Kumekuwepo na
taarifa iliyoandikwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Clouds Media Group
za Facebook na Instagram ikimnukuu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt.
Grace Magembe akisema kuwa ‘‘Upimaji wa VVU nyumba kwa nyumba sasa
rasmi, mchakato unaendelea na zoezi litaanza rasmi mwishoni mwa mwezi huu“.
Ofisi ya Taifa
ya Takwimu (NBS) kwa mara nyingine, inapenda kutoa ufafanuzi kwamba UKIMWI
HAUPIMWI NYUMBA KWA NYUMBA bali inafanya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya
UKIMWI Tanzania ambapo UKIMWI ni ugonjwa mmojawapo unaopimwa katika utafiti
huu. Aidha, utafiti huu unafanyika
kwenye kaya chache ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze
kuwakilisha kaya nyingine ambazo hazihusiki moja kwa moja. Utafiti huu unajumuisha kaya zipatazo 16,000
ambazo ni sampuli iliyochaguliwa kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara
na Zanzibar na unahusisha watu wazima wasiopungua 40,000 na watoto takribani
8,000.
Kwa Dar es
Salaam, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI utahusisha kaya
zisizozidi 1,000
kati ya kaya 1,000,000
na unatarajia kuanza tarehe 31 Mei, 2017 na kuendelea kwa wiki zisizozidi tatu
(3).
Mbali na upimaji
wa UKIMWI, utafiti huu pia unapima kiwango cha maambukizi ya Kaswende, Homa ya
ini (Hepatitis B), uwepo wa viashiria
vya usugu wa dawa, maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa watu
wanaoishi na VVU (Viral load), wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu wa rika
zote pamoja na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell count).
Aidha, kupima ni hiari na watakaogundulika kuwa na maambukizi, watapata rufaa
ya kwenda kupatiwa matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Ifahamike
kwamba, utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/17 unafanyika
nchini kwa mara ya nne (4) ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa
pili mwaka 2007 na wa tatu mwaka 2011. Hivyo, NBS inapenda kuwatoa hofu Wananchi
kuwa, kufanyika kwa utafiti huu sio jambo jipya na Watanzania ambao wamekuwa
wakipitiwa na utafiti huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia
90 na mpaka sasa utafiti huu umeshafanyika katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na
kwa upande wa Tanzania Zanzibar, utafiti huu umekamilika katika maeneo yote
yaliyochaguliwa.
Utafiti wa
Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania unaendelea kufanyika nchini,
ukisimamiwa na NBS kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania
Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya
Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
No comments:
Post a Comment