Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
11/8/2015. Dar es salaam.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imetangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai
2015 na kusema kuwa umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.4 kutoka
asilimia 6.1 iliyokuwepo mwezi Juni 2015.
Hii
inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa mwezi
Julai 2015 imeongezeka ikilinganishwa na kasi ya upandaji bei ya bidhaa
na huduma iliyokuwepo mwezi Juni mwaka 2015.
Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
salaam amesema kuongezeka huko kumesababishwa na kasi ya upandaji wa bei
ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo
mbalimbali nchini.
Amezitaja bidhaa za vyakula
zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko huo kutokana na upandaji wa bei
katika masoko kwa mwezi Julai 2015 kuwa ni mchele kwa asilimia
27.9,mahindi asilimia 2.3, unga wa muhogo asilimia 9.2, nyama asilimia
4.5, samaki 12.2, na maharage asilimia 5.9.
Kuhusu
Fahirisi za Bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya
bei ya bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi hapa Tanzania,
Kwesigabo amesema zimeongezeka hadi kufikia 158.78 kutoka 158:12 za
mwezi Juni.
Amesema kuongezeka kwa fahirisi za
bei kumechangiwa na ongezeko la bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na
bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo gesi ya kupikia kwa asilimia 3.7,
mafuta ya dizeli 5.9, mafuta ya Petroli ailimia 4.9, unga wa mahindi
asilimia 2.5, ulezi asilimia 2.9, samaki asilimia 4.8, viazi vitamu
asilimia 2.6 na ndizi za kupika asilimia 3.4.
Kwesigabo
amesema uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma za mlaji kwa mwezi Julai , 2015 umefikia shilingi 62 na senti 98
ikilinganishwa na kiasi cha shilingi 63 na senti 24 za mwezi Juni
2015.
“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania
katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Julai ,2015
na umepungua hii ina maana kuwa sasa mtu anahitaji kuongeza ziada ya
shilingi 38 ili aweze kununua bidhaa na huduma sawa na zile alizokuwa na
uwezo wa kuzinunua katika mwezi Juni"
Kwa
upande wa mfumuko wa Bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwezi Julai,
2015 Bw.Kwesigabo amesema kuwa una mwelekeo unaofanana , Kenya umepungua
kidogo hadi kufikia asilimia 6.62 na kutoka 7.03 mwezi Juni 2015 huku
Uganda ikiwa na mfumuko wa Bei wa asilimia 5.4 kutoka asilimia 4.9 za
mwezi Juni, 2015.
No comments:
Post a Comment