesema Prof. Mjema.
Amesema wahitimu hao
wana nafasi kubwa ya kuendelea kuwa mfano kwa kuendelea kutoa mrejesho kwa
uongozi juu ya nini kifanyike katika kuendeleza sekta ya elimu chuoni hapo
sanjali na kueleza mapungufu yaliyopo
pamoja na kutoa michango yao juu ya namna ya kuendeleza kiwango cha taaluma.
Amebainisha kuwa chuo
hicho kinahitaji kiasi cha shilingi bilioni 3 ili kiweze kukamilisha miradi
mbalimbali ya maendeleo ya upanuzi wa kampasi zake, ujenzi wa
miundombinu,uongezaji wa vifaa vya kufundishia, madarasa, maabara na kumbi za
mihadhara.
Kwa upande wake Bw. Alexander Msofe akizungumza
na wahitimu hao kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho ambaye ndiye
alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema
chuo hicho kinafurahia matunda ya mafanikio ya kutimiza miaka 50 tangu
kuanzishwa kwake.
Amewaambia wahitimu hao
kuwa licha ya changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo hicho kimeweza kuongeza
idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwa mwaka kutoka 25 waliodahiliwa mwaka 1965 hadi 14,000 katika mwaka wa masomo wa 2014/15
pamoja na ongezeko la idadi kozi za
masomo zinazotolewa kutoka 1 hadi 6.
Bw. Msofe ameongeza kuwa chuo cha CBE sasa kinatimiza miaka 50
kikiwa chuo pekee Afrika ya Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya
Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya vipimo.
Mafanikio mengine ni
pamoja na kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia
shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu (PhD) chuoni
hapo pamoja na chuo kuanzisha
ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha
Eastern Finland katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia
TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.
Aidha, katika kuelekea tamati ya maadhimisho
ya chuo hicho yatakayofanyika Januari 13, mwaka 2015 ameitaka jamii na wahitimu wote
wa chuo hicho wajitokeze wingi kutoa michango
yao ya hali na mali itakayowezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa na mihadhara,
maabara na vyumba vya kulala wanafunzi.
Kwa upande wao
wanafunzi waliowahi kusoma chuoni hapo wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati
wa hafla hiyo wametoa wito kwa wadau mbalimbali wenye mapenzi mema kujitokeza
kuchangia ukamilishaji wa programu mbalimbali za maendeleo zilizoanzishwa na
uongozi wa chuo hicho.
Wamesema kuwa badala ya
kuiachia serikali pekee jamii na wahitimu hao wanayo nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya chuo hicho
kutokana na wao kuendelea kufaidika na elimu waliyoipata kipindi wakiwa
wanafunzi wa chuo hicho.
Wameiomba serikali
kuhakikisha kuwa inaendelea kukisaidia chuo hicho na kukitumia kupata ushauri
wa kufanikisha masuala mbalimbali yakiwemo mafunzo kwa wafanyabiashara na uimarishaji
wa mifumo ya ukusanyaji wa kodi hapa nchini ili kuondoa tatizo la asilimia
kubwa ya watu kukwepa kodi.
No comments:
Post a Comment