Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB
Mkwizu akifungua mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali Mtandao
jijini Arusha.Zaidi ya wataalam wa TEHAMA 500 kutoka Wizara, Idara,
Wakala,Taasisi, Halmashauri wako jijini Arusha kujadili mafanikio na
changamoto za Serikali mtandao.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dk.Jabiri Bakari akitoa
ufafanuzi kuhusu Serikali Mtandao kwa washiriki wa Mkutano wa kwanza wa
Serikali Mtandao unaofanyika katika ukumbi wa AICC jijini Arusha.
Mtaalam wa masuala ya Serikali Mtandao kutoka nchini Singapore,Tan
Kim akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Serikali mtandao kwa washiriki
wa Mkutano wa kwanza wa Serikali mtandao unaofanyika jijini Arusha.
Wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka maeneo
mbalimbali nchini wakifuatilia Masuala mbalimbali wakati wa mkutano wa
kwanza wa mwaka wa Serikali mtandao unaofanyika jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa -MAELEZO
ARUSHA.
Serikali
imewataka watalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
walio katika utumishi wa umma kote nchini kufanya kazi zao kwa
kuzingatia maadili, weledi na ubunifu ili kuwawezesha wananchi kupata
huduma za serikali kwa njia ya mtandao katika maeneo mbalimbali na
kuondoa malalamiko yanayotokana na utoaji wa huduma usiokidhi viwango.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu wakati akifungua Mkutano
wa kwanza wa mwaka wa Serikali mtandao wa Maofisa TEHAMA kutoka Wizara,
Idara,Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Amesema
Watumishi wa umma wasipotimiza wajibu wao kikamilifu wanasababisha
malalamiko kwa wananchi na kuifanya Serikali kushindwa kufikia malengo
iliyojiwekea.
"Ni muhimu wote mtamtambue kuwa
utumishi wa umma imara hujenga serikali na Taifa imara, utumishi wa
kufanya kazi kwa mazoea na kusukumwa hauna tija kwa taifa letu"
Amesema.
Ameongeza kuwa ili kufikia malengo ya
kuimarisha utawala bora na kuongeza tija na ufanisi Serikali imekuwa
ikisisitiza matumizi ya TEHAMA ili kuimarisha mawasiliano ya haraka,
yenye uhakika na salama ndani ya taasisi mbalimbali za Serikali; kuanzia
kwenye Wizara, Mikoa hadi ngazi za Halmashauri pamoja na Balozi
mbalimbali nje ya nchi.
Amefafanua kuwa katika
kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa muhimu na kuimarisha usalama wa
Serikali na raia wake Serikali imeendelea kujenga na kuongeza uwezo wa
kupambana na majanga kwa kutumia teknolojia.
Aidha,
amesema Serikali kwa kutambua mchango wa TEHAMA inaendelea
kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zikiwemo za baadhi ya mifumo
kutokuongea, kutowasiliana na kutobadilishana taarifa kati ya taasisi
na taasisi pia rudufu ya mifumo ambapo kila taasisi inakuwa na juhudi za
kipekee katika kusimika na kutumia miundombinu ya TEHAMA ambayo
ingeweza kutumiwa na zaidi ya taasisi moja pamoja na changamoto ya
mifumo kuwa na viwango vya usimikaji tofauti.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao ( e Government
Agency) Dkt. Jabiri Bakari awali akiwakaribisha Wataalam wa Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano waliohudhuria Kongamano hilo amesema kuwa
katika kuimarisha uwazi na upatikanaji wa Takwimu huria, Serikali
imeendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA ili kuwawezesha wananchi
kupata huduma zinazotolewa na Wizara na Taasisi kwa njia ya mtandao.
Amesema
kuwa Serikali inaendelea kufanya vizuri katika kufanikisha lengo kubwa
la kufikisha huduma kwa wananchi na kuongeza kuwa mpango wa Serikali
uliopo sasa ni kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha taarifa zote za
wananchi kuwa katika sehemu moja.
Akizungumza
kuhusu mkutano huo Dkt.Jabiri amesema kuwa washiriki zaidi ya 500
kutoka taasisi mbalimbali za Serikali watapata fursa ya kujadili
masuala mbalimbali ya ushirikiano katika kutekeleza jitihada za
Serikali Mtandao nchini pamoja na Kutafuta ufumbuzi wa changamoto za
serikali mtandao zilizopo nchini ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na
kijamii.
Aidha, wataalam wa TEHAMA wa Tanzania
waliohudhuria kongamano hilo watapata fursa ya kujifunza kutoka kwa
wataalam wengine wanaohusika na Serikali Mtandao kutoka nchi zinazofanya
vizuri katika eneo la Serikali mtandao zikiwemo India na Singapore.
Ameongeza
kuwa katika mkutano huo mada mbalimbali zitajadiliwa zikijikita katika
usimamizi wa Serikali Mtandao nchini Tanzania, Hali ya miundombinu ya
Serikali mtandao na Utekelezaji wa Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa
uwazi.
Mada nyingine zitahusu uimarishaji wa
uwazi na Mfumo wa Takwimu huria nchini Tanzania na uimarishaji wa huduma
za Serikali kupitia simu za mkononi na mifumo inayotumika kutoa huduma
kwa wananchi.
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa
Arusha Bw.Agostin Mapunda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa
Arusha amesema kuwa Matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali
yamerahisisha utendaji wa kazi na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema
sasa wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali zikiwemo za upataji wa
hati za ardhi kwa haraka zaidi kupitia mifumo ya TEHAMA iliyoanzishwa na
serikali.
Ameongeza kuwa ni vema mabadiliko
hayo yakaendelezwa kutokana na umuhimu wake katika kufanikisha utendaji
wa Serikali, kupunguza muda na kuokoa gharama!
"Tuko
kwenye njia sahihi ya kuufanya utendaji wa Serikali kupata mafanikio
kupitia mtandao, hali hii tunaona imepunguza matumizi na gharama kubwa
waliyokuwa wanaipata wananchi kufuata huduma ambazo sasa zimerahisishwa
kupitia mtandao"
Amefafanua kuwa wananchi sasa
wanaweza kulipia ankara zao za umeme, maji na huduma nyingine kupitia
simu zao za mkononi jambo ambalo hapo awali halikuwepo.
No comments:
Post a Comment