Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kata ya Mabwepande, Abdallah Kunja, akizungumza na mwandishi wa mtandao kuhusu changamoto mbalimbali pamoja na kufungwa kwa zahanati hiyo.
Jengo la Zahanati ya Kata ya Babwepande likiwa limefungwa baada ya huduma za afya kuhamishiwa Hospitali ya mji mpya kwa wahanga wa mafuriko.
Dotto Mwaibale.
WAKAZI wa Kata ya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wameiomba manispaa hiyo kuifungua zahanati yao iliyofungwa kwa muda mrefu ili waondokane na adha ya kufuata huduma za afya mbali.
Wakazi hao walitoa ombi hilo Dar es Salaam jana wakati wakielezea changamoto zao mbalimbali zilizopo katika kata hiyo ikiwemo ya kufungwa kwa zahanati iliyokuwa ikiwasaidia kupata huduma za afya kwa ukaribu zaidi.
Akizungumza na mtandao mmoja wa wakazi wa eneo hilo Lightness Mshondo alisema kufungwa kwa zahanati hiyo na kuhamishiwa mji mpya kwa wahanga wa mafuriko kumezorotesha upatikanaji wa huduma za afya katika eneo lao.
"Tulikuwa na zahanati yetu ya Serikali hapa katika kata yetu lakini Manispaa ya Kinondoni waliifunga na kututaka tuwe tunakwenda kwenye hospitali iliyojengwa ambako wapo wahanga wa mafuriko ambapo ni zaidi ya kilomita tatu kutoka hapa tulipo" alisema Mshondo.
Mkazi mwingine wa eneo hilo Rose Lungwana alisema wamekuwa na changamoto kubwa pale mkazi wa eneo hilo anapokuwa amezidiwa kwa homa, kupata dharura ya kuumia na hasa kwa wajawazito wanapopatwa na uchungu wa kujifungua kutoka hapo usiku kwenda mji mpya kuifuata hospitali.
"Kabla ya kuifunga zahanati hii huduma zote tulikuwa tukizipata hapa ikiwemo ya kujifungua lakini leo hii sisi tusiokuwa na uwezo tukiumwa usiku tunakuwa katika mateso makali ukizingatia jiografia ya hapa Mabwepande sio nzuri kutokana ya kuwa na msitu" alisema Lungwana.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kata ya Mabwepande, Abdallah Kunja alisema suala la kuifunga zahanati hiyo na kuihamishia mji mpya ni changamoto kubwa kwa wananchi wa kata hiyo.
Alisema alishangaa kuona wakati serikali ikihimiza kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi manispaa ya Kinondoni inawaondolea huduma hizo na kuzipeleka mbali" alisema Kunja.
Kunja alisema tayari kupitia kamati ya maendeleo za kata hiyo wamepeleka maombi Manispaa kuomba kuifungua zahanati hiyo.
Alisema zahanati hiyo yenye nyumba mbili za madaktari ilikuwa ikihudumia wakazi wengi wa eneo hilo lakini sasa majengo yake yameanza kuchakaa kwa sababu hayatumiki na baada ya kuondoa vifaa tiba vyote huku madaktari wakihamishiwa katika hospitali iliyopo mji mpya kwa Wahanga wa mafuriko.
Jitihada za gazeti hili kumpata Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Aziz Msuya ili kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba baada ya kupigiwa simu yake mara kadhaa ikawa inaita pasipo kupokelewa.
No comments:
Post a Comment