Mwenyekiti
wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam Steven Lusinde akizungumza wakati wa hafla fupi ya
uzinduzi rasmi wa utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo walio
kwenye sekta isiyo rasmi iliyofanyika leo jijini hapa.(Picha na Veronica Kazimoto,TRA)
Na
Veronica Kazimoto,
Dar
es Salaam,
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho vya
Wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na
Wamachinga.
Akizungumza
wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Kichere amesema kuwa, utoaji wa
vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo unatokana na marekebisho ya Sheria ya
Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la Bajeti la Mwaka wa
Fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia
vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.
"Baada
ya marekebisho ya Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, zoezi hili la kuwatambua
wafanyabiashara wadogo lilianza kutekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama
vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Idara
ya Uhamiaji", alisema Kichere.
Kichere
alieleza kwamba, TRA kwa kushirikiana na
wadau hao, ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa
Kariakoo jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na
Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo leo hii baadhi yao wamepatiwa
vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi wa
utoaji wa vitambulisho hivyo.
Ameongeza
kuwa, zoezi la kutambua vikundi
mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo na kuwapatia Kitambulisho cha Taifa na
Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi linaendelea kufanyika nchi nzima na kubainisha
kuwa, ili wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo maalum, wanatakiwa kujiunga katika vikundi
vinavyotambuliwa kisheria na Serikali, kuwa na Kitambulisho cha Taifa, kuwa na
Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ya kikundi alichojiunga nacho pamoja na
kuchangia shilingi 10,000.
"Zoezi la kuwatambua
wafanyabiashara wadogo linaendelea kufanyika nchi nzima na vitambulisho maalum
vinavyotolewa kwa wafanyabiashara hao vitadumu
na kutumika kwa kipindi cha miaka mitatu (3). Maelezo ya mfanyabishara mdogo yaliyopo
kwenye kitambulisho hicho maalum ni pamoja na jina na picha ya mfanyabiashara,
jina la eneo analofanyia biashara, Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na Sahihi
ya mfanyabiashara husika", Alifafanua Kichere.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam,Sophia Mjema ameishukuru Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuwatambua
wafanyabiashara wadogo ili waweze kupiga hatua kiuchumi kutoka daraja la chini
hadi la kati na hatimaye kuweza kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa
kodi mbalimbali.
"Lakini
kwanza naomba nimshukuru,Rais John Magufuli kwa hii ndoto yake
ya kuwasaidia wanyonge waliokuwa wanafanya biashara ndogo ndogo kutambulika na
Serikali na kisha waondoke katika hali ya daraja la chini na kufikia daraja la
kati. Nafurahi kuwaeleza kwamba, ndoto
ya Rais imetimia", alisema Mjema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es
Salaam Steven Lusinde amesema kuwa, wamefurahishwa na azma ya Serikali ya
kuwatambua wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi kwa kuwa wamekuwa na
hamu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.
"Sisi
wamachinga tumekuwa na hamu kubwa sana ya kuchangia Taifa letu kwa sababu
tunaamini chochote tunachokiona katika nchi hii bila sisi kuchangia hakiwezi
kwenda", alieleza Lusinde.
Moja
ya majukumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ni kukusanya mapato ya Serikali
sambamba na kutoa elimu kwa walipakodi na watanzania kwa ujumla ili kuongeza
uhiari wa ulipaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yanahitajika
katika kuleta maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake.
No comments:
Post a Comment