Na Anna Nkinda – Lindi
Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa Kata ya Ng’apa wilaya ya Lindi mjini kuchagua
viongozi waadilifu na wenye sifa ambao watawaongoza wananchi kusimamia shughuli
za maendeleo yao.
Mama Kikwete ambaye ni
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
wilaya ya Lindi mjini alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na wananchi
waliohudhuria mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali
za mitaa uliofanyika katika Kata hiyo.
Mama Kikwete alisema
kuna baadhi ya watu wanachagua viongozi kwa ushabiki pasipo kuangalia kiongozi
huyo kama ana sifa au la, na kuwasisitiza wananchi hao siku ya uchaguzi ikifika wasifuate mambo ya
ushabiki na kuchagua kiongozi kwani ushabiki hauna manufaa yoyote.
“Nawaombeni muwapigie
kura za ndiyo viongozi wote wa CCM wanaogombea
nafasi za Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za Mitaa, kwani hawa wanasifa na mkiwachagua
kutakuwa na manufaa kwenu na vizazi
vyenu hivyo basi wote mliojiandikisha siku
ya uchaguzi ikifika mjitokeze kupiga
kura na kukichagua Chama chetu”, alisema
.
Aidha MNEC huyo
aliwakumbusha wanachama wa CCM siku ya uchaguzi kutokwenda kupiga kura wakiwa
wamevaa sare za Chama au mavazi yoyote yenye kuonyesha ushabiki wa Chama cha
siasa hiyo hairuhusiwi na kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Maadili ya
vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi .
Kuhusu elimu Mama
Kikwete alisema Serikali ya CCM kwa kushirikiana na wananchi imefanikiwa
kujenga shule za Sekondari nchi nzima na
ifikapo mwakani maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi katika shule hizo
zitakuwa zimekamilika na kuanza kutumika.
Alisema, “Ninawaomba
wazazi na walezi msimamie watoto waende shule ili wawe na maisha bora hapo
baadaye kwani tatizo kubwa lililoko hapa
ni watoto kutokwenda shule. Serikali imewajengea shule na maabara lakini kama
watoto wenu hawataenda shule ni kazi
bure, ili shule hizi ziwe na faida kwenu ni lazima watoto wenu wasome”.
Mama Kikwete pia
alitembelea Kata ya Makonde na kuongea na wanachama pamoja na wagombea wa
nafasi za Uenyeviti na Wajumbe na kuwapongeza
viongozi wa zamani ambao wanamaliza kipindi chao cha uongozi kwa kazi kubwa
waliyoifanya ya kutekeleza na kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Aliwapongeza wanawake
waliojitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi jambo ambalo litawawezesha
kuingia katika ngazi ya maamuzi.
Mama Kikwete yupo
wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kichama ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye kampeni na kuwanadi wagombea wa chama
hicho wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali
za Mitaa, Vijiji na Vitongoji utakaofanyika
tarehe 14 mwezi huu.
No comments:
Post a Comment