Mhandisi wa Masafa kutoka
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano nchini, TCRA, Bw Francis Mihayo (kushoto)
akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya tatizo la
kutoonekana vizuri kwa chaneli za ITV na EATV katika king’amuzi cha kampuni
hiyo, kulia kwake akifuatilia kwa makini ni Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Bw
David Kisaka. Katika mkutano huo Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano nchini,
TCRA na StarTimes walitoa ufafanuzi juu ya tatizo linalopelekea tatizo hilo,
mkutano huo uliofanyika leo katika duka la kampuni hiyo lililopo
Mikocheni-Bamaga jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Ufundi wa StarTimes Tanzania, Bw Abdulkadir Mbeo (kushoto) akitoa ufafanuzi
kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya tatizo la kutoonekana vizuri
kwa chaneli za ITV na EATV katika king’amuzi cha kampuni hiyo na kulia kwake
akifuatilia kwa makini ni Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Bw David Kisaka.
Katika mkutano huo Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano nchini, TCRA na StarTimes
walitoa ufafanuzi juu ya tatizo linalopelekea tatizo hilo, mkutano huo
uliofanyika leo katika duka la kampuni hiyo lililopo Mikocheni-Bamaga jijini
Dar es Salaam.
Waandishi wa habari
wakifuatilia kwa makini tukio zima lililotoa taarifa sahihi juu ya tatizo la
kutoonekana vizuri kwa chaneli za ITV na EATV katika king’amuzi cha kampuni
hiyo. Katika mkutano huo Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano nchini, TCRA na
StarTimes walitoa ufafanuzi juu ya tatizo linalopelekea tatizo hilo.
Dar es Salaam, Februari 2015.
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kampuni ya matangazo ya dijitali ya Star Media (Tanzania) Limited wametoa ufafanuzi juu ya matangazo hafifu ya chaneli za ITV na EATV yalianzakuruka kwa wiki moja iliyopita.
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kampuni ya matangazo ya dijitali ya Star Media (Tanzania) Limited wametoa ufafanuzi juu ya matangazo hafifu ya chaneli za ITV na EATV yalianzakuruka kwa wiki moja iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Msaidizi wa Ufundi, Kitengo cha Tekinolojia wa kampuni ya Star Media Tanzania ambao ni wasambazaji na wauzaji wa ving’amuzi vya StarTimes nchini, Mhandisi Abdulkadir Mbeo amesema kuwa, “Wakazi wa Dar es Salaam wamekuwa wakipata tabu kutazama chaneli za ITV na EATV kupitia king’amuzi cha StarTimes kutokana na muingiliano unaosababishwa na mitambo ya masafa ya WiMAX, tatizo hilo lililojitokeza mapema mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu. Hali hii imesababisha usumbufu mkubwa kwa wateja wetu na umma kwa ujumla ambao wamekuwa wakifurahia matangazo yetu tunayoyatoa katika ubora wa hali ya juu.”
“Baada ya uchunguzi wa kutosha uliofanywa na wahandisi kutoka StarTimes kwenye mitambo yao wamegundua kwamba tatizo limejitokeza katika vyanzo vya nje ambavyo ni mitambo ya mawasiliano yenye mfumo wa WiMAX.” Alisema na kuongezea Mhandisi Mbeo, “TCRA kama chombo chenye dhamana ya udhibiti na urushaji wa matangazo ya dijitali nchini ndio chombo pekee kwa ajili ya usuluhishi pindi yanapotokea matatizo kama haya ya kuingiliana kwa mawimbi kwa kampuni zinazohusika.”
“Baada ya kuwasilisha tatizo hilo, timu ya wahandisi wa kampuni ya StarTimes na TCRA walifanya uchunguzi wa kutosha ili kuweza kubaini mitambo hiyo ya WiMAX ambayo imekuwa ikiingiliana na urushaji wetu wa matangazo katika kituo cha Makongo.” aliongezea
“Utafiti ulifanyika kwa makini na majibu yakawa mazuri na yenye kuleta ufumbuzi. Timu iligundua kuwa kuna ufungaji mpya wa mitambo ya WiMAX ambayo inasababisha muingiliano wa mawimbi ya satelaiti yanayopokelewa na dishi la stesheni za ITV na EATV na kusababisha upokeo wa mawimbi hafifu katika dishi linalotumiwa na StarTimes kwenye kituo chake cha kurushia matangazo.”
“Pili, timu ya wahandisi hao imebaini kuwa ufungaji huu wa mitambo mipya ya WiMAX inafanya kazi katika wigo ambao kwenye kiwango cha juu cha Megahatzi 3.598. Mawimbi hayo yapo karibu na satelaiti ya ITV pamoja na EATV kwenye kmiwango cha Megahatzi 3.644 na hivyo kusababisha matatizo ya moja kwa moja kwenye muingiliano wa urukaji wa chaneli hizi. Na mwisho kabisa, mitambo hii ya WiMAX inapokea nguvu ambayo ni kubwa na hivyo kuifanya satelaiti inayorusha matangazo katika mitambo ya Makongo kuchafuka.”
Kutokana na utafiti huo na tafakari ya kina, ni wazi kwamba mawimbi ya WiMAX yaliyogunduliwa katika mitambo ya kurushia matangazo ya runinga kwa njia ya antenna za nje katika kituo cha Makongo inaingiliana na ile ya satelaiti inayorusha chaneli za ITV na EATV na hivyo kupelekea matangazo hayo kuchafuka.
“Lakini katika hali isiyo ya kawaida na bila ya kufanya uchunguzi wa kutosha na kwa kushirikisha uongozi wa StarTimes, stesheni za ITV na Radio One zimetangaza kuwa matatizo hayo yamesababishwa kwa makusudi na kampuni hiyo. Kutoka na taarifa hizo zilizokuwa zikirushwa na vituo vya ITV na Radio One, wateja wetu na watanzania kwa ujumla wamekumbwa na wasiwasi na hofu kubwa juu ya utoaji wa huduma zetu.” Alihitimisha injinia wa kampuni hiyo
Akiongezea juu ya ufafanuzi huo Mhandisi Masafa wa TCRA, Bw Francis Mihayo amebainisha kuwa ni kweli wamepokea malalamiko hayo na mpaka sasa uchunguzi unaendelea ambapo tatizo limekwishagundulika linasubiri kupatiwa ufumbuzi.
“Ni kweli tumepokea malalamiko kutoka kwa kampuni ya StarTimes Tanzania kuwa baadhi ya wateja wao wanalalamika kutoonekana vizuri kwa chaneli za ITV na EATV jambo ambalo linawaletea usumbufu mkubwa na kupoteza imani kwao. Sisi kama mamlaka husika na ambao ndio tunadhamana ya kutoa idhini ya utoaji wa masafa ya urushaji wa matangazo tunaowajibu wa kushirikiana na pande zote mbili ili kulitatua hili tatizo.” Alisema Bw Mihayo
“Ningependa kuwatoa hofu watanzania kuwa uonekaji huo mbovu wa matangazo ya chaneli hizo sio wa makusudi kama inadhaniwa au kutangazwa kwenu bali ni sababu za maingiliano ya mitambo ambayo hivi punde tutairekebisha. Nawaomba muwe na subira kwani lengo ni kuhakikisha kila mtanzania anapata matangazo bora kabisa ya kidijitali.” Alihitimisha mhandisi huyo kutoka TCRA
Naye kwa upande wake Meneja wa Mauzo wa kampuni hiyo, Bw David Kisaka alibainisha kuwa, “Tunapenda kuwatoa hofu wateja wetu na watanzania kuwa StarTimes inongozwa na falsafa makini inayolengwa kumuwezesha kila mtanzania kuweza kupata matangazo ya dijitali kwa gharama nafuu. Hilo ni dhahiri kwani mpaka sasa hatuna mpinzani kwa utoaji wa huduma bora za gharama nafuu zinazopendwa na kila mtu.”
“Hivi karibuni StarTimes imezindua ofa kabambe ya king’amuzi nafuu cha kulipia kwa mwezi cha shilingi elfu nne pamoja na kifurushi kipya cha NYOTA. Huduma hii mpya imewalenga wateja wote hasa wale wa kipato cha chini ambao siku zote wamekuwa wakiamini matangazo ya dijitali ni kwa watu wenye vipato vikubwa.” Aliongezea Kisaka
Bw Kisaka alihitimisha kwa kusema kuwa StarTimes inapenda kuwahakikishia kuwa siku zite imejidhatiti katika kutoa huduma bora za matangazo ya dijitali na kwa bei nafuu. Kwa kulifanikisha hilo, kampuni inafanya jitihada za kutosha kufungua matawi ya kutosha nchi nzima ili kumfikia kila mtanzania. (Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)
No comments:
Post a Comment