Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jioni hii kuhusu kuchukuliwa kwa benki hiyo ambayo ilikuwa ikimilikiwa na serikali kwa asilimia 100.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mabenki, Kenedy Nyoni (kushoto), akichangia jambo kwenye mkutano huo. Kulia ni Gavana wa Benki Kuu, Profesa Beno Ndulu.
Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Victoria Msina (kulia), akimkaribisha Gavana Beno Ndulu kuzungumza na wanahabari. Wa pili kutoka kulia ni Kaimu Katibu wa Benki, Mustafa Ismail.
Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi Wapiga picha za habari wakiwa kazini.
Taswira ya ukumbi huo wakati wa mkutano.
Na Dotto Mwaibale.
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imechukua usimamizi wa Benki ya Twiga Twiga Bancorp Limited) kuanzia Oktoba 28- 2016 imefahamika.
Hayo yamebainishwa na Gavana wa Tanzania, Profesa Beno Ndulu Dar es Salaam leo jioni wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu hatua hiyo ya kuchukuliwa kwa benki hiyo ambayo serikali ilikuwa ikiimiliki kwa asilimia 100.
"Kwa mamlaka iliyopewa benki kuu chini ya kifungu cha Sheria namba 56 (1) (g) (i) na 56 (2) (a)-(d) cha Sheria ya mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 benki kuu ya Tanzania imeamua kuchukua usimamizi wa benki hiyo kuanzia tarehe 28 Oktoba 2016" alisema Ndulu.
Alisema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kubaini kuwa benki hiyo ina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 20016 na kanuni zake.
Alisema upungufu huo wa mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki hiyo kutahatarisha usalama wa amana za wateja wake.
Profesa Ndulu alisema kutokana na uamuzio huo Benki Kuu ya Tanzania imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa benki hiyo na imemteua Meneja Msimamizi ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za benki ya Twiga kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa benki kuu.
Alisema pia Umma unaarifiwa kuwa katika kipindi kinachokadiriwa kufikia wiki moja kuanzia siku ya taarifa hii, shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za benki hiyo zitasimama ili kutoa nafasi kwa ajili ya kupanga taratibu za uendeshaji wa benki hiyo.
Alisema Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.
No comments:
Post a Comment