Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe akizungumza wakati wa mkutano.
tunakutana miezi sita baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015 na takribani mwaka mmoja tangu tuzindue rasmi Chama chetu kinachopigania
kujenga siasa na jamii ya Ujamaa wa Kidemokrasia. Aidha, leo tunakutana
tukikaribia mwaka mmoja tangu tuzindua Azimio la Tabora ambapo tulidhamiria kuhuisha
Azimio la Arusha ambalo mwakani linatimiza miaka 50 tangu litangazwe na Chama
cha TANU kule mjini Arusha. Aidha, na muhimu Zaidi, tunakutana miaka miwili
tangu chama chetu kiliposajiliwa rasmi. Nawapongeza Kamati ya Maendeleo ya
Jamii kwa kuandaa maadhimisho ya wiki ya chama kuanzia tarehe 1 Mei 2016.
Tangu tulipokutana Tabora mpaka leo kuna mambo mengi sana
yametokea ikiwemo Uchaguzi Mkuu ambao umewezesha Chama chetu kupata uwakilishi
Bungeni na kuongoza Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji na uwakilishi kwenye
Halmashauri za Wilaya 11 nchini. Chama chetu kimekua na sote kwa pamoja
tujipongeze kwa hatua kubwa tuliyopiga.
Katika kujipongeza kwetu kuna watu mbalimbali ambao kwa namna
moja au nyingine wametusaidia kufika hapa tulipo. Wengine wametangulia mbele ya
haki, akiwemo Ndugu yetu Mzee Estomih Malla aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Fedha na mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini, na wengine katika
ngazi mbalimbali za chama. Viongozi wetu wa chama katika ngazi za kuanzia
matawi, kata na majimbo; katika ngazi ya mkoa na Taifa walijitahidi kwa kadiri
ya uwezo wao kukifanya chama kisonge mbele na kupanda mbegu. Nachukua fursa hii
kuwapongeza wote kabisa na kuwashukuru kwa kazi kubwa mliyofanya. Kwa namna ya
kipekee kabisa nampongeza Mgombea wetu wa Urais, Mama Anna Elisha Mghwira na
Mgombea Mwenza wake Ndugu Hamad Yusuf, kwa kuzunguka nchi nzima kukitangaza
chama chetu na kukiweka katika ramani ya siasa nchini. Kazi haijaisha, lazima
iendelee ili kuweza kutimiza malengo yetu ya kujenga siasa mpya katika nchi
yetu, siasa za masuala na kuachana kabisa na siasa za matukio. Katika uchaguzi
uliopita tulipenda mbegu na ikaota. Kazi kubwa tuliyo nayo sasa ni kuilea mbegu
hii na kuhakikisha kwamba inakua kwa kasi ili hatimaye mwaka 2020 chama chetu
kiweze kuchukua usukani wa kuongoza nchi yetu. Mpango Mkakati
mtakoujadili na kuupitisha leo umeanisha kwa kina namna ya kuilea na kuikuza
mbegu hii.
Timu yetu ya Watendaji wa Makao Makuu ya chama na Vikao vya
Halmashauri Kuu tayari vimepitisha Mpango Mkakati kwa upande wao na
sasa ni zamu ya Mkutano huu wa Halmashauri Kuu kujadili na kupitisha Mwelekeo
wa Chama chetu katika Miaka mitano ijayo. Kama myakavyoona, Kauli Mbiu yetu
mpya inayopendekezwa ni SIASA ni MAENDELEO (Developmental Politics). Tunataka
tujihangaishe na mambo ya wananchi, kero za wananchi, changamoto za wananchi na
kushiriki nao kupata mawajawabu ya Changamoto hizo. Tunataka kila mahala ambapo
Chama chetu kimepata uwakilishi kuongoza tofauti na vyama vingine; kuonyesha
kuwa kweli tunataka kufanya siasa tofauti. Kila Mtaa ambao ACT Wazalendo ina
Mwenyekiti au mjumbe, kila Kijiji ambacho tunaongoza na kila Kata ambayo tuna
Diwani, lazima iwe tofauti kimaendeleo na kiuwakilishi. Kila Mamlaka ya
Serikali ya Mtaa ambayo tunaongoza tuonyeshe tofauti na Mamlaka ambazo wenzetu
wanaongoza. Tujikite kwenye mambo ya wananchi. Ndio Siasa ya Ujamaa inataka
hivyo.
Hali ya Nchi yetu
Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii
Kisiasa
Hivi sasa nchi yetu ina Serikali mpya. Rais ameanza kazi kwa
kasi kubwa katika eneo moja muhimu sana ambalo lilikuwa moja ya msingi mkubwa
wa kuanzishwa chama chetu – kupambana na ufisadi. Rais anaita ‘kutumbua
majipu’. Chama chetu kilimuunga mkono Rais katika hatua ya mwanzo kabisa katika
jambo hili. Ninaamini kuwa bado tutaendelea kumuunga mkono kwani ufisadi ni
kansa na ni lazima kwanza kuizuia isisambae na kisha kuanza kuitibu kabisa.
Hatua ambacho zinachukuliwa sasa na Rais ni hatua muhimu sana katika kuondoa
‘kutogusika’ kwa baadhi ya watu katika nchi yetu. Mnamkumbuka wakati tunazindua
Chama tulizungumzia kuhusu ‘cartels’ -
vikundi maslahi ambavyo vimeshika uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo,
tunasema kuwa bado Rais hafanyi inavyopaswa. Bado Rais anapapasa suala la
Ufisadi. Kuna mambo ya muda mrefu ambayo tunaendelea kama nchi kuyalipia Rais
ameyakalia kimya. Mfano ni suala la Tegeta Escrow. Bado Mtambo wa IPTL upo
chini ya matapeli na kila mwezi Serikali inawalipa matapeli hawa zaidi ya Tshs.
8 bilioni wazalishe au wasizalishe umeme. Hivi ndio vikundi maslahi ama cartels
katika sekta ya Nishati ambavyo bila kuvibomoa Rais ataonekana anachagua katika
vita hii.
Suala la HatiFungani ya dola za kimarekani 6 milioni. Ni kweli
kwamba kuwa kuna watu tayari wamefikishwa mahakamani kwa rushwa ya dola milioni
sita. Lakini Serikali imefisha inaowaita madalali wa rushwa hiyo. Walioitoa
rushwa hiyo Benki ya Standard ya Uingereza haipo mahakamani. Waliopokea rushwa
hiyo maafisa wa Wizara ya Fedha hawapo mahakamani. HatiFungani hii ambayo
Serikali imeanza kulipa riba yake ni ghali mno na imeongeza Deni la Taifa kwa
kiwango cha shilingi 1.2 trilioni bila ya riba. Itakapofika mwaka 2020 ambapo
tutakuwa tumemaliza kulipa deni hili, tutakuwa tumelipa zaidi ya shilingi 1.8
trilioni, shilingi bilioni 600 zaidi! Watanzania zaidi ya 2000 duniani kote
wameweka saini kutaka Taasisi ya Rushwa kubwa nchini Uingereza ( SFO ) kufungua
upya shauri hili na kuitaka Benki ya Standard iwajibike kwa ufisadi huu dhidi ya
nchi masikini kama yetu.
Rais wetu angeongoza Watanzania kukataa mikopo ya namna hii
ambayo inafukarisha nchi ingekuwa ni hatua kubwa sana. Lakini TAKUKURU wanaona
ni sifa kuweka ndani watu kwa bilioni 12 bila kutuwaambia watu watakaofaidika
na bilioni 600 zaidi tutakazolipa katika deni hili. Ndio naama tunasema Rais na
Serikali yake bado hawafanyi ya kutosha katika vita dhidi ya rushwa. Sio suala
la kutumbua majipu tu, ni suala la kuweka mfumo madhubuti ambao utazuia rushwa
kabisa.
Chama chetu cha ACT Wazalendo ni lazima kiendelee kuunga
mkono juhudi zozote za kuondoa ufisadi nchini kwetu. Hata hivyo Chama chetu ni
lazima kiendelee kukosoa Serikali pale ambapo tunapoona mambo hayaendi sawa.
Tusiogope kuikosoa Serikali kwa hoja kwani kukosoa Serikali ni tukio muhimu
sana la kizalendo.
Hivi sasa Wabunge wa vyama vya Upinzani wamesusia Bunge kwa
sababu kuu tatu. Moja ni Bunge kutoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya
Taifa na Televisheni Binafsi, mbili ni Matumizi nje ya mpango wa Bajeti
iliyopitishwa na Bunge na tatu ni Serikali kutokuwa na ‘instruments’ kwa
Mawaziri. Hoja hizi ni hoja za msingi sana. Ni Haki ya wananchi kuona moja kwa
moja namna ya wawakilishi wao wanavyofanya kazi. Censorship ni moja ya dalili
za kujenga udikteta nchini. Kwamba anayepaswa kuonekana moja kwa moja ni mtu
mmoja tu; inakuwa kama Korea Kaskazini hivi! Hili ni jambo ambalo Chama chetu
lazima kiungane na vyama vingine kulikemea kwani ukiliacha hatujui kitafuata
nini. Kwamba Bunge lina studio zake nk, ni jambo la kuhadaa tu wananchi.
Umeshawapa wananchi uhuru wa kuona Bunge moja kwa moja kwa miaka 10, halafu leo
unawanyang’anya? Mwalimu Nyerere alipata kusema “ jambo lolote linalowapa uhuru
wananchi ni jambo la kimaendeleo”. Suala la gharama ni hoja dhaifu mno maana
kampuni huru kama Azam TV na Startv walikuwa wanaonyesha bila hizo gharama za
Serikali. Ni lazima kushikamana na wenzetu katika jambo hili.
Suala la Matumizi kufanyika nje ya Mfumo wa Bajeti ni suala
la kisheria. Bajeti inaongozwa na Sheria mbalimbali kama vile Sheria ya Fedha (
The Finance Act), Sheria ya Matumizi na Sheria ya Fedha za Serikali ( Public
Finance Act). Kuna taratibu za Fedha za Serikali kuhamishwa kutoka fungu moja
kwenda fungu jengine au ndani ya fungu husika. Katika Sheria zote hakuna mahala
Rais amepewa mamlaka ya kuhamisha fungu lolote lile. Hivyo, hoja iliyotolewa na
Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Ujenzi kuongezewa fedha mara 4
zaidi ya fedha ilizotengewa na Bunge ni hoja yenye nguvu sana. Izingatiwe kuwa
Rais alikuwa Waziri katika Wizara iliyoongezewa Fedha hizo. Sio hoja ya
kupuuza. Tukipuuza leo Rais anaweza kuamua kufanya lolote na nchi ikaingia
kwenye taharuki. Lazima tumkatalie ili ajifunze kufanya kazi kwa mujibu wa
Katiba na Sheria za Nchi yetu. Mwalimu Nyerere alipata kusema “ Kuna mambo Rais
akifanya, ya hovyo wananchi wakatae, awe Rais awe Rais square”. Dhana ya
Mamlaka ( Power) ni dhana ngumu sana, ukilamba bila kuzuiwa utaendelea kulamba
tu. Tumzuie Rais kupoka madaraka ya vyombo vingine vya dola. Tumuunge mkono
kutekeleza madaraka yake ya Urais lakini lazima tuhakikishe kwamba haingilii
mamlaka ya vyombo vingine.
Suala la ‘instruments’ ni suala linaloendana na suala la
matumizi kubadilishwa. Kimsingi bila instruments Baraza la Mawaziri lina watu 2
tu – Rais na Makamu wa Rais. Kama Waziri Mkuu hana instruments hakuna Waziri
Mkuu. Kama Mawaziri hawana instruments, hakuna mawaziri. Hivi sasa Serikali ina
mawaziri hewa na hata maamuzi yao ni hewa. Instruments ni jambo la kisheria.
Ndio zinatoa mamlaka kwa Mawaziri kufanya kazi. Hivyo kutokana na kutokuwa na
Instruments kimsingi Rais ni Waziri wa Wizara zote nchini hivi sasa. Natoa wito
kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ahakikishe Mawaziri wanapewa instruments ili
waweze kuwepo kisheria na maamuzi yao yawe ya kisheria. Chama chetu kisikubali
nchi kuendeshwa na mtu mmoja kwa jina la Rais. Nchi yetu inaendeshwe kikatiba.
Hata hivyo nataka kuwaasa Wabunge katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Bunge la 11 lazima liwe tofauti na Mabunge yaliyopita.
Mabunge yaliyopita yalikuwa na kazi ya kupambana na ufisadi kwa sababu Serikali
iliyopita ilionekana kutofanya kazi hiyo vizuri. Bunge lilijipa kazi ya ‘kutumbua
majipu’ na kuilazimisha Serikali kutekeleza Maazimio ya Bunge. Hivi sasa kazi
hiyo ya kutumbua majipu inafanywa na Serikali yenyewe, inafanywa na Rais
mwenyewe. Hivyo Bunge lazima litafute wajibu mpya katika kipindi hiki. Bunge na
hasa wabunge wa upinzani lazima sasa kutazama njia mbadala za kuifanya Serikali
iwajibike. Kwa mfano, ni dhahiri nafasi ya wazi kabisa ni katika kuanisha
mwelekeo wa nchi na kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji. Ni lazima
kubadilika na kubadili aina ya siasa. Tusifanye mambo yanayotarajiwa; kwa mfano
kutoka tu bungeni halafu tunarudi tena. Kama Serikali inaenda kinyume na
sheria, katiba na kanuni, kwa nini tusifanye mikutano ya wananchi, bunge la
wananchi ambapo tunajadili kwa uwazi mambo yanayotusibu. Tunaweza kutumia
vizuri digital technology kuhakikisha ujumbe wetu unafika kwa wananchi bila
kujali kama TBC wanaweka live au la. Ni lazima tuwe innovative katika Siasa.
Tusifanye siasa za kila siku.
Kiuchumi
Serikali imewasilisha mpango wa Bajeti ambapo inatarajiwa
kukusanya na kutumia zaidi ya shilingi trilioni 29 katika mwaka wa fedha
2016/17. Hii ni sawa na asilimia 28 ya Pato la Taifa ambalo sasa ni shilingi
trilioni 98. Hata hivyo kwa fedha zetu za madafu inaonekana ni nyingi sana,
kwani inatokana na kuporomoka kwa shilingi dhidi ya fedha za kigeni hasa dola
ya kimarekani. Hata hivyo ni Bajeti kubwa yenye ongezeko kubwa hasa katika
makusanyo ya ndani na mikopo ya ndani.
Serikali itaongeza wigo wa kodi na hata kufikia wachuuzi
wadogo wadogo kama wamachinga ili kuweza kupata fedha za kutekeleza Lakini pia
Serikali itakopa fedha nyingi sana kutoka nje ya nchi, takribani shilingi
trilioni 2. Aidha, serikali itakopa sana kwenye benki za ndani na hivyo
kufukuzana na wafanyabiashara katika mikopo ya ndani. Haya ni mambo ambayo ni
muhimu kuyatazama katika muktadha mzima wa uchumi wa nchi yetu. Nina mashaka
makubwa sana kama wachumi Serikalini waliikalia vizuri Bajeti ianyopendekezwa
kwani kuna maeneo ambayo yanatia mashaka makubwa.
Kwa mfano, Serikali inasema itaongeza mapato wakati mapato
katika bidhaa zinazoingizwa kutoka nje yameanza kushuka. Kwa mujibu wa Taarifa
ya Benki Kuu ya Mwezi Februari 2016, mizigo kutoka nje katika Bandari ya Dar es
Salaam imeshuka kwa 40%. Katika mazingira hayo na kuzingatia kuwa tunategemea
kodi ya forodha kwa asilimia 30 ya mapato yetu, mapato yatashuka tu. Vilevile
Serikali imeshindwa kuzingatia kuwa Uchumi wa Dunia sasa unashuka na Uchumi wa
Afrika unashuka. Tanzania sio kisiwa na inategemea sana uchumi wa Dunia na hasa
nchi kama China ambapo uchumi wao umeporomoka sana. Chama chetu kiitake
Serikali kuitazama upya Bajeti na kuelekeza fedha za kutosha katika maeneo yatakayowezesha
uzalishaji wa ndani na hasa katika sekta ya kilimo ili kudhibiti kuporomoka kwa
uchumi wa Dunia.
Kijamii
Hali ya wananchi ni mbaya; bidhaa zimeanza kupanda bei kuliko
ilivyokuwa kabla ya uchaguzi. Chama chetu kijadili kwa undani hali ya maisha ya
wananchi na kutoa tamko na mapendekezo ya namna ya kukabiliana na hali hiyo.
Hali ya huduma za afya na elimu bado ni mbaya na hakuna mabadiliko makubwa ya
ubora wa elimu na huduma za afya. Chama chetu kishauri Wabunge kuwatazama
wananchi katika michango yao Bungeni ili Bajeti ya nchi yetu ihangaike na keri
za wananchi.
Hitimisho
Ninawaomba wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama muendelee kuwa
wamoja na tuweze kujenga chama imara chenye kujali shida za wananchi. Tuna
wajibu mkubwa na uwezo wa rasilimali fedha mdogo licha ya kwamba tuna
rasilimali watu kubwa yenye kuweza kuleta mabadiliko. Ninawaomba tusivunjike
moyo bali tutumie kila tulichonacho kujenga chama chetu katika misingi ya
Ujamaa wa Kidemokrasia nchini kwetu. Nawatakia mkutano mwema.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
Jumatatu 25 Aprili
2016.
No comments:
Post a Comment