KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Thursday, September 3, 2015

SERIKALI KUENDELEA KUTOA KIPAUMBELE KWA WAHANDISI WAZALENDO.

 Baadhi ya Wahandisi wahitimu kutoka katika vyuo na taasisi mbalimbali wakila kiapo cha utii kwa Taaluma yao mbele ya Kamishna wa Viapo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi yanayoendelea
  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akizungumza na Wahandisi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa Siku ya Wahandisi nchini mwaka 2015 jijini Dar es salaam.
 Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikabidhi vyeti na miongozo mbalimbali ya utendaji wa kazi kwa Wahandisi baada ya kuapishwa nchini
 Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikabidhi vyeti na miongozo mbalimbali ya utendaji wa kazi kwa Wahandisi baada ya kuapishwa nchini
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB) Mara baada ya ufunguzi wa Siku ya Wahandisi nchini  mwaka 2015 leo  jijini Dar es salaam.(Picha/Aron Msigwa -MAELEZO).


Na.Aron Msigwa- MAELEZO.
Dar es salaam.

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuwatumia wahandisi wazalendo waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kutekeleza miradi  ya ujenzi wa miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi kwa mwaka 2015 leo jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kuwa Wahandisi  wanao mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa kuifanya mipango iliyo kwenye karatasi kuwa katika uhalisia unaoonekana kwa macho.

Amesema fani ya uhandisi inagusa maisha ya watu moja kwa moja hasa  sekta ya ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme, majengo,miundombinu ya migodi, hospitali, barabara, viwanda na shughuli nyingine za kihandisi.

"Ni jambo lililowazi kuwa tuna kila sababu ya kujivunia maendeleo na mafanikio tuliyofikia, tuna kila sababu ya kuwatumia na kutoa kipaumbele kwa wahandisi wazalendo ,wahandisi wetu wanaweza" Amesisitiza Balozi Sefue.

Amewataka wahandisi hao kuendelea kuzingatia weledi pindi wanaposimamia  utekelezaji wa miradi ya Serikali ili miradi hiyo iendane na thamani halisi ya fedha za wananchi kwa kuwa  Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miradi hiyo.

"Nawataka muendelee kuzingatia weledi,muwe waadirifu na mfanye kazi kwa bidii ili tufikie malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025,mkumbuke kuwa kazi mnazofanya zinaonekana na watu wote, zikiwa mbaya au  kuwa chini ya viwango watasema tu na mtaonekana hamzingatii taaluma wala viapo vyenu" Amesisitiza.

Amesema toka mwaka 2005 hadi 2015 Sekta ya Uhandisi nchini Tanzania imeweza kuwanufaisha watanzania kwa kuzalisha ajira 256,480 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mzauri kwa kuboresha shule , vyuo na taasisi mbalimbali ili ziweze kuzalisha  wahitimu bora wenye kuhimili ushindani soko.

Aidha, ameziagiza Halmashauri kote nchini kuhakikisha kuwa zinakuwa na wahandisi waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi kabla ya Juni 30, 2016 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika ubora wa wahandisi wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuimarisha ushirikiano uliopo katika sekta ya ujenzi baina Tanzania na  nchi za jirani.

Awali akiongea kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuongea na washiriki wa maadhimisho hayo Naibu Katibu Mkuu,Wizara ya Ujenzi, Muhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa siku hiyo inatoa fursa kwa wahandisi kote nchini kukutana na kubadilishana uzoefu wa kitaalam katika kuleta maendeleo nchini.

Amesema Bodi ya Usajili wa Wahandisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imewezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo nchini Tanzania lengo kubwa likiwa ni kuweka msukumo na msisitizo wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2015, kuangalia changamoto na mikakati ya kukabiliana nzao.

Ameongeza kuwa mkutano huo wa mwaka unafanyika nchini Tanzania kwa mara ya 13  ukizishirikisha baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo  Nigeria,Afrika kusini,Malawi, Kenya na wawakilishi kutoka Norway.

Amefafanua kuwa kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN)  sekta ya ujenzi imetoa mchango mkubwa kupitia wahandisi waliopo nchini kwenye shughuri za ujenzi wa miundombinu, ushauri na usimamizi wa miradi mbalimbali.

Amebainisha kuwa kasi ya Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati inaendelea kutekelezwa kwa kasi kupitia sekta ya ujenzi, viwanda,kilimo, umwagiliaji na  shughuli za migodini.

Ameeeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa wahandisi wazalendo na kuweka mkazo katika kushughulikia changamoto walizonazo ili taifa liendelee kunufaika kutokana na gharama kubwa inayotumika kuwasomesha.

"Serikali inatumia gharama kubwa kuwasomesha wahandisi wetu, ni jambo jema tukiendelea kuweka mkazo ili kuwalinda wahandisi wa ndani na mabadiliko yaliyopo yanayoweza kusababisha wengi wao kutafuta ajira nje ya nchi" Amesema.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB) Muhandisi Steven Mlote ameeleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi nchini yanaambatana na majadiliano ya kina kuhusu shughuli za kihandisi nchini na miaka 15 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Aidha, amesema kuwa ERB imewatambua na kuwapa Tuzo na zawadi mbalimbali wahandisi na wahitimu wa Taasisi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao mwaka 2014/2015 huku baadhi ya wahandisi wahitimu wakiapa kiapo cha utii kwa taaluma yao.

Ameongeza kuwa katiaka kipindi cha siku 2 za maadhimisho hayo kutakuwa  na   maonesho ya kiufundi ya jumuiya za wahandisi wa Tanzania  na taasisi mbalimbali za elimu ya Uhandisi zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Uhandisi na Teknolojia St.Joseph , Chuo cha Ardhi (ARU), Makandarasi ,Kampuni za Ushauri wa kihandisi,Mashirika na makampuni ya kibiashara na taasisi za utafiti.

No comments: