Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imesema kuwa ina
mkakati mkubwa wa kuhakikisha vipimo vyote muhimu vinapatikana katika Hospitali
za Kanda na Mikoa nchini.
Hayo yamesemwa na
Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Mpoki
Ulisubisya alipokuwa akiongea katika kipindi cha TUNATEKELEZA
kinachorushwa na Televisheni ya Taifa ya TBC1 kwa ushirikiano na Idara ya
Habari-MAELEZO.
“Mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha huduma
zote ziwe karibu na wananchi na pia vipimo vyote vya msingi vipatikane mahali
wananchi walipo kwa mfano tunategemea kuwe na mashine za mionzi ya X ray,Ultra
sound,na vipimo vya Moyo katika
hospitali za Wilaya na pia hospitali zote za kanda zitakuwa na vipimo vyote vya
kirufaa,”Aliongeza Dkt Mpoki.
Aidha amesema Serikali inategemea kuweka wataalamu na
vifaa katika Hospitali za Kanda na Rufaa ambapo kwa sasa kuna hospitali nne za
kikanda ambazo ni KCMC, Bugando (BMC), Taasisi ya Benjamini Mkapa mkoani Dodoma,
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na nyingine ambayo iko katika ujenzi mkoani Mtwara na
pia mkoani Tabora ambazo zote zitakuwa na vifaa na wataalamu waliobobea katika
fani mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali iko bega kwa bega na wadau wa
Afya ambapo katika Halmshauri ambazo hazina Hospitali wataingia mkataba wa
huduma na Hospitali teule ikiwamo za dini na binafsi ambapo wagonjwa watapata
huduma bila matatizo ili mradi wafuate sera tulizoweka pamoja na
kanuni,taratibu na sheria za uendeshaji wa Taasisi hizo ili kuhakikisha
wananchi wanapata huduma zilizo Bora.
Mbali na hayo Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuwa
kila Kijiji kiwe na Zahanati bora ambapo kutakuwa na tabibu, muuguzi na
mfanyakazi wa afya ya jamii.
No comments:
Post a Comment