Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Desemba 2016, amekutana na
kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, Alhaji Aliko Dangote.
Katika mazungumzo hayo, Rais
Magufuli amemhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa serikali ya Tanzania
itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini katika kutimiza
lengo lake la kuwa na Tanzania ya Viwanda.
Rais Magufuli amesema kuhusu
kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote kilichopo Mkoani Mtwara hapakuwa na
tatizo lolote ila kulikuwa na watu
ambao walitaka kujinufaisha
binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya biashara za ujanja kitu ambacho serikali
yake haikiruhusu.
Amemtaka Dangote kununua gesi
moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu
ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.
''Iwapo unataka maelezo yoyote
ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya
kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja
kwa lengo la kupiga dili '' amesema
Rais Magufuli.
Dokta Magufuli amesema Dangote
ametaka eneo dogo ambalo angelitumia kusafirishia
saruji yake wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa shilingi bilioni
43 kitu ambacho hakina uhalisia wowote
bali ni watu ambao wanataka kutengeneza faida kitu ambacho hakiwezekani.
Kwa upande wake mmiliki wa
Kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote ameshangazwa na
baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza
makaa ya mawe toka nje ya Tanzania kitu ambacho amesema hakiingii akilini kwa
sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.
Katika kuthibitisha hilo, tayari Mfanyabiashara huyo ameingiza malori
mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake. Ameongeza kuwa lengo la kufanya
biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia ana lengo la kuisaidia
serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya kuagiza mali ghafi
toka nje ya nchi ambazo zinapatikana
nchini.
Alhaji Dangote amemuhakikishia
Rais magufuli kuwa ataendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania
na kamwe hana nia yoyote ya
kufunga kiwanda chake kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari bali ana
mpango wa kuangalia fursa nyingine zaidi za uwekezaji hapa nchini kutokana na
uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika
hatua nyingine Rais Dkt. John Pombe Magufuli
amuapisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Olonyokie Ole-Sendeka
anayechukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo cha kazi na
kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Wengine walioapishwa na Rais
Magufuli ni Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na
Mifugo (Kilimo), Dkt. Maria Sasabo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Mawasiliano), Dkt. Aloyce K. Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii na Bibi Grace Alfred Martin kuwa Balozi (Mkuu wa
Itifaki).
Jaffar Haniu,
Naibu
Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam.
10 Desemba, 2016.

No comments:
Post a Comment