Na
Daudi Manongi-MAELEZO.
Tanzania inategemea
kupata Megawati 400 za umeme kutoka Ethiopia ikiwa ni moja ya makubaliano yaliyofikiwa
baada ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile
Mariam Desalegn.
Hayo yamesemwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa
akizungumza na vyombo vya habari juu ya makubaliano na mikataba ambayo nchi za
Tanzania na Ethiopia wametiliana saini leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“Tukitaka kujenga
uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na umeme wa kutosha,wenzetu Ethiopia
wametuonyesha njia na mimi nimemuomba Mhe.Waziri atusaidie wataalamu kutoka
nchini kwake ili waje tuwaonyeshe maeneo mbalimbali watusaidie
katika kupata umeme wa uhakika kwa kujenga mabwawa ya umeme ambayo yamesaidia
sana katika kupatikana kwa umeme wa kutosha nchini kwao.”Aliongeza Rais
Magufuli.
Aidha amesema kuwa
kupatikana kwa umeme huo kutasaidia kuleta changamoto kwa shirika la umeme
nchini katika kuwapatia wananchi bei ya chini na hivyo kuleta ushindani katika
upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake
Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn amesema kuwa wana mengi ya
kujifunza kutoka Tanzania kwani nchi hizi mbili zina historia inayofanana na
kuongeza kuwa hakuna haja ya wao kwenda nje ya Afrika kupata uzoefu katika
masuala mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo
kuu la kuja nchini ni kwa sababu anahamini nchi hizi mbili zinaweza kuunganisha
nguvu zake na kuwa nguzo kuu katika maendeleo katika eneo la ukanda wa Afrika
Mashariki na kati.
“Tanzania na Ethiopia
ni nchi ambazo zina ushirikiano mzuri sana,sisi sio washindani bali
tunasaidiana katika masuala mbalimbali kwani tumekuwa katika hatua mbalimbali
za kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini katika hatua zinazofanana,na huu ni
wakati muafaka katika kuimarisha ushirikiano wetu kwa faida ya watu wetu kwa
ujumla”Alisisitiza Mhe.Desalegn.
Aidha amesema kuwa mabadiliko ya kilimo katika nchi zetu ndio msingi wa maendeleo pamoja na utumiaji wa teknolojia bora utasaidia katika maendeleo ya viwanda
vidogo vidogo.
Viongozi hawa
wamekubaliana kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu juu ya namna sekta
mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki, madini
na gesi, elimu na mawasiliano.
Ziara ya Waziri Mkuu Mhe.
Haile Mariam Dessalegn imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza
kuwa wakati umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa
thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
No comments:
Post a Comment